MWAKA MMOJA MADARAKANI… Rais Mwinyi kuwalipa waliotapeliwa ‘DECI’

ZANZIBAR

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuwalipa watu waliotapeliwa mabilioni ya fedha kwa njia ya upatu.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja wa uongozi wa Awamu ya Nane ya Zanzibar (SMZ), Mwinyi anasema utapeli huo uliofanywa na Kampuni ya Masterlife umeathiri sana mzunguko wa fedha.

“Kampuni hii ilikusanya Sh bilioni 38.7 kutoka kwa wananchi wapatao 10,317, wengi wao wakiwa ni wananchi wanyonge.

“Idadi hii ya watu na kiwango hicho cha fedha ni kikubwa mno kwa watu maskini na kimesababisha kundi kubwa la wananchi kupata matatizo makubwa ya kiuchumi. 

“Serikali imefanya uamuzi wa kuwalipa wananchi hawa amana walizoweka baada ya kufanya uhakiki. Lengo ni kuwasaidia waathirika hawa ambao maisha yao yameathiriwa sana na tatizo la kitapeli,” amesema Rais Mwinyi. 

Utapeli huo unafanana na ule uliowahi kufanywa miaka takriban 10 iliyopita na Kampuni ya DECI ya jijini Dar es Salaam na kuwaachia umaskini mamia ya wananchi.

Dk. Mwinyi anasema: “Serikali itaendelea kukamata mali za kampuni na za wakurugenzi wake kufidia fedha zitakazotolewa. 

“Hadi sasa Sh bilioni 6.7 zimepatikana kutoka kwenye akaunti zao.”

Kwa upande mwingine, Dk. Mwinyi amesema Sh bilioni 230 zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) zitatumika kuimarisha sekta za afya, elimu, maji safi na salama, nishati na uwezeshaji wananchi kiuchumi. 

Anasema katika kuimarisha sekta ya afya wametenga jumla ya Sh bilioni 69 kutekeleza miradi ya kuimarisha miundombinu ya afya, ikiwamo ujenzi wa hospitali mpya ya ngazi ya mkoa katika Mkoa wa Mjini Magharibi katika eneo la Lumumba.

Anasema hospitali hiyo itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 200 kwa wakati mmoja na ikiwa ya ghorofa tano na itawekwa vifaa tiba vya kisasa, ikiwamo CT scan, MRI, huduma za uchunguzi wa maabara za kisasa na huduma za afya za dharura na uwezo wa kutoa huduma mbalimbali za kibingwa ikiwamo za macho na meno.

 “Utekelezaji wa mipango yetu mikuu ya  maendeleo pamoja na ahadi nilizotoa wakati wa  Uchaguzi Mkuu lakini kwa bahati mbaya sana hatukuweza kuzitekeleza kama tulivyotarajia kutokana na athari nyingi za kiuchumi na kijamii zilizotokana na kuibuka kwa Uviko-19 au corona kama ilivyozoeleka,” anasema na kuongeza:

“Hali hii imezifanya serikali zetu zote mbili  kuumiza vichwa kutafuta hatua gani za kuchukua ili kujikwamua kutoka hapa tulipo, ndipo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikaomba mkopo kutoka IMF kwa ajili ya kufufua uchumi wetu na Zanzibar imetengewa dola milioni 100 za Marekani sawa na shilingi bilioni 230.

 “Miongoni mwa masharti ya mkopo huo ni kwamba zitumike zaidi katika kuimarisha sekta zilizoathiriwa na corona ikiwamo afya ambayo tumeitengea Sh bilioni 69. Kwa kuzingatia masharti ya mikopo, fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kupunguza athari za corona kwa uchumi na maisha ya wananchi kwa kuimarisha miundombinu ya sekta ya afya.”

Katika hatua nyingine, anasema hospitali hiyo mpya ya ngazi ya mkoa itakuwa na kliniki na wodi za kulaza wagonjwa kwa lengo la kuongeza wigo wa kutoa huduma bora na kupunguza idadi ya wanaokwenda Hospitali ya Mnazi Mmoja itakayoendelea pia kuboreshwa kupitia msaada wa Benki ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (BADEA) ili ikidhi hadhi ya kuwa ya rufaa. 

Anasema ujenzi wa Hospitali mpya ya Lumumba utagharimu Sh bilioni 14 na utaanza mara moja.

Pia anasema serikali yake imeamua kwa makusudi kutumia fedha hizo kuiboresha kwa kuipatia Hospitali ya Abdalla Mzee iliyopo mkoani Pemba vifaa vya kisasa na madaktari wataalamu wa kutosha na kuipandisha hadhi kuwa hospitali ya mkoa ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi  wa Mkoa wa Kusini na Pemba kwa ujumla.

