Tatizo la Tanzania si Katiba mpya

Mwaka 2012 niliandika makala katika safu hii iliyosema: “Nitakuwa wa Mwisho Kuishabikia Katiba Mpya”.

Nilisema nimejitahidi kutafakari ni kwa namna gani Katiba mpya itatuletea mabadiliko ya kweli tunayoyataka, nimekosa majibu – na sidhani kama nitayapata.

Fikra zangu zikanirejesha enzi za kudai Uhuru. Wapo walioamini kuwa kwa kupata Uhuru, taifa letu lingepiga hatua kubwa kimaendeleo. Wapo waliojiaminisha kuwa kwa kupata Uhuru, maana yake umasikini ungetoweka. Wengine wakauona Uhuru kama kitu pekee cha kutufikisha kwenye nchi ya kimaendeleo.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitambua athari za dhana hiyo. Akaja na Uhuru na Kazi, akiamini kuwa Uhuru pekee haukuwa suluhu ya matatizo yetu, isipokuwa kwa kufabya kazi kwa juhudi na maarifa.

Hizo zilikuwa njozi. Miaka 54 baada ya Uhuru, tuna makabwela wengi. Idadi yao inaongezeka.

Ugumu huu wa maisha umewafanya wengi waamini kuwa kwa kupata Katiba mpya, basi kila kitu kitakuwa kwenye mstari. Tunarejea tena kwenye njozi zile za zama za Uhuru. Wanaamini kwa kupata Katiba mpya, watapata milo mitatu kwa siku, watasomesha watoto, watajenga nyumba, watanunua magari, watafanya kila linalomfaa mwanadamu ili aweze kuishi kwa sifa zitakazomtofautisha na wanyama wengine. Wapo walioamini kuwa kwa Katiba mpya, basi mafisadi, wezi, wahujumu uchumi na wahalifu wengine, watakoma.

Nikasema mwaka huo wa 2012 kwamba wakati fulani aliyekuwa Rais wa Ghana, Jerry Rawlings, alipata kuuliuzwa ni kwa namna gani ameweza kuifikisha nchi yake kwenye maendeleo ya kupigiwa mfano.

Rais Rawlings, akajibu kwa kujiamini kabisa kwamba ametumia sera za Tanzania na maandiko ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Julius Nyerere, kuifikisha Ghana hapo ilipofika. Akasifu maandiko na sera za Tanzania akisema vilikuwa vimebeba mafunzo maridhawa kwa taifa lolote la Afrika kuweza kuvitumia kwa mazingira yake na kujipatia maendeleo.

Huyo alikuwa Rawlings. Yupo mwingine. Huyu ni Rais Paul Kagame wa Rwanda. Kwa Kagame, Tanzania ni darasa tosha. Amekuwa muwazi kueleza mbinu alizozitumia kuifikisha Rwanda hapo ilipo; nyingi akiwa amezinakili kutoka kwetu. Nidhamu, utendaji kazi na kuyashusha maendeleo kwa wananchi. Haishangazi kuiona Rwanda ikiitumia Oktoba 14 kama siku rasmi ya kumkumbuka Mwalimu Nyerere, kwa sababu kwa maandiko yake, wamefanikiwa.

Waliofaidika kwa sera za Tanzania ni wengi mno. Siwezi kuwataja wote. Ninachojaribu kukisema hapa ni kwamba hata kabla ya Katiba mpya, Tanzania tumekuwa na sheria na sera nzuri sana. Tumepata bahati ya kuwa na maandiko mazuri na viongozi walioona mbali, lakini vyote tumevipuuza. Tumeviweka kando. Sasa tunalilia Katiba mpya kana kwamba itakuja na kitu cha ajabu sana.

Kama hatutabadilika na kuwa watu wa vitendo, hiyo Katiba mpya hata ikipambwa kwa maandishi ya dhahabu na almasi, na ikafukizwa maradhi ya karafuu; itakuwa kazi bure.

Rais John Magufuli, amethibitisha kwa vitendo kuwa tatizo la Tanzania, hasa kwa miaka 10 iliyopita si Katiba, bali ni uongozi mbovu wa nchi uliozaa mafisadi, wakwepa kodi, wauaji, watumbua maisha, walafi wa fedha na mali za umma, wazembe na matapeli wa kila aina.

