Lindi

Na Aziza Nangwa

Uongozi wa Hospitali ya St. Walburg’s Nyangao mkoani Lindi umeamua kupeleka huduma za kibingwa za upasuaji wa mifupa baada ya kuona kuna changamoto kubwa ya huduma hiyo kutokana na ajali za pikipiki

na mamba, JAMHURI limeambiwa.

Taarifa zinasema kabla ya kuanza huduma za kibingwa za mifupa, uongozi wa Hospitali ya St Walburg’s Nyangao iliingia mkataba na Taasisi ya Mifupa Muhimbili kusaidia wagonjwa wenye matatizo ya mifupa.

Lengo la hospitali ni kuwasaidia wananchi wa mkoa huo kupata huduma za kibingwa za mifupa badala ya kwenda Dar es Salaam kutibiwa wanapopata ajali.

Katika makala hii JAMHURI lilitembelea hospitali hiyo na kuona huduma za kibingwa za mifupa zinavyosaidia wananchi kutatua changamoto za magonjwa ya mifupa.

Ofisa Utawala wa hospitali hiyo, Charles Laizer, anasema wazo la kupeleka huduma za kibingwa lilitolewa na uongozi wa hospitali baada ya kuona kuna changamoto kubwa ya rufaa kwa wagonjwa wa mifupa.

Laizer anasema wagonjwa wengi waliokuwa wakifika hospitalini hapo kutibiwa walikuwa wamevunjika vibaya kwa ajali na walihitaji huduma ya haraka ya upasuaji wa mifupa.

“Wagonjwa wengi wanaoletwa hapa kwetu wanakuwa wamepata ajali za pikipiki na mamba, tulikuwa tunawaandikia rufaa ya kwenda kutibiwa MOI kwa sababu tulikuwa hatuna wataalamu hao,” anasema

Laizer.

Laizer anasema kabla ya kupeleka huduma hizo uongozi wa hospitali ulipitia lengo la serikali linavyohitaji katika sekta ya afya, ambalo linataka kufikisha matibabu ya kibingwa maeneo ya pembezoni, hasa vijijini ziwe karibu na wananchi.

Anasema baada ya kupitia lengo hilo hospitali iliamua kushirikiana na Taasisi ya Muhimbili ili kuwasaidia wagonjwa na kupunguza rufaa.

“Baada ya kujilidhisha kwamba kuna uhitaji wa huduma hiyo tulikwenda kumuona Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicious Boniface, ambaye alikubali ombi letu baada ya kuona umuhimu wake kwa jamii,” anasema Laizer.

Anasema Dk. Boniface alikubaliana nao haraka kwa sababu MOI walikuwa na wazo kama lao ambalo lilikuwa katika malengo ya kutanua huduma za kibingwa kwenye mikoa mbalimbali.

Laizer anasema baada ya kukubali ombi lao waliingia mkataba na MOI kupeleka madaktari bingwa kila baada ya wiki mbili, kupeleka huduma za kibingwa, sanjali na kuwajengea uwezo madaktari na manesi waliopo hospitalini hapo.

“Kabla ya kuanza kazi ya upasuaji, mkurugenzi alituma wataalamu kwenda kuangalia mazingira ya hospitali, miundombinu na vifaa vya kisasa vinavyohitajika kama vipo. Ndipo walipoanza kazi na sisi,” anasema.

Laizer.

Laizer anasema tangu kusainiwa kwa mkataba huo mwaka 2019, wananchi hasa wa hali ya chini, wamepata huduma hizo kwa urahisi ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwanzo.

“Huduma hii kwa kiasi kikubwa imekuwa mkombozi kwa wananchi wa hali ya chini, kwani kwa kiasi kikubwa ndio watumiaji wa usafiri wa bodaboda kuliko wenye uwezo,” anasema Laizer.

Anasema kuwapo kwa huduma za MOI ni msaada mkubwa kwa serikali na wananchi, kwa sababu kumepunguza msongamano wa kupeleka wagonjwa Dar es Salaam kutoka Kanda ya Kusini.

