Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Bagamoyo
Imeelezwa kuwa mabadiliko ya tabianchi yamechangia kuwepo kwa mwingiiliano wa wanyama na binadamu na kusababisha kuibuka kwa migogoro.
Hayo yamebainishwa na Dk Elikana Kalumanga kutoka RTI International ambaye ni Meneja wa Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari za mazingira na uhifadhi ambao ni wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET).
“Mabadiliko tabianchi ni chanzo kimojawapo ambacho kimechangia binadamu kuingia kwenye maeneo ya wanyama na kusababisha kuwepo kwa mwingiliano ambao husababisha mgongano katika njia za wanyama,” amesema Dk Kalumanga.
Ameongeza kuwa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unatekelezwa katika shoroba saba ambazo ni Kwakuchinja inayohusua Tarangire na Manyara, Msitu wa Amani na Nilo, Udzungwa na Hifadhi ya Nyerere, Ruaha Rungwa na Katavi, Ruaha Rungwa na Inyonga na Kigosi Moyowosi- Burigi Chato.
“Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili umekuwa na mafanikio makubwa katika maeneo husika kutokana na kuwepo kwa mwamko kwa wadau wengine kuelekeza nguvu kwenye shoroba zingine” amesema.
Amesema pia mradi huo umeangalia eneo la mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa na athari kubwa katika baadhi ya maeneo na tayari umeonyesha mafanikio kwa kipindi cha miaka miwili ya utekelezaji katika maeneo husika.
Aidha, Kalumanga amesema pia mradi huo umeangalia eneo la mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa na athari kubwa katika baadhi ya maeneo, hali ambayo inachangia mwingiliano wa wanyama na binadamu kuongezea kutokana na kutafuta mahitaji, hivyo migogoro kuongezeka.
“Tumeweka mkazo pia kwenye kupambana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kuhifadhi misitu na kupanda miti mipya ambayo itawezesha kukabiliana, huku tukihakikisha wananchi wanafaidika kwa sasa na vizazi vijavyo,” amesema.
“Elimu kwa jamii itasaidia kupunguza migongano kati ya wanyama na binadamu kwani shoroba zina fursa nyingi hivyo tunapaswa kuzitunza ili zichangie uchumi na maendeleo,” amesema.
Naye Ofisa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS), Ruben Magandi amesema kuwa, TFS inashiriki kutunza na kuendeleza shoroba hasa kwa kuhamasisha katika upandaji miti.
“Sisi tunashirikiana na taasisi zingine za kisheria na za usimamizi wa maliasili zilizopo kwenye shoroba mbalimbali na tumeona mwamko ni mkubwa kwa jamii kushiriki,” amesema.
Amesema ili kuhakikisha shoroba zinakuwa endelevu ni jukumu la kila mdau kulinda na kuhifadhi mimea ambayo ipo hatarini kutoweka.
Ametaja mimea ambayo ipo hatarini kutoweka ni Mpingo, Msandali na Mkurungu ambayo ina mchango mkubwa katika uhifadhi na mazingira.
Magandi amewataka wadau wote wa uhifadhi kushiriki kutunza misitu na kupanda miti ya asili na matunda kwenye maeneo yao ili kujiongezea kipato.
Aidha, Magandi ameainisha changamoto ambayo wanakutana nayo katika uhifadhi ni baadhi ya watu kuvamia misitu kwa ajili ya kilimo, kukata mikaa na shughuli nyingine kinyume cha sheria.
Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa JET, John Chikomo amesema kuwa ili kupunguza changamoto hizo, ni vyema waandishi wa habari wakaelimisha jamii kuhusu faida na hasara za utunzaji mazingira katika kulinda shorona na misitu.
” JET kwa kushirikiana wadau mbalimbali ikiwemo RTI wanaosimia Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili wamekuwa wakiratibu mafunzo na kuwezesha waandishi kwenda kuona na kuandika habari za uhifadhi wa shoroba ambapo matokeo yake yamekuwa mazuri,” amesema.
Chikomo amesema kuwa ni mwaka wa tatu tangu kuanza kwa uekelezaji wa mradi huo na kumekuwa na mafanikio, hivyo ni vyema waandishi wakaelimisha jamii kupitia kalamu zao ikiwa ni pamoja na kuongeza nguvu katika uandikaji habari kuhusu faida za utunzaji misitu.