Suzy Butondo, JamhuriMedia, Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme amewataka wazazi na walezi kuwalea watoto katika malezi bora, na kuwapa lishe bora, ikiwa ni pamoja na kuwasalimia watoto wakiwa tumboni ili wakue wakiwa na afya njema na akili.

Pia amewataka wadau wa maji mkoani humo na Mamlaka zinazohusika kushirikiana na Maafisa afya kutibu maji katika bwawa la Songwa lililopo wilayani Kishapu,linalodaiwa kuwa ndiyo chanzo cha kueneza ugonjwa wa kipindupindu, wilayani Kishapu.

Hayo ameyasema leo kwenye kikao cha maandalizi ya kampeni ya chanjo ya surua na Rubella na tathimini ya pamoja,na kujadili mwenendo na udhibiti wa ugonjwa wa kipindu pindu.

Mndeme amesema kampeni hii ina lengo la kuongeza kinga kwa watoto wote wenye umri wa kuanzia miezi tisa hadi miezi 59 kwa kuwapatia chanjo hata kama wameshapata chanjo hizo, katika utaratibu wa kawaida wa kutoa huduma za chanjo.

“Mkoa unatarajia kuwachanja watoto 300,193 ambapo jumla ya vituo 236 vya kutolea huduma za afya na vituo 123 vya muda vimeandaliwa kwa ajili ya kutoa huduma za chanjo, na kwenye eneo la lishe, mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali unaendelea kupambana na tatizo la utapiamlo hasa udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano,”amesema Mndeme.

Pia Mndeme amesema mkoa umeweza kupunguza kiwango cha udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano kutoka asilimia 32:1, mwaka 2018 hadi kupungua asilimia 27:5, na katika mwaka 2022 uzito pungufu umepungua kutoka asilimia 13:3 na mwaka 2018 hadi asilimia 8:6, mwaka 2022 kiwango cha ukondefu kwa watoto chini ya miaka mitano kimepungua kutoka asilimia 4:3
mwaka 2018 hadi asilimia 1:3 mwaka 2022 .

“Pamoja na mafanikio hayo bado kiwango cha udumavu kiko juu ambapo kinatakiwa kushuka kufikia asilimia 20 , hivyo tuongeze nguvu tutokomeze udumavu ndani ya mkoa wetu sote tukatae ulemavu na udumavu, nawaomba wazazi wote kuwapeleka watoto wenye sifa zakupatiwa chanjo wawapeleke ili kujikinga na magonjwa hayo”amesema.

Mndeme akizungumzia ugonjwa wa kipindu pindu amesema katika Mkoa wa Shinyanga tangu Desemba 2023 hadi Februari 12 mwaka huu, wlipatikana wagonjwa 192, ambapo Kishapu walikuwa 109, Kahama 60, Manispaa ya Shinyanga 23 huku vifo vikiwa sita, na Februari 13 kumeibuka wagonjwa wapya 11 ambao wanatoka wilayani Kishapu kata ya Maganzo,Songwa na Mwigumbi ambapo chanzo cha ugonjwa huo ni maji ya bwawa la Songwa.

“Niwaombe sana wadau wa maji na mamlaka zinazohusika mshirikiane na maafisa afya kuyatibu hayo maji ya kwenye bwawa la Songwa muyawekee dawa za kuuwa wadudu wanaosababisha ugonjwa wa kipindupidu ili kuzuia usiendelee kuenea pia niwaombe wazazi muwasalimie watoto wenu wakiwa tumboni na kuwaambia maneno mazuri kwani wanasikia ,”amesema Mndeme.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Shinyanga Faustine Mlyutu, amesema Mkoa umejipanga kukabiliana na ugonjwa wa Kipindipindu, na umejipanga kutekeleza njia mbalimbali za kuweza kudhibiti ugonjwa huo ili usiweze kuenea, kwa kugawa dawa za kinga za kutibu Maji, ambazo ni (Aqua Tab)na kufanya ukaguzi wa kaya zisizo na vyoo kuziagiza zijenge vyoo bora.

Naye Dk. Magenda Kihulya kutoka TAMISEMI amesema ni vizuri wakazuie ugonjwa wa kipindupindu na wananchi wazingatia maelekezo ya wataalamu wa Afya pamoja na kuwa na vyoo bora, kwani sheria inaelekeza watu wasio na vyoo wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria, wanatakiwa kuwa na vyoo bora ili kuepuka magonjwa yamilipuko.

By Jamhuri