Magufuli, kwa mwezi mmoja amepandisha makusanyo ya kodi kwa Sh bilioni 500 zaidi, si kwa Katiba mpya, bali ile ile ya mwaka 1977.

Katiba ya sasa ukiisoma hutaona kama ina dosari nyingi za kuwafanya wengine waisigine au waiponde. Haina udhaifu huo. Katiba yetu imeeleza vema kabisa namna ya kulinda rasilimali za nchi yetu. Imeeleza dhima ya kila Mtanzania katika kulinda na kuhifadhi rasilimali asilia. Imeainisha haki ya kila Mtanzania kutendewa haki mbele ya vyombo vya utoaji haki. Imesema wananchi wote wako sawa mbele ya sheria.

Kutoka na Katiba, tuna sheria nyingi. Tuna sheria hadi za kuzuia uvutaji sigara katika hadhira-sheria ambayo haipo katika mataifa mengi duniani. Tuna sheria za kulinda na kuhifadhi mazingira. Sheria hizo zikatungiwa sheria ndogo ndogo zinazozuia kukata miti hovyo, kujisaidia maeneo yasiyoruhusiwa, kutotupa taka ovyo, na kadhalika.

Pamoja na utitiri wa sheria zote hizo, tujiulize, kitu gani kimetukwamisha hata tusiweze kusitekeleza? Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliwahi kutoa ripoti inayoonyesha namna Tanzania inavyotafunwa. Sheria za kuwabana wezi zipo, tena zipo sheria kali kama ile ya Uhujumu Uchumi. Kila mwaka CAG anatoa ripoti akiainisha majizi wanaolimaliza taifa. Anafichua njama zinazofanywa na viongozi na wafanyabiashara kuhakikisha Tanzania inasalia mifupa. Hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika. Hawachukuliwi hatua si kwa sababu Katiba ni mbaya, au sheria hazipo, bali kwa sababu ya wanaopaswa kuifanya kazi hiyo nao kuwa ni sehemu ya tatizo. Hatua hazikuchukuliwa kwa sababu Rais tuliyekuwa naye ameshiriki kuimiza nchi. Familia yake imeshiriki uhalifu mwingi wa kiuchumi. Amewatumia ndugu na marafiki zake kuiongoza nchi.

Wafanyabiashara wamekwepa kodi kwa Katiba hii hii, na wamenaswa kwa Katiba hii hii. Tatizo si Katiba, isipikuwa aliyekuwa ameapa kuilinda.

Sherehe za Uhuru hazikubadilishwa staili ya kuadhimishwa kwa kutumia Katiba mpya. Usafiri haukufanywa kwa Katiba mpya. Safari za viongozi na watumishi wa umma hazikuzimwa kwa Katiba mpya. Watoto wetu watasoma bure, si kwa Katiba mpya. Watendaji wazembe wanafukuzwa si kwa Katiba mpya. Upuuzi sasa unafutwa nchini si kwa Katiba mpya.

Muhimbili wanapata dawa na malazi kwa Katiba ile ile. Wakulima watalipwa kwa Katiba ile ile. Fedha za umma zinaokolewa kwa Katiba ile ile. Watumishi wa umma wanawahi kazini kwa Katiba ile ile. Kumbe basi, tatizo la Tanzania si Katiba, isipokuwa tulikuwa hatuna uongozi kwa miaka 10. Mungu ni mwema, hadi leo tuko salama. Mungu anatupenda sana Watanzania.

Katiba yetu hakuna mahali inasema wageni ndiyo wawe wa kwanza kufaidi rasilimali za nchi. Haisemi wao ndiyo wafaidi samaki wetu maziwani na baharini, lakini yote haya yamefanyika huku umasikini ukiongezeka kwa wananchi. Kwenye sheria za nchi yetu ipo inayompa mamlaka Rais kuidhinisha mtu anyongwe. Hii ndiyo adhabu kali kabisa katika nchi yetu. Tumeshindwa kuitumia. Je, Katiba mpya italeta sheria gani kali kuliko hiyo? Sheria ya kunyonga ukoo wote wa mhalifu?

 Sheria dhidi ya wahujumu uchumi ipo, sheria ya kufilisi mali za mafisadi zipo, hiyo Katiba itakuja na jipya gani?