“Huduma hii imeweza kusimamia ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayotaka kuimarisha huduma za afya kwa wananchi, hasa walioko vijijini. Hii nimeinukuu kutoka katika kifungu cha 83:A cha ilani ya CCM kinachosema: ‘Huduma za afya ni kuhakikisha maisha ya Watanzania wengi wenye vipato vya kawaida yameokolewa kutokana na kuimarishwa kwa utoaji wa huduma za matibabu ya kibingwa hapa nchini’,” anasema Laizer.

Anasema faida nyingine za huduma za kibingwa ni kupunguza gharama za serikali kupeleka wagonjwa nje kupata matibabu ya mifupa kama zitasambazwa kwenye mikoa yote.

Laizer anasema faida nyingine ni kuwaleta madaktari bingwa katika maeneo ya vijijini kuona fursa, kwani kuja kwao katika wilaya na mikoa kutawapatia madaktari nafasi ya kupenda kujishughulisha na kilimo na ufugaji wakati wakiendelea na kazi za kila siku.

“Hii itawafanya vijana wengi kupenda kufanya kazi maeneo ya vijijini badala ya kufanyia mijini pekee, hivyo itakuwa ni njia pekee ya kulipa fadhila kwa jamii,” anasema Laizer.

Anasema mpango huo utasaidia jamii kunufaika na vijana wao kwa sababu walisomeshwa kwa fedha za serikali ikiwamo vijijini ambako hospitali hizo zipo.

Laizer anasema kuwapo kwa mpango huo kumepunguza hatari ya vifo kwa wagonjwa wanaopata ajali na kuvunjika viungo mbalimbali, kwani mwanzoni ilikuwa vigumu kusafiri mgonjwa aliyevunjika kwenda Dar es

Salaam, umbali wa kilometa 570 kwa zaidi ya saa nane.

Laizer anasema tangu huduma hiyo ilipoanzishwa mpaka sasa wamekwisha kuwafanyia upasuaji wagonjwa 445, ambapo mwaka 2019 waliwafanyia upasuaji wagonjwa 135 chini ya madaktari wanane kutoka MOI na mwaka 2020 waliwafanyia wagonjwa 310 chini ya madaktari 22 kutoka katika Hospitali ya MOI waliposhirikiana na madaktari wa St Walburg’s Nyangao.

“Kwa sasa tumeanza kuwapeleka shuleni baadhi ya madaktari na manesi kupata ujuzi wa kutoa huduma hizo na za dharura. Madaktari wetu kwa sasa tayari wana ABC ya utoaji huduma za kibingwa za mifupa ambazo walipewa na madaktari wenzao kutoka MOI,” anasema Laizer.

Baada ya mpango huo kuanza walifanikiwa kuwavuta wadau mbalimbali kutoka nje ya nchi kushirikiana na wa ndani ili kuwawezesha kupata vifaa vya kisasa, ukarabati wa jengo la upasuaji na nyumba za watumishi.

Matarajio ya baadaye ya hospitali ni kuongeza madaktari wa mifupa, watoto na usingizi, japokuwa tayari serikali imekwisha kuwaleta baadhi yao na wafanyakazi wengine.

Aliwataja watumishi wanaotarajia kuwa nao hivi karibuni ni madaktari bingwa wa moyo, pua, upasuaji wa jumla na mifupa ili huduma zote za kibingwa zifanyike hospitalini hapo.

Laizer anasema hospitali kwa kuona umuhimu wa kufanya kazi kisasa, katika kitengo cha kompyuta tayari wamekwisha kuleta wataalamu kutoka nje ya nchi kushirikiana na wa ndani kufunga mitambo ya kisasa ya

kompyuta itakayorahisisha utendaji kazi na utoaji huduma haraka.

Anasema mkakati mwingine ni kujenga miundombinu imara kwa ajili ya huduma za dharura, wodi ya pekee, sanjali na nyumba za wafanyakazi.

Laizer anasema ni vema serikali iendelee kuwawezesha ili iwe rahisi kwao kutoa huduma, hasa za kiuchunguzi, maabara, mionzi, dawa na vifaa tiba, ambapo upatikanaji wa vyote hivyo utaifanya Hospitali ya St. Walburg’s Nyangao kuwa msaada kwa wakazi wa Mkoa wa Lindi.