 Anasema serikali itajenga hospitali 10 katika ngazi  ya wilaya zenye uwezo wa kulaza wagonjwa 100 kwa wakati mmoja kila moja na kujenga nyumba za wafanyakazi zitakazotosha kuhudumia familia  16 kwa gharama ya Sh bilioni 22.  

Dk. Mwinyi anasema hospitali hizo zitajengwa  katika wilaya zote za Unguja na Pemba isipokuwa  kwa Wilaya ya Mkoani itakayohudumiwa na Hospitali ya Mkoa na kazi za ujenzi wa hospitali hizo zitaanza Desemba, mwaka huu.

“Hospitali hizi zitatoa huduma za uchunguzi kwa kutumia vifaa vya kisasa (X-ray ya kijiditali, ultrasound na maabara za kisasa),” anasema na kuongeza:

“Huduma zitakazopatikana katika hospitali hizi ni za ICU, magonjwa ya wanawake, upimaji wa mimba, uzazi wa kawaida na huduma za upasuaji.”  

Anasema serikali itanunua magari 12 ya kubebea wagonjwa (ambulances) na zitasambazwa katika hospitali zote za wilaya na mbili za mkoa na itanunua magari matano ya kusambazia dawa katika hospitali na vituo vya afya vya Unguja na  Pemba kutoka Bohari ya Dawa (MSD).

Aidha, anasema serikali itanunua mitambo ya kuchomea taka za hospitali (incinerators) kwa  hospitali zote za wilaya na mikoa, na miwili kati  ya hiyo itakuwa yenye uwezo mkubwa wa kuchoma taka nyingi hatarishi kwa wakati mmoja  na itafungwa katika hospitali za mikoa.

Anasema huduma za damu salama zitaimarishwa  kwa kupatiwa vitendea kazi muhimu vinavyoendana na mahitaji husika ili kutoa huduma muda wote kwa kuwa Kitengo cha Damu  Salama kwa sasa hakina vifaa hivyo.

Pia anasema serikali itanunua mitambo miwili  katika hospitali za Pangatupu na Abdalla Mzee ya kuzalisha hewa tiba (oxygen) huku kila mmoja ukiwa na uwezo wa kuzalisha mitungi 400 kwa siku na itatumika katika hospitali nyingine za Unguja na Pemba zitakazohitaji huduma hiyo.

Kwa upande wa sekta ya elimu, anasema wameamua kuelekeza Sh bilioni 69.0 kwa ajili ya kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali kwa lengo la kuimarisha kiwango cha elimu inayotolewa hapa nchini. 

Kwa kutumia fedha hizo, anasema serikali itakamilisha ujenzi wa madarasa 425 yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi na utagharimu Sh bilioni 7.656.

 Anasema wanakusudia kujenga madarasa mapya 706 katika wilaya zote 11 za Unguja na Pemba kwa ngazi ya awali, msingi na sekondari yatakayokuwa mapya. 

“Yatajengwa kupitia ujenzi wa shule mpya 35 zikiwamo 22 za awali (mbili kwa kila wilaya) na 13 za msingi na sekondari. Saba kati ya hizo zitakuwa  ni za ghorofa na zitajengwa katika maeneo ya Mwanakwerekwe, Mtopepo, Bweleo na Kwahani kwa Unguja,” anasema na kuongeza:

 “Mwambe, Kwale na Makangale kwa Pemba. Shule mbili zitajengwa eneo la Jendele kwa Unguja na Chakechake kwa Pemba zitakazokuwa  ni maalumu kwa ajili ya elimu mjumuisho.”

Anasema maeneo mengine ya ujenzi wa shule hizo ni Mpendae, Kipapo, Pujini na Mgelema na utagharimu jumla ya Sh bilioni 43.973.

Aidha, anasema wameelekeza Sh bilioni 6.871  kwa ajili ya ujenzi wa vyoo 1,693 vya wanafunzi  katika ngazi zote za elimu na Sh bilioni 7.898 zitatumiwa kwa kufanya ukarabati wa shule 22 na kati ya zitakazofanyiwa matengenezo makubwa ni Haile Sellasie, Chaani, Mlimani, Matemwe na Uzini kwa Unguja na Konde, Chasasa na Kiwani Mauwani kwa Pemba. 

