pg 1Ni vigumu kupata maneno sahihi ya kutumia yakaeleweka kutokana na janga ambalo watendaji wa Serikali walioshiriki katika majadiliano ya kuibinafsisha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL Group) waliliingiza taifa, kwani mkataba wa TBL ni balaa kubwa kwa nchi, baada ya siri kuvuja.

 Nakala ya Mkataba ambayo JAMHURI limeipata, inaonyesha kuwa mwekezaji alitumia ujuzi wa aina kuingiza Serikali mkenge kwani katika mjadala na mkataba wa awali, alikubaliana na Serikali kuwa TBL ingemilikiwa na Serikali kwa uwiano wa asimia 50 kwa 50 ya hisa zote, ila miaka 22 baadaye, Serikali ya Tanzania imejikuta haimiliki hata hisa moja.

 Serikali ya Tanzania ililambishwa asali, na kuanza kumeza mate kabla ya utamu kufika kwenye ulimi, ila mwisho wa siku kilichotokea imepoteza gawio lote ililokuwa inapata kutoka TBL ambapo sasa mwekeazaji anamilikia asilimia 62 ya hisa na wazawa wanadaiwa kumiliki asilimia 38 kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam, lakini hawana sauti yoyote.

 Hii inatokana na ukweli kwamba katika mwaka wa fedha ulioisha, mwekezaji kupitia Bodi ya Wakurugenzi anayoimliki alitangaza kutowapa wanahisa gawio la mwisho kutokana na biashara anayofanya ya kujiuzia bidhaa za TBL kwa bei ya kutupa kwa kampuni dada nje ya nchi na kuhamisha faida kwa nja ya tozo za usimamizi na mrahaba.

 Oktoba 8, 1993, mwaka ambao mkataba ulisaini, mkataba usioonyeshi majina ya watia saini zaidi ya kuona saini zao tu kwa niaba ya Tanzania Breweries Limited na Bevman Services, ndipo kosa lilianzia. Iwapo Serikali ingekuwa makini ingeanza kuutilia shaka mkataba huu tangu mwanzo, ila hilo halikutokea.

Kitu ambacho kingeishitua Serikali, wakati kampuni iliyokuwa inaingia mkataba na Serikali kuingia katika ubia na TBL ni kampuni ya Bia ya Afika Kusini (SAB), Kampuni hii ilitumia kampuni nyingine ya Indol iliyosajiliwa Uholanzi kuingia mkataba na Serikali kama wanahisa wa TBL.

 Maajabu si hayo tu, Kampuni ya Indol iliyoingia mkataba na TBL siyo iliyosimamia mkataba huo, mara tu baada ya kusaini mkataba, siku hiyo hiyo, Serikali ilisaini mkataba mwingine na kampuni ya Bevman Services ya Uholanzi iliyoteuliwa na Indol kuwa msimamizi wa uendeshaji wa TBL.

 Katika utangulizi wa mkataba, kifungu cha 2.1 unasema: “Indol ni chombo ambacho SAB humiliki na kusimamia uwekezaji wa aina mbalimbali nchini Afrika Kusini kupitia kwake.” Maelezo hayo yaliifanya Serikali kufungulia mlango wa wao kuondoshwa TBL.

 

Mitego katika mkataba

 Mtego wa kwanza uliwekwa katika kifungu cha 2.4.1 ambapo Serikali na SAB, ambayo baadaye mwaka 2007 iliingia ubia na kiwanda cha Miller cha Marekani kilichokuwa cha pili kwa ukubwa kwa uzalishaji wa bia duniani kilipolipa dola bilioni 5.5 kama deni lililokuwa linakikabili kiwanda cha Miller, ndipo kampuni hii ilianza kuitwa SABMiller, iliyoendeleza kosa la kimkataba.

 Chini ya kifungu hiki, Serikali bila kuhoji ilikubali Kampuni ya SAB kupitia Indol kuwekeza mtaji wa dola 14,585,000 (Sh bilioni 32 kwa sasa) kwa njia ya ukarabati wa mitambo iliyochakaa ya TBL kwa viwanda vya bia ya Dar es Salaam na Arusha. Pia kilitaka mwekezaji aangalie uwezekano wa kujenga kiwanda kipya Mwanza.

