na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Pwani

Rufiji Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff ameagiza timu ya wataalamu wa TARURA Makao Makuu na ya Mkoa wa Pwani kufanya mapitio ya usanifu wa daraja la Bibi Titi Mohammed-Mohoro linalotarajiwa kujengwa wilayani hapa.

Mhandisi Seff ameyasema hayo mara baada ya kufanya ukaguzi wa mradi huo na kuona jinsi maji yalivyojaa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Mhandisi Seff amesema lengo la mapitio hayo ni kuhakikisha kuwa uwezo wa daraja litakalojengwa litamudu kupitisha maji ya mvua na kutoka bwawa la Nyerere endapo yatafunguliwa bila kuleta madhara yoyote kwa wananchi.

Aidha,Mhandisi Seff alifanya kikao na viongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Rufiji upande wa pili wa daraja hilo ambao pia walionesha wasiwasi wao kutokana na historia ya eneo hilo na maji kutoka bwawa la Nyerere endapo yatafunguliwa wakati mvua zinaendelea kunyesha.

Hata hivyo Mhandisi Seff aliwahakikishia viongozi hao kwamba mapitio hayo ni kujiridhisha kuwa usanifu uliofanyika unakidhi na kupitisha maji yatakayoongezeka bila kuleta madhara yoyote.

Daraja la Bibi Titi Mohammed-Mohoro linatarajiwa kuwa la zege na kukamilika kwake itaenda kuondoa kilio cha muda mrefu cha wakazi wa vijiji vya Mohoro na Chumbi pamoja na kuimarisha uchumi.

By Jamhuri