Hospitali hiyo kwa sasa imekuwa mkombozi kwa mikoa ya Mtwara, Ruvuma na nchi jirani ya Msumbiji. Wagonjwa wa matatizo ya mifupa wamekuwa wakipenda kutibiwa St. Walburg’s Nyangao kwa sababu ya ubora wa huduma.

Zuwena Abdalah, Kaimu Muuguzi Mkuu anasema majukumu yake ni kuhakikisha anapokea wagonjwa mbalimbali wanaoletwa hospitalini hapo na kuwaingiza kwenye orodha kwa ajili ya kuwaona madaktari.

Zuwena anasema baada ya hapo anapitia wodi zote walizolazwa wagonjwa ili kuona kama kuna mgonjwa mwenye changamoto na kutoa ripoti kwa uongozi.

Dk. Fausta Liundi ni daktari bingwa wa upasuaji anayesema kazi yake kubwa ni kufanya upasuaji kwa wagonjwa wa aina zote wanaofika kutibiwa isipokuwa mifupa.

Dk. Fausta anasema hulazimika kuingia OPD kuangalia kama kuna mgonjwa anahitaji kufanyiwa upasuaji, ahakikishe ni wa aina gani ili aweze kumpangia siku na muda wa kufanyiwa upasuaji iwapo amekamilisha vipimo.

Dk. Fausta anasema ujio wa madaktari bingwa wa mifupa kutoka MOI umewapa msaada mkubwa, kwa sababu umeongeza idadi ya wagonjwa wanaotibiwa mifupa katika hospitali yao.

“Faida nyingine ni kwamba wametupa elimu ya utoaji wa huduma za mifupa, kwani kuelewa moja kwa moja ni lazima uende darasani,” anasema Dk. Fausta.

Anasema kwa siku wanahudumia wagonjwa kati ya 12 mpaka 14, kutegemea na wingi wa wagonjwa. Anasema kwa kushirikiana na wenzake wanafanya upasuaji siku zote, isipokuwa siku za wikiendi, labda kama kuna dharura. 

Justine Chilumba, Muuguzi Mkuu na Nesi Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji anasema mgonjwa akishafika katika kitengo chake lazima ahakikishe anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa aina gani ili iwe rahisi kumwandaa.

“Hapa tuna vyumba vitatu, kimoja ni maalumu kwa ajili ya mifupa, vingine vya upasuaji mchanganyiko,” anasema Chilumba.

Anasema baada ya hapo anaangalia vipimo vilivyoandikwa na daktari kama mgonjwa amekwisha kupimwa, kisha anaangalia aina za vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya upasuaji.

Chilumba anasema changamoto kubwa kwa sasa ni upungufu wa manesi kwa ajili ya kuweka zamu ya kufika   hospitalini, hali inayowalazimu kwenda kazini kila siku.

Anaiomba serikali kuwapatia wauguzi wanne wenye ngazi ya certificate of medical attendant, ili kuondoa upungufu huo na kuwapa nafasi ya kupumzika badala ya kuwa kazini kila siku.

Dk. Tito Lazaro kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili anasema kazi ya kwenda kufanya upasuaji kwa wagonjwa wa mifupa ilianza mwaka 2019 baada ya hospitali hiyo kupeleka pendekezo kwao la kutaka huduma zao ziwepo katika Mkoa wa Lindi.

Dk. Lazaro anasema baada ya kuingia mkataba na hospitali hiyo, taasisi yao imekuwa ikipeleka madaktari bingwa kila baada ya wiki mbili kufanya huduma ya upasuaji kwa kushirikiana na madaktari wa St. Walburg’s Nyangao.

Anasema kwa sasa wagonjwa walio wengi ni waliovunjika kwa pikipiki. Wananchi wengi hasa wa hali ya chini wamekuwa wahanga wakubwa wa ajali kutokana na kutegemea usafiri huo kwa asilimia kubwa, hivyo ni vema serikali ikaweka mikakati ya kuwadhibiti waendesha pikipiki wazembe wanaogharimu maisha ya watu kila siku.

“Kwa hapa wagonjwa ninaowapokea wengi ni waliopata ajali za pikipiki wakavunjika miguu au mikono na waliojeruhiwa na mamba,” anasema Dk. Lazaro.

