DAR ES SALAAM

NA ALEX KAZENGA


Kuna fursa nyingi za kiuchumi na kimazingira ambazo zimejificha katika taka ambazo kimsingi zinaonekana hazina faida yoyote katika jamii.
Hayo yamebainika katika maonyesho ya siku mbili ya wajasiriamali wa mazingira nchini.
Katika maonyesho hayo yaliyofanyika Desemba 11 na 12 katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, wajasiriamali hao wameonyesha shughuli mbalimbali za utunzaji wa mazingira ikiwemo urejelezaji wa taka.
JAMHURI limefika katika maonyesho hayo na kushuhudia fursa adhimu zilizojificha kwenye taka zinazoonekana kuzagaa kila mahali. Moja ya mambo yaliyoonyeshwa ni jinsi taka zinavyoweza kugeuzwa kuwa ajira ya kujiongezea kipato kwa watu mbalimbali katika jamii kama walivyofanya wajasiriamali hao.
Miongoni mwa washiriki wa maonyesho hayo ni Kampuni ya Tanpack inayojishughulisha na urejeleshaji karatasi nyeupe zilizotumika na maboksi ya kufungia mizigo kuwa bidhaa zinazouzwa tena dukani.
Mbali na kampuni hiyo, JAMHURI limeishuhudia Kampuni ya Maisha High Group inayotengeneza chakula cha kuku na nguruwe kiitwacho Green Feed kwa kutumia funza, mende, maganda na mabaki ya vyakula.
Ofisa Masoko wa Tanpack, Jacqueline Kaizilege, anasema umefika wakati kwa Watanzania kuyaelewa vema mazingira yao na kutumia fursa za vitu vinavyowazunguka kuboresha maisha yao.
Anaeleza kuwa Kampuni ya Tanpack inajishughulisha moja kwa moja na masuala ya usafi wa mazingira ya nyumbani na kupitia mwanya huo wameweza kuzalisha bidhaa mbalimbali za usafi wa nyumbani.
“Lengo letu ni kuhakikisha mazingira ya nyumbani yanatunzwa ipasavyo kwa afya ya kila mtu.
“Kinachotakiwa kwa sasa ni kuwaelimisha Watanzania kujali mazingira na wasiwadharau wazoa taka,” anasema Jacqueline.
Anaongeza kuwa kwenye taka kuna fursa za ajira endapo Watanzania wataelimishwa namna ya kutenganisha taka, kwani kila taka ina umuhimu wake.
“Watanzania wakielimishwa wakajua jinsi ya kutenganisha taka, fursa za ajira zinaweza kuongezeka na watu kujiongezea kipato, pia uchumi wa nchi utakua kwa kasi,” anasema.
Anasema kwa asilimia kubwa bidhaa wanazozalisha ni taka za karatasi na maboksi huku akionyesha karatasi mbalimbali laini za kuijifutia (tissues) zilizozalishwa kutokana na mabaki ya karatasi za mitihani ya wanafunzi.
Anasema wanazalisha karatasi laini za kujifutia mikono na midomo, karatasi laini za jikoni (kitchen towel), karatasi laini za mikono tu (hand towel), karatasi za chooni na karatasi laini kwa ajili ya kufutia vioo vya magari, kusafisha uso na kuweka maofisini.
Mbali na bidhaa hizo anasema wanarejelesha maboksi yanayotupwa katika masoko mbalimbali na kutengeneza bahasha za kaki na karatasi za kujaladia madaftari kwa ajili ya wanafunzi.
Anawaasa Watanzania kutunza mazingira, kwani yakiachwa bila kutunzwa huenda ukafika muda nchi ikaingia kwenye gharama ya kununua hewa ya oksijeni kama zinavyofanya nchi ambazo zinakabiliwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira.
Naye, Mwenyekiti wa Maisha High Group, Rwihula Daniel, anasema kampuni yake inajishughulisha na usindikaji wa taka na uzalishaji wa vyakula lishe kwa ajili ya mifugo.
Anasema malighafi wanayotumia kuzalisha chakula hicho ni wadudu aina ya funza na mende pamoja na mabaki ya vyakula.
“Kwa kutumia maganda ya vyakula kama viazi, mihogo, ndizi, nyanya na vitunguu tunazalisha unga lishe kwa ajili ya chakula cha kuku na nguruwe. Tunavikausha vyote kwa pamoja kwa kutumia mashine kisha tunasaga unga wake tunachanganya na funza ama mende waliosagwa na kutengeneza chakula cha Green Feed,” anasema Daniel.

572 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!