MUSOMA

NA JOVINA MASSANO
 

Maji ni uhai kwa kila kiumbe kilichopo katika dunia. Kama msemo huo una ukweli ndani yake, basi wakazi katika vijiji kadhaa katika wilaya za Musoma Vijijini na Butiama wanatarajia kuanza kupata uhai huo, kwani wataanza kupata huduma ya maji safi na salama hivi karibuni.
Hilo linafuatia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji kati ya Tanzania na Kampuni ya Metito Overseas Limited ya Misri inayoshirikiana na Kampuni ya Jandu Plumbers Limited ya jijini Arusha.
Mradi huo mkubwa wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 61, ambao umesainiwa katika Kijiji cha Nyamisisi mbele ya wananchi wa wilaya hizo mbili, unatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi hasa kina mama kwa kuwaondolea adha ya kufuata maji umbali mrefu.
Mradi huo unaogharamiwa na Serikali ya Tanzania, Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA) na Mfuko wa Maendeleo wa Saudi Arabia (SFD), unatarajiwa kutoa maji kwa ajili ya zaidi ya wakazi 30,000 wa wilaya hizo mbili katika vijiji 20. Kwa muda mrefu wakazi hao wametegemea visima vifupi na vyanzo vingine vya maji visivyo vya uhakika.
Uamuzi wa serikali kugharamia mradi huo ni kielelezo cha azima yake ya kutoa huduma endelevu ya maji safi  na salama pamoja na elimu ya usafi wa mazingira kwa wananchi wake. Hii ni njia mojawapo ya kutekeleza Sera ya Maji ya Taifa ya Mwaka 2002 inayolenga kuhakikisha wananchi vijijini wanapata maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Katika bajeti yake ya mwaka 2019/20, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwakwamua wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria  na kuweza kuwatengea bajeti ya Sh trilioni 1.3 za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji ili kuwaepusha na magonjwa mbalimbali ya kipindupindu, kuhara, minyoo na magonjwa mengine yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.
Katika hotuba yake wakati wa utilianaji saini wa mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo, alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, inataka kila mwananchi apate huduma ya maji safi na salama ya kutosha kwa gharama ambayo anaweza kuimudu.
“Sekta ya maji ni miongoni mwa sekta za kupewa kipaumbele katika mkakati wa kutoa huduma bora ya maji na kukuza uchumi na kupambana na umaskini kutokana na umuhimu wake mkubwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda nchini,” anasema Prof. Mkumbo.
Pia anasema ili mradi huo uwe endelevu ni jukumu la Mamlaka ya Maji, serikali na wadau wote kwa pamoja kushirikiana kulinda na kutunza miundombinu ya maji, kwani serikali imetumia gharama kubwa kuijenga. Hilo litakwamisha utekelezaji wa azima ya kuhakikisha watu wengi wanapata huduma bora ya maji safi na salama.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, aliipongeza serikali kupitia wizara hiyo kwa jinsi ambavyo imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya maji katika Mkoa wa Mara, huku akisifia utekelezaji wa ahadi ya Rais Dk. John Magufuli katika kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015.
Malima aliwaonya baadhi ya wananchi na watendaji wa Mamlaka ya Maji ambao watabainika kuhujumu mradi huo. Anasema kuhujumu mradi huo ni sawa na kuihujumu serikali na rasilimali zake.
“Serikali imetumia fedha nyingi sana na ni jukumu lenu wananchi wote kuulinda mradi huu ili uweze kuwa endelevu na kuweza kuwanufaisha hata wajukuu wetu na kufurahia matunda mema ya serikali ambayo kwa wakati huo sisi sote huenda tusiwepo duniani,” anasema.
Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, pamoja na kupongeza juhudi hizo kubwa zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, anaomba vijiji vitano ambavyo ni Tegeruka, Mayani, Katariyo, Nyangoma na Kurwaki ambavyo vinapitiwa na mradi navyo viweze kuingizwa kwenye orodha ya kunufaika na mradi huo.
“Nina uhakika kuwa vijiji hivyo vikipata huduma ya maji safi na salama vitaondokana na adha nyingi ambazo zimekuwa ni changamoto kwa muda mrefu kwa wananchi hao,” anasema.
Ahmed Farouk pamoja na Harbinder Jandu, ambao ni wakurugenzi wa Kampuni ya Metito Overseas Ltd na Jandu Plumbers Ltd wanaohusika na ujenzi wa mradi huo mkubwa wa maji, wameahidi kukamilisha ujenzi wa mradi huo kwa muda wa miezi 24 uliopangwa na serikali ili waukabidhi kwa wananchi waendelee na kunufaika na huduma ya maji.
Katika ujenzi wa mradi huo, wakurugenzi hao waliainisha kazi zitakazofanyika kuwa ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji katika eneo la Mugango, ujenzi wa mtambo wa kutibu maji wenye uwezo wa kuzalisha lita za ujazo 35,000 za maji, ujenzi wa njia kuu za kusafirishia maji yenye urefu kwa kilometa 47, ujenzi wa mtandao wa usambazaji maji, ujenzi wa matanki sita ya kuhifadhia maji yenye ujezo wa mita 100 hadi 3,000 na ujenzi wa ofisi za mamlaka eneo la Kiabakari.
Kazi pia zitahusisha ujenzi wa vituo 40 vya kuchotea maji, ujenzi wa mabirika manane ya kunyweshea mifugo, ujenzi wa nyumba za wafanyakazi na mitambo ya kusukumia maji, ujenzi wa nyumba za mitambo na ufungaji wa pampu, ujenzi wa vituo vya kusukumia maji, nyumba za walinzi na ununuzi wa dira za maji.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji, Mugango — Kiabakari – Butiama, Mhandisi Cosmas Sanda, anasema hapo awali kulikuwa na uchakavu mkubwa wa mitambo na miundombinu iliyosababisha kukosekana kwa upatikanaji wa maji safi na salama ya uhakika kwa wananchi wasiopungua 76,000 wa maeneo hayo.
“Ujenzi huu ukikamilika upatikanaji wa maji utaongezeka kutoka asilimia 67 kwa sasa hadi kufikia asilimia 100, na zaidi ya wakazi 164,924 watapata huduma bora ya maji na kuchangia kuinua uchumi wa sekta nyingine zinazotegemea maji, ikiwemo viwanda, elimu, utalii, pamoja na afya,” anasema.
Neema Shabani, mkazi wa Kiabakari anabainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo kutawaepusha na changamoto ya ndoa kuingia katika migogoro, kwani watapata maji kwa haraka tofauti na sasa ambapo upatikanaji wa maji una changamoto kubwa.
“Nia yetu kina mama ni kuona tunaondokana na matatizo ya maji ambayo kwa kiasi kikubwa yanatukabili katika maeneo yetu na kutusababishia wakati mwingine kutolewa lugha chafu na waume zetu, wakitutuhumu kwamba tunatoka nje ya ndoa, kumbe muda mwingi tunautumia kutafuta maji,” anabainisha.
Kwa upande wake mkazi wa Kiabakari, Naomi Mwita, anasema kukamilika kwa mradi huo kutawasaidia wanafunzi katika shule mbalimbali kutotumia muda mwingi kutafuta maji na badala yake kutumia muda huo katika masomo yao, hivyo kuinua ufaulu.
 
–tamati—
 
 
Mkurugenzi wa Metito Overseas Limited, Ahmed Farouk (kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya maji, Prof. Kitila Mkumbo, wakisaini makubaliano ya ujenzi wa mradi wa maji utakaohudumia wakazi wa vijiji 20 vya wilaya za Musoma Vijijini na Butiama.

Mwisho

By Jamhuri