Na Suzy Butondo,Jamhuri Media,Shinyanga

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro amewataka watumishi wote wa manispaa kuacha kufanya kazi kwa mazoe, badala yake watoke maofisini kwenda kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzitatua kwa wakati.

Agizo hilo amelitoa leo wakati akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Shinyanga, kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa halmashauri ya wilaya hiyo, ambapo amewataka watumishi wote kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake watoke ofisini waende wakawahudumie wananchi katika maeneo yao.

Mtatiro amesema Rais Samia Suluhu anataka wananchi wahudumiwe, wasikilizwe kero zao kwa kutendewa haki, kwani mtumishi ukimtendea haki mwananchi na wewe unapata haki kwa Mungu, hivyo ni vizuri wananchi wakasaidiwa kwa karibu mahitaji yao.

“Wananchi wetu wakitendewa haki inakuwa haki hadi kwa mungu na mimi kwenye suala la haki sina mswalia mtume , nimetumwa hapa kwa ajili ya kufanya kazi na kusimamia haki za wananchi, mimi sitaki kuona watumishi wakifanya kazi kwa mazoea, nahitaji nimsikilize mwananchi hatuwezi kumuacha akiendelea kupata matatizo kwa kusababishwa na watu wachache,”amesema Mtatiro.

“Kama upo kwenye utumishi unatakiwa uwe na roho ya kufanya kazi, nitafanya kila ninachoweza ili kuhakikisha kila mtumishi anakaa kwenye mstari, kazi hii niliyopewa ni zamana ya muda mfupi tu, ambayo ni ya kumsaidia Rais wetu mama Samia Suluhu, hivyo watumishi wa manispaa mjiandae kufanya kazi na kuwahudumia kwa wakati, mimi namchukia mtumishi ambaye hamsikilizi mwananchi ukiitwa kimbia na utumike “ameongeza .

Amesema kila mmoja atimize wajibu wake hataki kuona Mkuu wa mkoa au waziri anakuja kutatua matatizo ya Wilaya ya Shinyanga mjini, hao wakija ni kwa ajili ya kuzindua miradi mbalimbali na kutoa pongezi kwa kazi iliyofanyika.

“Baadhi ya wananchi waliokuwa wamehudhulia kikao hicho akiwemo Musa Maganga Mabula,Rose Makanyaga na Suzana Magoso wamemshukuru mkuu wa Wilaya huyo kwa kuwasikiliza kero zao, ambapo wamesema wanaamini atawasaidia katika kupata haki yao kwa wakati”amesema Charles Nkiliku.

“Tunakushukuru sana Mkuu wetu wa wilaya kwa hiki ulichokifanya katika siku ya leo Mungu akubariki sana, hivyo tunaamini tumepata jembe, hapa umesikiliza kero nyingi sana hasa za masuala ya ardhi na tayari zingine umezitatua leo leo na zingine ambazo bado tunaamini utazitatua tu, hatuna budi kumshukuru Rais na kumwambia asante kwa kutuletea mtu anayejali wananchi wake,” amesema Mwajuma Ally.

Katika kikao hicho wananchi wengi wamesema kero na changamoto zao mbalimbali wengine wagonjwa walikuwa wakihitaji msaada wa matibabu wengine mitaji, kila mmoja ametatuliwa hitaji lake na kuondoka kwenye kikao hicho akiwa na furaha na amani, ambapo ameahidi ataendelea kuzunguka kwenye maebeo husika, ili kuhakikisha kero zote zilizopo zinatatuliwa.

By Jamhuri