 Wakati huo, TBL ilikuwa na hisa 2,000,000. Serikali ilimtaka mwekezaji kutoa dola 3,500,000 na kwamba kwa kutoa kiasi hicho angepewa hisa 2,000,000, ambazo zingemilikiwa na mwekeazji SAB au Indol au SABmiller kwa sasa.

 Bila kufunga zizi, Serikali ikakublai kifungu cha 5.2.2 kilichomruhusu mwekezaji kuwekeza hadi dola milioni 19, huku akisema angetoa wastani wa dola milioni 5 kwa ajili ya vifaa vya ukarabati.

 Mkataba huo unaizuia Serikali kufanya biashara ya bia katika JAMHURI ya Muungano wa Tanzania nje ya TBL, ila unamruhusu mwekezaji kuleta vinywaji kutoka nje ya nchi au kuzalisha vinywaji vya aina hiyo na kuviuza kwenye soko la ndani kwa maana ya kushindanisha bia za TBL na bia za kimataifa sokoni. Ndiyo maana leo kuna bia kama Castle na nyingine.

 

Nembo za biashara

 Wawekezaji walijiandaa. Walijua kuwa Tanzani hakuna aliyefahamu lolote kuhusu masuala ya haki miliki na biashara ya haki ya umikili wa nembo. Mkataba huu uliainisha nembo zinazomilikiwa na TBL kuwa ni Safari Lager, Crown Lager na Ndovu Lager.

 Ni kutokana na hilo, bia kama Kilimanjaro, bingwa, vinywaji kama konyagi, chibuku na nyingine kwa sasa vimesajiliwa Uholanzi ambapo kila mwaka TBL inalipa si chini ya dola milioni 1 kwa ajili ya matumizi ya nembo hizo.

 Kifungu cha 1.17 cha Mkataba wa Nyongeza, kinamruhusu mwekezaji kusajili nembo za bidhaa za TBL nje ya nchi suala ambalo kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na kampuni ya ActionAid ya Uingereza ni moja ya mikondo ya kuhamishia faida nje ya nchi.

 Kifungu cha 16 cha mkataba huo kiliwapa SAB haki ya kununua malighafi kutoka sehemu yoyote wanakoona inafaa na nafasi hii wameitumia vilivyo. Mkataba katika kifungu cha 22, unaitaka Serikali kupunguza ushuru katika bia, lakini wao wanazidi kuongeza bei hata kabla ya kuongezewa ushuru kama walivyofanya Aprili Mosi, mwaka huu kwa kuongeza bei karibu bia zote kuwa Sh 2500 kwa chupa.

  

Kutumia EPA

Wakati mwekezaji alikuja na mbwembe nchini kuwa angewekeza, akafufua viwanda na kujenga kiwanda kipya cha bia, kifungu cha 23 ndani ya mkataba kiliitaka Serikali kutafuta vyanzo vya mapato ikiwamo mikopo na fedha za wafadhili kwa ajili ya kujenga kiwanda cha Mwanza. Hii pekee ilitosha kuwashitua, lakini hawakushituka.

 Mkataba ulipendekeza tozo za usimamizi na fedha za wafadhili wadau wa maendeleo kama “akaunti ya madeni ya nje (EPA)” zilizokuwa ziantolewa na Wajapani kuwa zingetumika katika shughuli za kukarabati na kuejenga kiwanda kipya cha bia Mwanza.

 Habari za uhakika zilizolifikia JAMHURI katika uchunguzi, zinaonyesha kuwa ingawa mwekezaji amepewa hisa kwa ulioitwa uwekezaji wa mamilioni ya dola hadi akaiondoa Serikali katika hisa za TBL, fedha nyingi zimetokana na mikopo au zilitolewa na Serikali hivyo Serikali ilipigwa changa la macho.

