Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu ameanza kuzifanyia tathimini taasisi na mashirika ya serikali, akisema kiu yake kubwa ni kuona taasisi na mashirika hayo yanafanya kazi kwa ufanisi kwa maslahi ya nchi.

Mchechu ameyasema hayo leo Julai 13, Dar es Salaam alipohudhuria mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ‘TADB’ na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere na kutoa wito kwa taasisi na mashirika yote kufanya kazi kwa ufanisi.

Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Nchechu akizungumza leo tarehe 13/7/2023 Jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Wahariri wa Vyombo vya habari uliofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere.

Mchechu amesema leo ameanza na TADB, lakini atakuwa na mikutano ya mara kwa mara, ili kuongeza ushirikiswaji wa taasisi hizo, lakini pia kufanya mabadiliko ya kiutendaji.

“Tunataka kuhakikisha kunakuwa na mawasiliano makubwa ya mashirika na wahariri wa vyombo vya habari, lengo kubwa hapa ni kuwafanya Watanzania ambao ndio wamiliki wa awali wa mashirika na taaisi hizo, ambapo Rais anamiliki kwa niaba yao basi wananchi hao waweze kujua yanafanya nini na waweze pia kuchangia mawazo yao,”amesema Mchechu.

Katika mkutano huo Mchechu ameitaka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kuwa na mikopo nafuu, ili kuwapata walengwa kwa urahisi, lakini pia kutoa elimu juu ya umuhimu wa mikopo hiyo.

“Kuna baadhi ya mazao yanachukua muda mrefu kuvuna unapomuambia mkulima atalipa mkopo baada ya muda fulani, anawaza bado nitakua sijavuna kwa hiyo wanaogopa ila wakipewa elimu na kuambiwa namna rahisi ya kulipa mikopo hiyo wengi watakuwa wanufaika,” amesema Mchechu.

Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Frank Nyabudenge akizungumza katika  kikao kazi kati na Wahariri wa Vyombo vya habari uliofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TADB, Frank Nyabudenge amesema benki hiyo ina malengo ya kufanya mapunduzi makubwa kwenye sekta ya kilimo ndio maana wanatoa mitaji kwa wakulima na kuongeza kwa sasa benki hiyo inazidi kupasua anga na kuna ongezeko kubwa la mikopo katika Serikali ya Awamu ya Sita.

” Idadi ya mikopo imekuwa ikipanda tulikuwa na mikopo Sh bilioni 110, ikipanda hadi Sh bilioni 152 ikafika Sh bilioni 262, na hadi kufikia Juni 30, 2023 tulikuwa na jumla ya mikopo Sh bilioni 317 na tunaamini hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu itaongezeka zaidi,” amesema Nyabudenge.

Mkurugenzi huyo amesema lengo lao ni kutanua wigo wa benki hiyo pamoja na kubadili mfumo wa kilimo Tanzania, lakini pia kuchagiza taasisi nyingine za kifedha kutoa mitaji kwa wakulima.

Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Nevelle Meena akizungumza jambo katika kikao kazi kati Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Wahariri wa Vyombo vya habari uliofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere.

By Jamhuri