Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa viongozi wa vyuo hapa nchini kuchukulia kwa umuhimu jukumu la kuandika na kuielezea vema Tanzania katika vitabu kwa maslahi ya taifa.

Makamu wa Rais ametoa wito huo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waandishi pamoja na Wadhamini wa Kitabu cha “Continuity with vision – The Roadmap to success for President Samia Suluhu Hassan” wakiongozwa na Mhariri Mkuu wa Kitabu hicho Prof Ted Maliyamkono , mazungumzo yaliofanyika leo tarehe 28 Januari 2023 Ikulu Jijini Dar es salaam. Amesema ni vema kuendelea kuwapa moyo wasomi wa nchi hii ili kutambua kwamba wanao wajibu wa kufanya tafiti na kuandika mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisayansi katika taifa letu.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akikabidhiwa kitabu cha “Continuity with vision – The Roadmap to success for President Samia Suluhu Hassan” na Mhariri Mkuu wa Kitabu hicho Prof Ted Maliyamkono mara baada ya mazungumzo yaliofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam leo tarehe 28 Januari 2023.

Pia Makamu wa Rais amewaasa watanzania kuendelea kujenga tabia ya kusoma vitabu pamoja na kuandika mazuri ya Tanzania kuanzia ngazi ya chini ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kwa kuandikwa na watu wa mataifa mengine.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewapongeza wadhamini wa Kitabu hicho ambao ni Benki ya CRDB na AFRICAB na kutoa wito kwa wafadhili wengine kujitokeza kuchangia katika kuweka kumbukumbu za taifa ikiwemo kumbukumbu za viongozi waliopita na waliopo madarakani pamoja na mabadiliko mbalimbali yanayofanyika.

Katika Hatua nyingine, Makamu wa Rais ametoa wito kwa vyombo vya Habari hapa nchini kuendelea kujielekeza katika masuala ya maendeleo ikiwemo kuwatembelea wananchi mbalimbali wabunifu na wanaoanzisha viwanada na ujuzi mbalimbali. Amesema vyombo vya Habari vinayo nafasi ya kurekebisha jamii hususani katika masuala ya uhifadhi wa mazingira pamoja na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kitabu cha “Continuity with vision – The Roadmap to success for President Samia Suluhu Hassan” kinaangazia uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan namna alivyopokea na kuendeleza sera za maendeleo na miradi ya kimkakati kwa maono na busara kutokana na hali halisi ya nchi ya Tanzania na Ulimwenguni kwa ujumla.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na Waandishi pamoja na Wadhamini wa Kitabu cha “Continuity with vision – The Roadmap to success for President Samia Suluhu Hassan” wakiongozwa na Mhariri Mkuu wa Kitabu hicho Prof Ted Maliyamkono walipofika kukabidhi kitabu hicho kwa Makamu wa Rais leo tarehe 28 Januari 2023 Ikulu Jijini Dar es salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Waandishi pamoja na Wadhamini wa Kitabu cha “Continuity with vision – The Roadmap to success for President Samia Suluhu Hassan” mara baada ya mazungumzo yaliofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam
Please follow and like us:
Pin Share