 

TBL ilibinafsishwa ikipata taifa

 Kati ya mambo yaliyomuuma Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni kubinafsishwa kwa Kampuni ya Bia Tanzania. Kampuni hii ilikuwa inatengeneza faida na ilikuwa chanzo kikuu cha mapato kwa Serikali ya Tanzania.

 Hadi inabinafsishwa mwaka 2003, ilikuwa imepata faida kabla ya kodi ipatayo 1,052,482,498.

 Ni katika hali hiyo ya kusikitisha, Serikali ilikubali kuingia mkataba unaotaka mwekezaji ateue Msimamizi wa Mradi (Bevman Services) ambaye naye analipwa wastani wa asilimia 1 ya mauzo yote ya TBL kabla ya kodi. Mwekezaji huyu mkataba unamruhusu kuleta wafanyakazi nchini ambao wanalipiwa nyumba, usafiri, posho, sehemu ya kulala na mwisho wa siku bado wanalipwa mishahara na mwajiri wao kutoka nje ya nchi.

 “Kwa mujibu wa kifungu cha 10 mwajiriwa atakayeletwa nchini (kufanya kazi TBL) masharti ya kuja kwake yataainishwa na Bevman, isipokuwa kwamba:- TBL itapaswa kulipa gharama za usafiri, posho ya kujikimu na matumizi yote iliyotumia Bevman au Afisa aliyeletwa, kwa jinsi itakavyokuwa.

 “Kampuni (TBL) inapaswa kulipa malipo ya hapa nchini ikiwamo kodi ya pango na malazi kulingana na afisa aliyekuja,” inasema sehemu ya 8 ya Makataba wa Huduma ulioingiwa kati ya TBL na Bevman Services. Hapa ina maana gharama hazina ukomo, na huu ni mmoja wa mirija ya kulinyonya taifa kwa njia ya kupunguza kiwango cha kodi itakayolipwa.

 Kwa kuthibitisha kuwa mkataba huu uliigeuza Tanzania shamba la Bibi, Kampuni ya Bevman inayopaswa kulipwa hiyo asilimia moja ya mauzo yote ya TBL kabla ya kodi, imepewa mamlaka haya:

 “Mwisho wa kila robo ya mwaka wa TBL, Bevman inapaswa kubainisha mauzo ya jumla kwa kampuni kwa robo ya mwaka, na ndani ya siku 30 tangu kubainishwa kwa malipo hayo, TBL inapaswa kuilipa Bevman kiwango amabcho ni asilimia 1 ya mauzo yote ya robo ya mwaka (kabla ya kodi),” inasema sehemu ya 10.2 ya Mkataa wa Huduma kati ya Bevman na TBL.

 Kwa maana nyingine, mwaka kama uliopita wa fedha wa TBL ambao mauzo kabla ya kodi yalikuwa zaidi ya Sh trilioni 1.2, Bevman Services amepata Sh bilioni 12 kabla ya tozo nyingine bila kutozwa kodi. Kiasi hiki kingeingia kwenye faida na kutozwa kodi kingeweza kuliingizia taifa wastani wa Sh 2,160,000,000.

 Kifungu cha 10.7 cha Mkataba wa Huduma kinasema: “Kiasi chote cha fedha kinacholipwa na TBL kwa Bevman chini na katika utekelezaji wa mkataba huu… kinapaswa kulipwa bila kuhusisha gharama za ubadilishaji fedha, kamisheni, au makato mengine yanayotajwa na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania… bila kodi ya zuio au kodi nyingine, ushuru, tozo au chochocte kiwacho.”

 Kifungu cha 10.8 kinasema kodi hizo zikitozwa, basi TBL itawajibika kuzilipa yenyewe. Hii ni kinyume na Sheria ya Kodi inayota kila mapato anayopata mtu, kampuni au taasisi yatozwe kodi.