Ndiyo maana nasema Katiba ya kweli ya Watanzania inapaswa kuandikwa katika mioyo na utashi wao, na wala si ya kuandikwa kama hii tunayoililia sasa. Katiba iwe katika mioyo ya Watanzania.

Tunapaswa kubadilika kifikra. Tunapaswa kuwajibika-kila mmoja kwa nafasi yake-tunapaswa kuwa watu wa vitendo zaidi badala ya blabla na porojo zisizokoma, tunapaswa kusimamia sheria na kanuni tunazojiwekea.

Tunaweza kuwa na Katiba nzuri sana, lakini bila kuwa na wasimamizi wa kweli wa Katiba hiyo, tutabaki kulialia na hata Rais wetu akiulizwa kwanini Watanzania mu maskini, atajibu kwamba hata yeye hajui.

Rais Magufuli amethibitisha pasi na shaka kuwa Katiba mpya na nzuri haitoshi kutufanya tushibe, haiwezi kuwasomesha bure watoto wetu, haiwezi kupunguza ajali za barabarani kama madereva wataendelea kubebwa, haiwezi kumaliza umasikini kama kila siku kazi yetu ni kuamkia vilabuni na kushinda kwenye michezo ya ‘pool’. Katiba mpya haiwezi kutufaa jambo kama wengi wetu tutakuwa tukisubiri kulishwa chakula na mtu mmoja katika familia ya watu 15.

Wala Katiba mpya haiwezi kutufaa lolote kama maono ya viongozi wetu ni kuwahamasisha vijana kukopeshwa bodaboda badala ya kuwapa matrekta na zana nyingine za kuwawezesha kuzalisha mali kwa njia za kisasa.

Katiba mpya haiwezi kutufaa kitu kama tutaendelea kuabudu ushirikiana na kuamini kuwa maendeleo ya mtu yanaletwa kwa imani za kijinga za kuwaua ndugu zetu albino na kuchukua viungo vyao.

Hatuwezi kubadilika kimaendeleo kama tutabaki kuwa taifa la watu wanaoamini tunguli na matangazo ya waganga matapeli eti wanaosafisha nyota na kutufanya tupande vyeo kazini. Kama ingelikuwa kweli mtu akipata dawa hizo anapanda cheo, basi kampuni ingekuwa na mameneja 50 au 100 kwa wakati mmoja!

Tuna rasilimali ya mabonde, wanyamapori, madini, maziwa, bahari, mito, ardhi isiyo na mfano; na ukwasi wa kila aina. Tunachohitaji si Katiba pekee, bali viongozi makini wa kuwafanya wananchi wafaidike na ukwasi huu. Kwangu mimi, suala la kuwabadili kwanza Watanzania kifikra ili waipende nchi yao, wapende kuwajibika ndiyo yangekuwa mambo ya maana zaidi.

Kwangu mimi, kiongozi mkuu wa nchi na wasaidizi wake ndiyo wanaoweza kuleta mabadiliko ya kweli kwa kuwaongoza wananchi na kusimamia rasilimali za nchi. Maandishi tu kwenye Katiba bila utashi wa viongozi yamethibitika kuwa si lolote wala chochote.

Tukiwa na Katiba mpya, lakini tukawa na kiongozi anayemzuia Waziri kupanua barabara eti kwa sababu kwa kufanya hivyo anawaudhi wapigakura, haki ya Mungu tutaendelea kuonekana kama taifa ya washirikina tu.

Mwisho, niseme kwamba Katiba nzuri haina maana kama uwajibikaji wa viongozi wetu na wananchi vitakosekana. Je, uwajibikaji utaletwa na maandiko tu; au kwa dhamira na utashi wa wenye nchi? Je, utaondoa dhambi katika jamii kwa kujenga makanisa au misikiti mingi?

Unaweza kuwa na makanisa na misikiti mizuri sana, lakini bila kuwa na mapadre na masheikh wenye weledi itakuwa kazi bure. Hili limethibitishwa na Kikwete na limerekebishwa na Rais Magufuli. Yapo mataifa yasiyokuwa na Katiba iliyoandikwa, lakini yapo mbele kimaendeleo. Nitakuwa wa mwisho kuamini kuwa Katiba mpya ndiyo suluhu ya madhila yote yanayotufika sasa.

Rais Magufuli amethibitisha kuwa upya wa gari si hoja! Hoja ni aina ya dereva. Dereva tuliyempata ni Rais Magufuli.