Wizara ya Afya imepiga marufuku matangazo ya waganga wa kienyeji na wale walioboresha neno hilo na kujiita ‘tiba mbadala’.

Uamuzi wa Serikali umekuwa kama mtego wa panya – unawakamata waliomo na wasiokuwamo. Si wote wenye kutoa aina hiyo ya tiba hawafai, ila ni ukweli kwamba kuna maelfu ya matapeli walionufaishwa na umbumbumbu wetu.

Miaka minne iliyopita, katika ukurasa huu huu, nilihoji ukimya wa Serikali katika kuwashughulikia matapeli wanaojitangaza bila woga kwamba wana uwezo wa ‘kusafisha nyota’, ‘kumvuta mpenzi aliye mbali’, ‘kumjaza mtu fedha za majini’, ‘kupanda cheo’; na kibaya zaidi kuwahadaa wazazi na wanafunzi kuwa wana uwezo wa kumfanya mwanafunzi afaulu mitihani kwa dawa watakazompa!

Matangazo haya ya kipuuzi yameenea kwenye nguzo za umeme na simu; kwenye kuta na kila mahali ambako wenye nayo wanaamini ‘wateja’ wao wanaweza kuyasoma. 

Vipo vyombo vya habari, hasa magazeti na redio; vimekubali kusambaza hatari hii kwa wananchi. Wakati nikifanya kazi katika kampuni ya Habari Corporation, moja ya sera zake kuu ilikuwa ya kuyakataa matangazo hayo ya kipuuzi hata kama mtangazaji angekuwa radhi kulipa kiasi kinono cha fedha. Huo ulikuwa na unaendelea kuwa uamuzi wa busara.

Kuzagaa kwa matangazo haya kulikuwa ni matokeo ya Serikali yetu dhaifu. Serikali Kuu ilifumba macho, hata ikashindwa kuzibana Serikali za Mitaa kukomesha utapeli huo. Matokeo yake Tanzania ikawa kwenye nafasi za juu za mataifa yanayoamini na kushiriki vitendo vya ushirikina. 

Siyo siri kuwa miongoni mwa sifa zetu Watanzania mbele za majirani zetu ni ushirikina! Hatuwezi kujinasua kwenye sifa hii mbaya kwa sababu ushahidi wa haya yanayosemwa upo. 

Mgeni anapoingia katika miji yetu akakuta nguzo za umeme na kuta zimepambwa kwa matangazo ya ‘Mganga kutoka Sumbawanga’, ‘Mganga kutoka Ufipa’, ‘Mganga kutoka Nigeria’ n.k picha anayoipata ni ya ushirikina na ujinga wetu.

Kuwapo kwa matangazo hayo kumechangia kwa kiwango kikubwa mauaji ya albino, vikongwe na ajuza wengi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa. Yamewafanya wengi wetu wasibangue bongo katika kujiletea maendeleo, badala yake wabaki wakiamini ndumba na upuuzi mwingine wa aina hiyo.

Januari mwaka huu, Shirika la HelpAge International lilisema kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2014 wazee waliouawa ni 4,612. Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ya mwaka 2009 inasema ajuza 2,583 waliuawa katika mikoa minane ikiwa ni wastani wa mauaji 517 kila mwaka. Mwanza pekee waliuawa ajuza 689 kati ya mwaka 2002 na 2007 ikiwa ni wastani wa mauaji 140 kila mwaka.

Mkoani Shinyanga, ajuza 242 waliuawa kati ya Januari 2010 na Juni 2011. Miongoni mwa sababu kuu za mauaji haya ni ramli zilizohamasishwa na matangazo haya ya kipuuzi.

Ndugu zangu, Taifa lolote lenye watu makini haliwezi kunyamazia hali hii, au kuwaunga mkono wapiga ramli na matapeli walioamua kuusaka utajiri kwa ghiliba.

Mwanzoni nimesema mtego wa panya huwanasa waliomo na wasiokuwamo. Matapeli waliojiingiza kwenye masuala ya tiba wameharibu kabisa maudhui na faida njema zinazotokana na tiba za asili ambazo Waafrika tulizitumia kabla, wakati na baada ya ujio wa wakoloni. 

Tiba za asili zipo nzuri na zinafanya kazi nzuri kabisa. Kuna ushuhuda mwingi tu wa watu waliopona kwa kutumia tiba mbadala. Mwanya huo umetumiwa na matapeli kubadili maudhui ya tiba hizo kutoka kwenye huduma na kuwa biashara.

Serikali ina wajibu wa kuwalinda watu wake kwa kila namna ikiwa ni pamoja na kuwaepusha dhidi ya matapeli hawa. Njia nzuri ambayo imetumiwa na Serikali kwa miaka yote ni kuwapo kitengo maalumu katika Wizara ya Afya kinachoshughulikia masuala ya tiba mbadala. 

Mara zote tiba zilipothibitishwa katika maabara kwamba zinafaa kwa matumizi ya binadamu, mgunduzi alipewa kibali ili awahudumie wenye kuzihitaji. Vitendo vya rushwa na uzembe wa wahusika katika kufuatilia sheria na kanuni zake kumesababisha wananchi wengi, si tu wapoteze fedha, bali pia wafariki dunia kwa kunywa dawa zisizo sahihi.

