Na Suzy Butondo,JamhuriMedia,Shinyanga

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limekamata silaha tano pamoja na watuhumiwa wawili kwa kosa la kutengeneza na kumiliki silaha kinyume na sheria huku likikamata vitu mbalimbali ukiwemo mtambo wa kutengenezea siraha uitwao Vice,vikiwemo bhangi, vitanda, magodoro , yai la mbuni na mkia wa nyumbu.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Shinyanga leo Jumatano Machi 27,2024, amesema mnamo Machi 13,2024 katika maeneo ya Kitongoji cha Izagala, Kijiji cha Ntundu, Kata ya Busangi, Tarafa na Wilaya ya Kipolisi Msalala Mkoa wa Shinyanga, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limekamata mtuhumiwa mmoja akiwa na mtambo wa kutengenezea silaha uitwao Vice.

Magomi amesema kuwa mtuhumiwa huyo pia alikamatwa akiwa na Silaha tatu aina ya Gobole, maganda matano ya risasi ya kutengeneza kienyeji, maganda manne ya Shotgun, vipande saba vya chuma na mbao mbili za kutengeneza silaha aina ya gobole.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi akionyesha vifaa mbalimbali vilivyokamatwa.

“Lakini pia mnamo tarehe 17/03/2024 huko maeneo ya Kijiji cha Bugomba “A”, Kata ya Ulewe, Tarafa ya Mweli Wilaya ya Kipolisi Ushetu na Mkoa wa Shinyanga Jeshi la Polisi lilimkamata mtuhumiwa mmoja na baada ya kupekuliwa nyumbani kwake alikutwa akiwa na silaha mbili aina ya Gobole zisizo na namba ya usajili,”amesema Magomi

Amesema gobole hizo zilikuwa na Risasi 03 za Ganda 1 ya risasi ya gobole, mafuta ya kusafishia bunduki na unga udhaniwao kuwa ni baruti akiwa amevihifadhi chumbani kwake bila kibali, kitu ambacho ni kinyume na Sheria za nchi, ambapo watuhumiwa wote wawili mara baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Pia Jeshi hilo limekamata Bhangi miche 169 na Kete 17, Pikipiki 11, mirungi bunda 38, TV 6, Sigara pakiti 159, Magodoro 05, Pombe ya moshi lita 5, Redio 3, Vyuma 31 mali ya TANESCO, Mtungi 1 wa gas aina ya Taifa, Kompyuta mpakato 1, Kitanda 01, Solar panel 01, Genereta 01 aina ya Appolo, Antena 1 ya Tv, Mafuta ya kusafishia bunduki, yai 01 lidhaniwalo kuwa la Ndege aina ya Mbuni pamoja na mikia 04 idhaniwayo kuwa ya mnyama aina ya Nyumbu.

Kamanda Magomi amesema jumla ya kesi 13 zimepata mafanikio ambapo, kesi 2 za kubaka washtakiwa wawili walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, kesi 2 za wizi washtakiwa wawili walihukumiwa kifungo kati ya miezi 6 mpaka miaka 7 jela.

Kesi moja ya kupatikana na bhangi mshtakiwa alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela, kesi moja kuvunja nyumba usiku na kuiba washtakiwa mbili walihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, kesi sita kuingia kwa jinai washtakiwa sita walihukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela na kesi moja kutishia kuua kwa maneno mshtakiwa mmoja alihukumiwa kwenda jela miezi mitatu.

Pia katika kitengo cha usalama barabarani limefanikiwa kukamata jumla ya makosa 3,315 huku makosa ya magari yakiwa ni 2,615 na makosa ya bajaji na pikipiki ni 700 wahusika waliwajibishwa kwa kulipa faini za papo kwa hapo.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linatoa wito kwa wananchi kuacha mara moja vitendo vya kihalifu na vilivyo kinyume na Sheria na halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya kihalifu

By Jamhuri