Anasema tathmini ndogo iliyofanywa inaonyesha kunakuwapo na idadi kubwa ya wagonjwa msimu wa mavuno na idadi inakuwa ndogo kipindi cha kilimo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa (MOI), Dk. Respicious Boniface, anasema taasisi yake iliona changamoto za watu wa Kanda ya Kusini ni kubwa hasa za huduma za matibabu ya kibingwa ya mifupa, hivyo ikaamua kuwasogezea huduma karibu.

Dk. Boniface anasema kusogezwa kwa huduma zao kwenye Hospitali ya St.Walburg’s Nyangao mkoani Lindi ni moja ya mikakati yao katika kutanua matibabu ya kibingwa ya mifupa katika Kanda ya Kusini ndiyo maana hata

walipopata ombi la kutoa huduma hizi walikubali haraka.

Anasema huduma za kibingwa zilianzishwa katika hospitali za St Walburg’s Nyangao, Lindi na St Benedict Ndanda, Mtwara kwa lengo la kupunguza rufaa na vifo kwa wananchi wa kawaida, vilivyokuwa vinatokea kwa kukosa huduma za haraka za matibabu ya mifupa katika Kanda ya Kusini.

“Tangu tuanze huduma za kibingwa za mifupa katika Kanda ya Kusini tumeweza kupunguza msongamano wa wagonjwa kuja MOI, lakini pia madaktari wetu wameweza kuwajengea uwezo wenzao wa Nyangao na Ndanda,” anasema Dk. Boniface.

Dk. Boniface anasema huduma za kibingwa zinazotolewa na MOI kwa kushirikiana na madaktari katika mikoa ya Lindi na Mtwara, zimekuwa kinara na mkombozi kwa wananchi wa hali za chini waliokuwa wakishindwa kumudu gharama za kupeleka wagonjwa Muhimbili.

Anaongeza kuwa taasisi yake imekuwa ikitoa madaktari bingwa kila wiki wakibadilishana kwa ajili ya kwenda kuwajengea uwezo madaktari na manesi wa kanda hiyo ili waweze kutoa huduma kwa siku za usoni bila kuwategemea madaktari wa MOI.

Dk. Boniface anasema huduma za kibingwa zilikuwa zinahitajika katika kanda hiyo ili kupunguza rufaa za kuja MOI. Tangu huduma hizo zilipopelekwa St. Walburg’s Nyangao, imekuwa kinara na mkombozi katika utoaji huduma za kibingwa hasa katika eneo la mifupa.

“Lengo la taasisi ni kupanua huduma za kibingwa za mifupa katika kanda zote ili madaktari waliopo katika maeneo hayo waweze kufanya tiba za kibingwa katika maeneo yao badala ya kuwapa wagonjwa rufaa,” anasema Dk. Boniface.

Dk. Boniface anasema mpango huo ni kuwaondolea gharama kubwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya kibingwa katika hospitali hizo. Ndiyo maana taasisi imeridhia kutoa madaktari bingwa kwenda kwenye hospitali za Kanda ya Kusini kutoa tiba za kibingwa za mifupa.

Anasema kwa sasa MOI inaona umuhimu wa kuwapatia elimu ya kuwajengea uwezo na mafunzo ya kutosha madaktari na manesi wa kanda katika baadhi ya mikoa ili iwe rahisi kwao kuwakusanya wagonjwa na kuwapatia tiba za mifupa huko huko.

Dk. Boniface anasema mpango uliopo sasa umepunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa kwa rufaa MOI kutoka katika mikoa mbalimbali nchini.

“Programu ya kuwafundisha madaktari ilikuwa ya mwaka mmoja, lakini tulivyoona huduma inakwenda vizuri, tuliamua kuongeza muda zaidi ili kuwajengea uwezo madaktari na manesi wengi zaidi kuhusu kuhudumia wagonjwa wa mifupa katika hospitali za Kanda ya Kusini,” anasema Dk. Boniface.

Dk. Boniface anasema mbali na kupeleka huduma hizo katika Kanda ya Kusini, wana mipango ya kutanua huduma za kibingwa za mifupa katika kanda mbalimbali nchini ili kupunguza rufaa katika mikoa hiyo.

By Jamhuri