Anasema watanunua madawati 8,000 kwa shule za msingi yatakayogharimu Sh bilioni mbili na watajenga nyumba 10 za walimu katika maeneo  ya visiwa 34 vidogovidogo vikiwamo Tumbatu,  Uzi, Njau, Kokota na Ng’ambwa na utagharimu Sh milioni 600 na utaanza Desemba, mwaka huu.

Kuhusu sekta ya maji, anasema wametenga  Sh bilioni 34.2 zitakazotumika kuongeza uzalishaji  wa maji kwa kuchimba jumla ya visima 28 Unguja  na Pemba na vitazalisha jumla ya lita milioni 14.1 kwa siku na kazi hiyo itagharimu Sh bilioni 2.1. 

Aidha, anasema serikali itatumia Sh bilioni 1.5  kwa ajili ya kuviendeleza visima 36 Unguja na  Pemba vilivyochimbwa kupitia mradi wa Ras Al Khaimah huku vikitarajiwa kuzalisha lita milioni 15.7 za maji kwa siku. 

Anasema watavifanyia ukarabati visima 49  vilivyowekewa pampu zilizo chini ya kiwango katika maeneo ya Unguja na Pemba na vinatarajiwa kuzalisha lita milioni 23.4 za maji  na kazi hiyo itagharimu Sh bilioni 6.9.

Pia anasema kupitia fedha hizo wamepanga kubadilisha mabomba ya maji chakavu na  kusambaza mapya kwa maeneo yasiyo na huduma na jumla ya kilomita 319 zinatarajiwa kuboresha mtandao huo. Gharama yake ni Sh bilioni  8.2.

Kadhalika, anasema wametenga Sh milioni 210  kwa ajili ya kukarabati matenki kwa Unguja na Pemba ili kuongeza kiwango cha uhifadhi wa maji.

 Anasema Unguja utafanyika ukarabati kwa matenki mawili na Pemba tenki moja na yote yana  uwezo wa kuhifadhi lita milioni 3.2 za maji.

 Pia anasema wametenga Sh bilioni 12.4 kwa ujenzi wa matenki mapya tisa yenye ujazo wa  lita milioni moja kwa kila moja huku Unguja wakijengewa matano na Pemba manne na jumla ya lita milioni 9.2 za maji zinatarajiwa kuhifadhiwa.

Kwa upande wa nishati, anasema serikali imetenga Sh bilioni 11 kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi changamoto za sekta ya umeme.

Anasema fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kuwapunguzia gharama za kuunganisha umeme wananchi Unguja na Pemba huku wastani wa wateja 30,000 wanatarajiwa kufikiwa. 

“Hii itajumuisha ujengaji wa miundombinu ya umeme mkubwa pamoja na ununuzi wa vifaa mbalimbali vitakavyotumika katika kazi hizo,” anasema na kuongeza:

“Katika mpango huo, mwombaji wa umeme  atachangia shilingi 200,000 badala ya shilingi 600,000 na gharama zilizobaki zitafidiwa na  serikali, huku lengo la uamuzi huo ni kupunguza gharama za uungaji wa umeme kwa wananchi na kuweza kumudu huduma hiyo kwa maisha yao.”

Katika sekta ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, anasema serikali imetenga Sh bilioni 85.4 kwa shughuli za kuwawezesha wajasiriamali katika uchumi wa bluu na nyingine za uwezashaji. 

 Pia anasema ameelekeza watumie Sh bilioni 36.5 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wa sekta ya uvuvi na mazao ya baharini. 

Kati ya fedha hizo, anasema Sh bilioni 20.36 zitatumika kuwapatia wavuvi wadogo wadogo boti 577 za kisasa zenye vifaa vyote muhimu vya uvuvi, ikiwamo mitego ya kisasa ya kuvulia na majokofu ya barafu.

Pia anasema wametenga Sh bilioni  2.5   kuwaendeleza wakulima wa mwani na boti 500 zitanunuliwa na Sh bilioni  1.7 zitatumika  kununulia vifaa kwa ajili ya kuendeleza zao hilo. 

Katika hatua nyingine, anasema serikali  itakamilisha ujenzi wa Kiwanda cha Mwani Pemba kwa thamani ya Sh milioni 500 kwa lengo la kusaidia uongezaji wa thamani ya zao hilo. 

Pia anasema wametenga Sh bilioni 1.1 za kuviwezesha vikundi 100 vya ufugaji wa majongoo ya bahari vilivyopo Unguja na Pemba.  

Anasema Sh milioni 402 zitatumika kuendeleza vikundi 60 vya ufugaji wa kaa na Sh bilioni 1.2 zitatumika kuwawezesha wafugaji na vikundi 40 vitanufaika na mpango huo.