Mo Dewji aendelea kukimbiza utajiri Afrika Mashariki, yumo 20 bora AFRIKA

Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Jarida la Forbes limemtaja mfanyabiashara Mtanzania, Mohammed Dewji (Mo) kuwa miongoni mwa matajiri vijana zaidi katika kipindi cha miaka 10 mfululizo akishika nafasi ya 12 Afrika mwaka 2024.

Tajiri huyo kijana ameajiri zaidi ya watu 40,000 katika kampuni na biashara anazoziongoza na kuzimiliki.

Mo ambaye ni mmiliki wa biashara mbalimbali Afrika na duniani kwa ujumla ikiwemo kampuni ya Mohamed Enterprises Limited (MeTL) ametajwa na jarida hilo kupanda katika nafasi za utajiri afrika kutoka 15 hadi 12.

Aidha jarida hilo maarufu na la kuaminika kwa upande wa habari za utajiri wa watu duniani limesema utajiri wa Mo umepanda kutoka Dola za Marekani 1.5 bilioni (Sh3.77 trilioni) mwaka uliopita hadi Dola 1.8 bilioni (Sh4.52 trilioni).

Kulingana na takwimu hizo Mo anakuwa tajiri namba moja Afrika Mashariki. Pia jarida hilo limemtaja Mo kuwa bilionea pekee aliyetia saini ahadi ya kutoa angalau nusu ya utajiri wake kwa ajili ya misaada mwaka 2016.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kwa ujumla ukwasi wa mabilionea 20 wanaoongoza Afrika uliongezeka kwa Dola 900 milioni (Sh2.26 trilioni) na kufika Dola Sh82.4 bilioni (Sh207.23 trilioni) mwaka 2024.

Upimaji wa ukwasi wa watu uliofanywa na Forbes uliangalia gharama halisi kwenye masoko ya mitaji na viwango vya kubadilishia fedha vilivyopo sokoni hadi Januari 8, 2024.

Hata hivyo, katika orodha hiyo ya matajiri Aftika, nafasi ya kwanza inashikiliwa na Aliko Dangote kutoka Nigera akiwa na utajiri wenye thamani ya Dola bilioni 13.9 (Sh34.96 trilioni) akifuatiwa na familia ya Johann Rupert yenye utajiri wa Dola bilioni 10.1 (25.4 trilioni).

Pia, nafasi ya tatu ikishikwa na familia ya Nicky Oppenheimer yenye utajiri wenye thamani ya Dola bilioni 9.4 (Sh23.6 trilioni).