Nimewasikia viongozi wangu wa chama tawala na nimewasikia viongozi wangu wa vyama vya upinzani. Wote wanazungumzia utendaji kazi wa Rais wangu, John Pombe Magufuli, katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Novemba 5, 2015 hadi Novemba 5, 2016.

Sina budi kukiri hadharani masikio yangu yamepokea manung’uniko na lawama kutoka kwa baadhi ya watu, na pia yamepokea maridhawa na heko kutoka kwa wananchi kuhusu utendaji kazi wa Rais, Dakta John Pombe Magufuli.

Nimeona na nimesiki11215697_1167859589910086_8793861981273459784_na mazungumzo yaliyonipa furaha na yaliyonipa kichefuchefu kutoka katika makundi hayo. Kwangu, lililo la msingi na bora Rais wangu ametenda mema au mabaya  kwa nia ya kuwakomboa wananchi  kutoka katika umaskini au kwa hisia zake za kujifurahisha.

Mazungumzo ya wananchi hao nayaweka kwenye mizani na kupima utendaji wake Magufuli una asili ya kauli zake kabla na baada kuwa Rais wa nchi hii, au una asili ya matukio ya wananchi baada ya yeye kuwa Rais wa Tanzania.

Utendaji mzuri au mbaya wa jambo lolote una asili ya kauli safi au chafu iliyokwishapangwa na dhamira au nia. Kwa mtu muungwana hubeba asili ya dhamira njema, na kwa mtu muovu hubeba asili ya nia mbaya. Wa kwanza anakusudia maendeleo na wa pili anakusudia mfarakano.

Ni ukweli unapotenda jambo fulani, wapo watu watakaokuona mwema na muungwana; na wapo watakaokuona hovyo na si mstaarabu. Maana na tafsiri ya hayo hutokana na muono na msimamo wa mtu akupimaye katika mizani yake ya fahamu.

Nimeanza kuzungumza hayo kwa kutaka kuonesha mambo mawili kuhusu Rais Magufuli juu ya uungwana na uwajibikaji wake kwa raia wake. Mambo hayo unapoyazingatia kiutendaji, elewa utatengeneza sifa ya uchapakazi. Usipoyazingatia, fahamu utatengeneza sifa ya uchukivu na uzembe – uungwana na uwajibikaji kwa upande wa kulia, uchukivu na uzembe kwa upande wa kushoto. 

Sifa hizo hutoa chambi kwa watu wanaokuona na wanaokufuatilia katika kauli na matendo yako. Ima watakupa sifa nzuri au mbaya na hayo ndiyo matokeo yake baada ya kipimo cha fahamu.

Matokeo haya hupenya ndani ya mishipa na misuli ya mwili wako na kujaza fahamu za ubongo wako kutambua na kuamini ulionalo ni kweli na sahihi. Utambuzi huo huwa una subira na busara au una ghadhabu na pupa. Yote mawili hukupa mwanya wa kusema lolote juu ya mtendaji.

Tanzania imeshapita katika awamu nne za utawala wa Serikali chini ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,  Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa na Dakta Jakaya Mrisho Kikwete. Kila mmoja alikuwa na namna yake ya kuongoza nchi kidemokrasia.

Marais hao walionekana wakitenda mazuri na mabaya na kumbukumbu zimewekwa vitabuni na kusimuliwa kwenye vikao mbalimbali. Leo Watanzania wanasimulia na kucheka na kusahau machungu kama mwongozo uliopita na kukumbuka mema kama dira ya maendeleo yao yajayo.

Awamu nne zilizopita tulizitia katika mizani na kupima uwezo na ubora wake ndani ya miaka 23 (ya Nyerere) na miaka kumi kumi (ya Mwinyi, Mkapa na Kikwete). Ukweli baadhi ya Watanzania walilamba tamutamu na wengine walimeza ladha chungu bila kumung’unya wala kutema. Sasa nyoyo baridi.

Leo Watanzania tumo katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Rais Dakta John Pombe Magufuli. Ndani ya mwaka mmoja Watanzania wameshaonja radha tamu na chachu kama vile katika awamu nne zilisopita. Hapa yakupasa kutafakari kwa undani  bila shaka utapata jibu maridhawa.

Serikali hii imeonesha dalili ya kutumia chachu katika kuchachisha (kubadili) au kuongeza ukali katika kuleta maendeleo ya watu wote waweze kulamba tamutamu kihalali. Mchakato huu ni moto kwa waliozoea kulamba tamu lakini baridi kwa waliolambishwa chungu. Na hapa ndipo penye mizani.

Ufisadi unatapatapa. Rushwa inakimbizwa na halali inaonekana. Dili zimezikwa na kilio kinasikika. Dharau inapotea na heshima inashika nafasi yake. Nidhamu na uwajibikaji zinaranda makazini. Kodi zinakusanywa na mapato yanaonekana. Uchumi unakuwa na mipango inatekelezwa. Wawekezaji wanamiminika na harufu ya ajira inavutika. Umasikini baibai.

By Jamhuri