Serikali yaja na suluhisho la upatikanaji wa nishati ya umeme migodini

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Madini imeanza mazungumzo na Kampuni ya TAQWA-DALBIT kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa upatikanaji wa nishati ya umeme migodini na maeneo yenye wachimbaji wadogo ili kuchochea shughuli za uchimbaji madini nchini Tanzania.

Mazungumzo hayo yamefanyika jana Jijini Dodoma na kuongozwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde na Naibu Waziri Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa pamoja na Menejimenti ya Uongozi wa Kampuni ya TAQA-DALBIT ikiongozwa na Meneja Mkuu Ndugu Amr Aboushad na Mkurugenzi wa maendeleo ya Biashara Ndugu Raphael Banzi

Akiwasilisha maelezo ya awali, Ndugu Amr Aboushad amesema kwamba Kampuni yao ipo tayari kuja na mpango wa uzalishaji wa umeme kupitia gesi kwa kufunga mtambo katika migodi na maeneo ya wachimbaji ambayo itasaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa zaidi ya nusu ya gharama inayotumika hivi sasa kupitia matumizi ya mafuta ya dizeli na petroli na awamu ya pili itahusisha uzalishaji wa umeme kupitia mfumo wa umeme jua ambapo Kampuni itafunga mtambo mkubwa kwa gharama yao na kuwaunganisha wachimbaji wadogo kwa malipo ya mwezi ya matumizi ya nishati hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo,Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameishukuru Kampuni ya TAQA-DALBIT kwa utayari wa kutatua changamoto ya upatikanaji wa nishati ya umeme migodini na kuagiza uongozi wa Wizara kuitisha mkutano wa haraka na wadau wote wakiwemo wachimbaji wadogo na wakubwa ili kupata fursa ya kujadiliana namna bora ya utekelezaji wa mpango huu.

Utekelezaji wa mpango huu utasaidia sana kuchochea shughuli za uchimbaji nchini Tanzania na hivyo kuongeza uzalishaji wa madini.