  

Kuajiri wafanayazi wa kigeni

 Mikataba yote iliyotiwa saini na TBL inaitaka Kampuni ya SABmiller kuhakikisa kuwa inafuata sheria za nchi. Wakati mwongozo wa uwekezaji kupitia kituo cha uwekezaji unataka kampuni au taasisi inayofanya uwekezaji nchini kuwa na wafanyakazi wa kigeni wasiozidi watano, vyanzo vya habari kwa gazeti hili vinaonyesha kuwa TBL kuna wafanyakazi wa kigeni 43.

 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TBL, Cleopa David Msuya, katika kujitetea kwa gazeti hili akidhani anaiokoa kampuni hiyo anasema TBL ina wafanyakazi wa kigeni 26, kiwango ambacho ni zaidi ya kiwango kinachokubalika kwa mujibu wa mkataba uliokubali kuheshimu sheria za Tanzania walioingia. Idara ya Uhamiaji imeliambia JAMHURI kuwa kiwandani hapo kuna wafanyakazi 29.

Kifungu cha 10 cha Mkataba huu, kinasema wafanyakazi wanaotumikia TBL kutoka Bevman Services mbali na malipo yaliyotajwa hapo juu, bado wanapaswa kulipiwa wastani wa dola 73,000 kila mfanyakazi kwa mwaka. Kiasi hiki ni sawa na Sh 160,600,000 kwa mwaka kwa kila mfanyakazi. Hivyo kwa kuwa na wafanyakazi 43, TBL inalipa mabilioni. Kiasi hiki sasa kinatajwa kuwa kimeongezeka na kufika dola 88,000 kwa kila mfanyakazi.

 

Mvua ya Mikataba

 Machi 9, 1995 ulikuwa mwaka ambao Serikali ilianza kupoteza umiliki wa TBL. Siku hiyo Serikali ilisaini mikataba sita ambayo kinyume na makubaliano ya mwaka 1993, mikataba hii ilifanya marekebisho makubwa katika mkataba wa awali na kuingiza wanahisa wengine kutokana na mikopo waliyochukua.

 Kinyume na walivyoeleza awali kuwa wangetoa mtaji wa kukarabari mitambo na kuwekeza katika kiwanda kipya cha bia Mwanza, mwekezaji sasa aliamua kuchukua mikopo na kuzipa hisa kampuni zilizotoa mikopo hiyo, hali iliyopunguza hisa za Serikali kidogo kidogo na hatimaye Serikali kubaki na hisa sifuri.

 Siku hiyo mwekezaji alichukua mkopo kutoka Kampuni ya International Finance Corporation wenye thamani ya dola 18,400,000 (Sh bilioni 40). Mkopo huu maelezo ya matumizi yake yanaacha maswali mengi. Kampuni hii ilipewa hisa asilimia 9.6 ya hisa zote za TBL kutokana na mkopo huo.

 Hamu ya mwekezaji haikuishia hapo, alichukua mikopo na kuwapa hisa wakopeshaji kulingana na mkopo waliotoa ambao ni Proporco – Kampuni ya Ufaransa (asilimia 1.8), Kampuni ya Dresdner ambayo ni Benki ya Luxembourg (asilimia 1.6) na Kampuni ya FMO (asilimia 0.8). TBL na Indol nazo zilisaini mikataba miwili tofauti iliyoshusha hisa za Serikali.

 Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa nyingi kati ya kampuni hizo zinamilikiwa na SABMiller au wana hisa ndani ya kampuni hizo, hali ambayo inathibitisha taarifa za uchunguzi za Shirika la ActionAid kuwa kampuni hii ina mchezo wa kujikopesha na kudai riba.

 SABMiller inapojikopesha, mara nyingi imejenga utaratibu wa kudai riba kubwa na hivyo kutumia mwanya huo kuonyesha kuwa inalipa deni, kumbe inajirejeshea kiasi inachotaka bila kulipa kodi katika nchi ilikowekeza.

 

Msuaya atuzwa kwa kazi nzuri

 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TBL, Mzee David Cleopa Msuya (86) ametajwa na vyanzo vya habari kwa Gazeti la JAMHURI kuwa anapewa tuzo na SABMiller kwa kazi aliyowafanyia mwaka 1993 wakati wanashauriana na Serikali kuingia kwenye ubia wa  kuibinafsisha TBL.