Kuna mengine yanasemwa ya kwamba wingi wa ‘madaktari wa tiba mbadala’ ni matokeo ya kufeli kwa Serikali kuwapatia wananchi huduma afya za kisasa.

Wapo wanaoamini kuwa ughali wa matibabu, ukosefu wa vifaa tiba, huduma mbaya za madaktari na wauguzi kadhaa ni miongoni kwa sababu zinazoliimarisha soko la ‘dawa mbadala’.

Sina hakika na madai hayo, lakini lililo wazi ni kwamba hata zama zile za huduma za afya zilipotolewa bure nchini kote, bado wapo waliochepuka na kwenda kwa waganga wa kienyeji wakiamini dawa za hospitali hazina msaada wa uponyaji. 

Vyovyote iwavyo, bado kuna ukweli kwamba zipo dawa za asili zenye uwezo mkubwa wa kutibu maradhi mengi.

Lakini Serikali haiwezi kusukumiwa lawama zote. Udhaifu wa wananchi wenyewe ni sehemu ya tatizo hili. Kwa watu wanaowaza barabara, ni jambo la ajabu mno kushawishiwa na hata kuweza kuamini kuwa mtoto anaweza kukaa nyumbani akichanjwa chale na kupewa dawa, halafu aingie kwenye chumba cha mtihani ashinde mitihani! 

Kama wapo waliothubutu nadharia hii na kufanikiwa, basi wajitokeze watoe ushuhuda. Naamini hawapo. Kuendelea kuamini ujinga wa aina hii ni hatari kwa mustakabali wa Taifa letu.

Jambo ambalo si rahisi kuthibitishwa kisayansi, Serikali makini haipaswi kulifumbia macho. Ni wajibu wake kupita huku na kule kwa lengo la kuwashughulikia wote wanaoeneza imani hiyo.

Ukiacha waganga wa kienyeji, kuna kundi jingine ambalo watu wengi wanakosa ujasiri wa kulisema hadharani. Kundi hili ni hatari kama lilivyo kundi la matapeli watoa tiba mbadala ambazo haziponyi.

Kundi hili ni la wajenga makanisa na waanzisha madhehebu.

Serikali yetu imetoa uhuru wa kuabudu kwa wananchi wake. Kama wasemavyo viongozi wetu wakuu mara kwa mara, Serikali ya Tanzania haina dini, lakini watu wake wana dini. Kwa kuzingatia kigezo hicho, Serikali imekuwa na idara maalumu chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inayosajili taasisi za kidini.

Kwa maudhui ya makala hii, napenda kuzungumzia usajili wa makanisa.

Ingawa Serikali imetoa uhuru wa kuabudu, bado sheria zipo za kuhakikisha uhuru huo hauathiri uhuru wa wengine, na pia aina hiyo ya imani haikinzani na haki za msingi za kibinadamu, mila, desturi na hata sheria za nchi.

Kinachoendelea sasa kwa baadhi ya makanisa mengi ni utapeli na wala si kumtumikia Mungu au kuwasaidia wanadamu kujengeka kiroho. Kuna makanisa mengi yaliyoanzishwa kwa misingi ya kibiashara zaidi, na walengwa wakuu ni watu wenye matatizo ya kimaisha wanaopumbazwa na kuaminishwa mambo ambayo kamwe hawawezi kuyapata.

Mungu anayepewa sadaka kupitia M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money sidhani kama ni Mungu yule ambaye wengi wetu tunamwabudu. Mungu ambaye hawezi kumponya mgonjwa bila mgonjwa huyo kuweka fedha kwenye bahasha na kumkabidhi ‘mchungaji’ au ‘mtumishi’; huyo si Mungu, bali mungu.

Katika hilo la fedha, siku hizi ‘Mungu’ ameweka viwango vya sadaka! Tunaambiwa na ‘watumishi’ kuwa ukitoa chini ya kiwango ‘anachotaka Mungu’, basi maombi yako hayatapokewa! Huhitaji akili nyingi kutambua kuwa hii ni sanaa ya wachache kujipatia fedha.

Yapo makanisa yanayotenga viti kulingana na hadhi ya mtoa sadaka. Kabwela anayetoa sadaka ya Sh 1,000 hawezi kuketi mbele! Viti vya mbele ni kwa wale wanaotoa Sh 50,000 au Sh 100,000 au Sh 500,000 na kuendelea. Kiti kizuri kinapatikana kadri fungu la mtoa sadaka linavyokuwa nono! Kiti cha mtoa sadaka iliyonona kinawekewa sponji! Huyu Mungu wa matabaka, ni Mungu gani?

Wenye makanisa wengi wanacheza na saikolojia ya watu wenye matatizo. Wanajua mwanamke anayetamani kuwa na mtoto yuko radhi kutumia kiasi chochote cha sadaka na maombi ili apate mtoto.

Wanajua kijana mtihitimu wa chuo anayehangaika kupata kazi, ni rahisi kumnasa kwa kumshawishi afanye maombi mengi na marefu yanayoambatana na kumtolea sadaka Mungu.

