Mkuu wa Mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere amewataka wakuu wa wilaya, wakurugenzi pamoja na wakuu wa idara za mazingira kila mmoja kuhakikisha miti inapandwa kama muongozo unavyoelekeza.

Hayo ameyasema wakati wa uzinduzi wa zoezi la upandaji miti mkoani hapa na kuagiza kila mwananchi kuhakikisha anapanda mti na kuutunza katika eneo lake.

Uzinduzi huo umfanyika katika kitongoji cha Sumbi, kijiji cha Nakwa kata ya Bagara Halmashauri ya mji wa Babati.

Mkuu wa mkoa amesema Mkoa wa Manyara utaendelea kusimamia vyema jitihada za Serikali katika kutunza mazingira na kuweka msisitizo wa uhifadhi wa mazingira kwa wananchi wote ili kuendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kuhamasisha upandaji miti kwa kupanda katika maeneo ya ofisi za umma kama shule, hospitali, vituo vya afya na zahanati.

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeendelea kuratibu utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya upandaji na utunzaji wa miti inayotekelezwa nchini ambapo kila Halmashauri inapaswa kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.

Kaulimbiu ya mwaka huu inasema Mazingira yetu, Tanzania Yetu, Nitaipenda daimaā€¯ kauli hiyo inatabananisha kuwa uzuri wa nchi ni sambamba na kupanda miti na kutunza mazingira kwa ujumla.

By Jamhuri