Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, amelaani kile alichokiita “uzalendo wa uadui” na ametaka Ulaya iungane kushughulikia uhamiaji ni kuzuia kuigeuza Bahari ya Mediterenia kuwa “kaburi la heshima”.

Mkuu huyo wa Kanisa Katoliki ameyazungumza kwenye hotuba yake refu ya kuunga mkono kuwakaribisha wahamiaji barani Ulaya iliyohitimisha kongamano la Kanisa lake juu ya masuala ya Bahari ya Mediterenia mjini Marseille, mji wa bandari wa Ufaransa ambao kwa karne kadhaa umekuwa makutano ya tamaduni na dini mbalimbali.

“Kuna kilio cha maumivu kinachotugusa sote, na kinaibadilisha Mediterenia, bahari yetu, kutoka kuwa chanzo cha ustaarabu na kuwa, bahari ya mauti, kaburi la heshima: ni kilio cha masikitiko cha kaka na dada zetu wahamiaji”, amesema.

Papa Francis amepokelewa kwenye mji huo na Rais Emmanuel Macron ambaye baadaye walipangiwa kuwa na mkutano wa faragha siku ya Jumamosi (Septemba 23) kabla ya kurejea mjini Roma.

Papa ameianza siku hiyo kwa kukitembelea kituo kinachowahudumia wenye mahitaji katika wilaya ya Mtakatifu Mauront, mojawapo ya maeneo masikini kabisa nchini Ufaransa, kinachosimamiwa na watawa na kilichoanzishwa na Mtakatifu Mama Teresa.