Wanatambua kiu ya Watanzania wengi ni kupata maisha mazuri – kupata utajiri. Wanatamani wamiliki magari mazuri, nyumba nzuri, wale na walale vizuri nk. Kiu yao ili iweze kutimilizwa na Mungu, wanapaswa waombe na waombewe. Kuombewa sharti kuendane na sadaka! Tumeaminishwa sasa kwamba kama hutoi sadaka, Mungu hawezi kusikiliza maombi yake!

Wapo wenye kazi zinazowapa kipato cha wastani ambao wakishapata fedha, sehemu ya fedha hizo, au zote; hupelekwa kwa mitume na manabii! Wakishapeleka, nao huanza kuombaomba fedha kwa ajili ya nauli au kugharimia mahitaji mengine. Kwao kunayumba kwa nabii au mtume kunanawiri.

Wapo waliofiwa na wapendwa wao, lakini wakaaminishwa na baadhi ya matapeli kuwa hao wanaodaiwa kufariki dunia, hawakufariki ila wamechukuliwa ‘misukule’. Wakawaaminisha kuwa wanao uwezo wa kuwasiliana na Mungu kwa njia ya maombi na kuirejesha hiyo misukule. 

Wapo waliotumia mamilioni ya shilingi kama sadaka kwa matarajio ya ‘kumridhisha Mungu’ ili aridhie kufufuka kwa ndugu au wapendwa wao! Siku zinakwenda hakuna aliyefufuka, lakini wanatulizwa kwa kuambiwa ‘kwa Mungu miaka 1,000 ni sawa na siku moja” kwa hiyo wawe na subira tu! Wapo waliosubiri sana, na hadi leo hakuna aliyefufuka kutoka katika wafu (misukule).

Ukichunguza maisha ya ‘wachungaji’, ‘watumishi’, ‘maaskofu’ na ‘manabii’ wengi ni mazuri kweli kweli. Wanakula vizuri; na kwa sababu hiyo wana siha njema kabisa. Wamejenga nyumba za kifahari. Wanaendesha magari ya bei ghali. Wanasomesha watoto katika shule zenye kutoza ada kubwa sana. Wanapochoka kuishi Tanzania kwa sababu ya joto au mbu, wanakwenda mapumzikoni Ulaya na Marekani! Matibabu yao ni India, Afrika Kusini, London na mara chache wanakwenda Nairobi.

Makabwela wanaotoa sadaka wamebaki wakiwa na maisha duni. Kadiri maisha yanavyowaendea kombo, ndivyo wanavyosisitizwa na viongozi wao wa kiroho wasikate tamaa. Waendelee kuomba kwa sababu kuna siku Mungu atasikia maombi yao!

Haya ni mambo ya kiimani ambayo Serikali inaweza isiwe na namna ya kuyadhibiti moja kwa moja, lakini bado inaweza kuwa makini kwenye usajili wa haya makanisa ya kiroho!

Kusema hivyo si kwamba simwamini Mungu, la hasha! Namwamini Mungu, lakini tofauti na hawa wenzangu, mimi namwamini Mungu wa kweli! Mungu wa M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money, huyo sijashawishika kumwabudu.

Marko 12:38 tunasoma haya: Katika mafundisho yake, Yesu alisema: “Jihadharini na walimu wa sheria. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi yao rasmi na kusalimiwa kwa heshima masokoni. 39 Pia wao hupenda kukaa viti vya mbele katika masinagogi na kupewa nafasi za heshima katika sherehe. 40 Hao hao ndio huwadhulumu wajane nyumba zao na ili waonekane kuwa wema wanasali sala ndefu. Mungu atawaadhibu vikali zaidi.”

Simwabudu Mungu anayeweka viwango vya sadaka na kumfanya aliyetoa kikubwa aketi mbele, aliyetoa kidogo aketishwe nyuma-mwisho kabisa!

Marko 12:41 ananijengea uhalali wa haya niyasemayo.

Neno la Mungu linasema: Kisha Yesu akaketi karibu na sehemu ya kutolea sadaka Hekaluni akawaangalia watu walivyokuwa wakiweka sadaka zao kwenye chombo cha sadaka. Matajiri wengi waliweka humo kiasi kikubwa cha fedha. 42 Lakini mjane mmoja fukara, alikuja akaweka sarafu mbili zenye thamani ya senti kumi.

43 Yesu akawaita wanafunzi wake akawaambia,“Ninawaambia hakika, huyu mjane ametoa zaidi kuliko wote! 44 Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali zao; lakini huyu mama ingawa ni fukara, ameweka kila kitu alichokuwa nacho, hata na kile alichohitaji kwa ajili ya riziki yake.”

Ukiacha matapeli kwenye tiba mbadala (nasisitiza kuwa si wote), eneo jingine hatari kabisa linalotumiwa kuwapumbaza na kuwaumiza wananchi wengi bila kujali kiwango chao cha elimu na ukwasi; ni hili la mlipuko wa manabii, mitume, wachungaji na watumishi! Turejee kwenye makanisa ya kweli yanayomhubiri Mungu wa kweli.

By Jamhuri