 Ukurasa wa 10 na 11 wa Taarifa ya Hesabu za TBL Group unaonyesha kuwa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni hiyo ina wajumbe wa Bodi 23 kati yao wakiwamo Watanzania 12 ambapo mmoja anatajwa mara mbili kwenye Bodi hiyo kutokana na wadhifa wake, kati ya Watanzania hao, Watanzania 10 wameteuliwa na SABmiller kusimamia masilahi yake na wawili tu ndio walioingia kwenye Bodi kutokana na nyadhifa zao serikalini.

Wajumbe wa Bodi ya TBL Group Watanzania walioteuliwa na SABmiller wanaotajwa kupewa masilahi manono na kufumbia macho uozo wa kuajiri wageni wengi kuliko inavyotakiwa kisheria, kufanya ununuzi nje ya nchi, kuruhusu Konyagi kushushwa bei na hivyo Serikali kupata kodi kidogo, kuruhusu malipo ya tozo za usimamizi nje ya nchi nao wametajwa.

Wajumbe hao wanaotumikia SABmiller kwani ndiyo iliyowateua ni, Mwenyekiti wa Bodi, Cleopa David Msuya tangu mwaka 2005, Balozi Ami Mpungwe tangu mwaka 2001, R. Mollel, ambaye mwaka 1997 aliteuliwa na Serikali kuiwakilisha TBL, lakini mwaka 2002 SABmiller ikamteua kuiwakilisha kwenye Bodi na amestaafu ujumbe Septemba, 2014 na Anold Kileo aliyeteuliwa na SABmiller tangu mwaka 1999. Mwingine ni P. J. I. Lasway, Mshauri wa Biashara aliyeteuliwa mwaka 2010.

Watanzania wengine ambao ni wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kutokana na nyadhifa zao kama watumishi wa TBL Group wakati ripoti hiyo inachapishwa Machi, 2015 ni Mwanasheria wa TBL Group, S. F. Kilindo, Mkurugenzi Mtendaji wa TDL (aliyefukuzwa) David Mgwassa, Mkuu wa Idara ya Vinywaji Baridi, K. Suma na Mkuu wa Utumishi, D. Magese.

Watanzania pekee wasio na uhusiano wa moja kwa moja na SABmiller katika Bodi hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Viwanda, Biashara na Masoko, Uledi A. Mussa, aliyeingia kwa wadhifa wake na E. Nyambibo, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, anayeiwakilisha Serikali hadi sasa.

Wachambuzi wa masuala ya biashara za kimataifa, wanasema kwa hali yoyote Watanzanai walioteuliwa na SABmiller kuingia kwenye Bodi na wafanyakazi wa TBL Group wanaoingia kwenye Bodi kwa nyadhifa zao, kwa kila hali hawawezi kutetea masilahi ya Tanzania, bali ya SABmiller iliyowateua kuingia kwenye Bodi.

 Upo uovu mwingi, kwamba vinywaji kutoka Tanzania vinauzwa kwa bei chee nchi za nje, wafanyakazi wa kigeni wanalipiwa dola 88,000 kila mmoja na mwisho wa siku fedha nyingi zinahamishwa kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi.

 Wafanyakazi ndani ya TBL wameiomba Serikali kuingialia kati sakata hili kuokoa fedha zinazotoroshwa kwa nia ya kuongeza kiwango cha kodi na hivyo kuisaidia Serikali kupata mapato makubwa yatakayoboresha huduma za jamii.

 Pia, wanaiomba Serikali kupitia mikataba hiyo kuona kama bado inastahili kuendelea kuenziwa au ikiwa Serikali imeibiwa wahusika watakiwe kulipa kodi sahihi walizostahili kulipa.

 

Mpendwa msomaji, kutokana na uzito wa habari ya TBL hasa mambo yaliyosheheni ndani ya mkataba huu, safu ya SITANII inayoandikwa na Mwandishi Deodatus Balile, itakujia wiki ijayo. Tunaomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza.

By Jamhuri