Na Mwandishi Wetu ,JamhuriMedia, Tabora

Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilayani Sikonge mkoani Tabora imemwachia huru Afisa Muuguzi daraja la II wa Hospitali ya wilaya hiyo Rayson Duwe aliyekuwa akikabiliwa na shitaka la kubaka mama mjamzito aliyekuja kupata matibabu hospitalini hapo.

Afisa Muuguzi huyo alifunguliwa shauri namba 18 la mwaka 2023 baada ya kutuhumiwa kumchoma sindano ya usingizi mama huyo aliyekuwa na ujauzito wa miezi 9 na kumuingilia kimapenzi pasipo ridhaa yake.

Akisoma hukumu hiyo juzi Hakimu Mkazi Mwandamizi wa wilaya hiyo Irene Lyatuu amesema ushahidi wa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha tuhuma zinazomkabili muuguzi huyo za kumbaka mteja wake aliyekuja kupata matibabu.

Amesema jumla ya mashahidi saba wa upande wa Jamhuri walifika mahakamani hapo kutoa ushahidi wao akiwemo daktari, lakini ushahidi wao uliibua hoja zilizokinzana kuanzia tarehe na muda tukio lilipotendeka.

Miongoni mwa hoja zilizokinzana ni pale shahidi wa kwanza (mama mjamzito mwenyewe) aliposema kuwa alibakwa tarehe 10 mwezi wa 6 majira ya saa 5 usiku ikiwa ni siku ya pili baada ya kufika hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu.

Shahidi wa pili ambaye ni Muuguzi hospitalini hapo amedai tukio hilo lilitokea tarehe 9 mwezi wa 6 majira ya saa 2 usiku huku shahidi wa tatu akidai lilitokea majira ya saa 4 usiku tarehe 9 Juni.

Amebainisha kuwa mashahidi wote waliopanda kizimbani hapo kutoa ushahidi wao hakuna aliyeweza kuthibitisha kwamba Muuguzi huyo alibaka mteja wake (mama mjamzito) aliyekuja kupatiwa matibabu hospitalini hapo.

Kufuatia ushahidi huo Hakimu Mwandamizi Irene alijaribu kupitia mashauri mbalimbali na kulinganisha na shauri hilo ili kutoa uamuzi wa tukio hilo, alisema upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha tuhuma hizo hivyo mahakama ina mwachilia huru.

Nje na mahakama, Mawakili wa upande wa utetezi walieleza kufurahishwa na uamuzi wa mahakama hiyo na kuongeza kuwa hakimu amemtendea haki mteja wao huku upande wa Jamhuri ukieleza kuwa wana dhamira ya kukata rufaa.

By Jamhuri