Upande wa Mashtaka katika kesi ya mauaji inayomkabili mke wa marehemu Bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita (41), umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa jalada la kesi hiyo lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini(DPP) analifanyia kazi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Mwita amedai kuwa jalada la kesi hiyo lipo kwa DPP analifanyia kazi, kisha atawapatia mrejesho hivyo anaomba kesi iahirishwe.

Hata hivyo, Wakili wa utetezi Omari Msemo kwa niaba ya Peter Kibatala aliutaka upande wa mashtaka kukamilisha kwa wakati upelelezi.

Kutokana na maelezo ya pande zote, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi July 23, 2018 itakapotajwa.

Mbali na Mrita, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ya mauaji namba 5 ya mwaka 2017 ni mfanyabiashara Revocatus Muyela na wote wanakabiliwa na shtaka mmoja la mauaji ya dada yake Erasto Msuya, Aneth Msuya.

Washtakiwa  wanadaiwa kumuua kwa makusudi dada wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Aneth Msuya tukio linalodaiwa kutokea May 25, 2016, maeneo ya Kibada Kigamboni Jijini Dar es Salaam.

By Jamhuri