Mwaka 2019 ni mwaka ambao Tanzania imeshuhudia uzinduzi wa miradi mingi mikubwa pengine kuliko mwaka wowote tangu nchi ipate Uhuru Desemba 9, 1961.

Hata hivyo, wakati baadhi ya watu wakiisifu Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi hiyo chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, wengine wametoa tahadhari kuwa namna miradi hiyo inavyotekelezwa kunaweza kuleta matatizo makubwa siku zijazo.

Haji Semboja, Profesa wa uchumi, amemmwagia sifa Rais Magufuli na serikali yake kwa kinachofanyika kuwa kitaacha alama kubwa kwa nchi katika kipindi kirefu kijacho.

Kwa upande wake, Profesa Abdallah Safari, ameliambia JAMHURI kuwa ingawa kuanzisha miradi mikubwa ni jambo jema, lakini kumekuwa na upendeleo katika miradi hiyo kiasi kwamba suala hilo linaweza kuwagawa Watanzania muda si mrefu.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, anasema bila kujali maendeleo ya watu ni hatari. Anasema kwa sasa watu wengi wamerudi katika maisha ya kula mlo mmoja, huku wengine wakiuza mali zao ili kupata chakula.

Baadhi ya vyanzo vinasema kuanzishwa kwa miradi mingi mikubwa kwa wakati mmoja kunaathiri hali ya uchumi wa nchi kwa wakati uliopo, wakitolea mfano wa kushuka kwa urari wa biashara kati ya bidhaa ambazo nchi inaagiza nje ya nchi na zile zinazouzwa nje.

Wachambuzi wa uchumi wanasema kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa Tanzania imekuwa ikiagiza biadhaa nyingi nje ya nchi kuliko inavyouza, hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa utangamano wa uchumi.

Pamoja na hayo, mwaka 2019 Watanzania wameshuhudia serikali ikianzisha miradi mingi mikubwa, inayotajwa kuwa ya kimkakati, miradi ambayo ina nafasi ya kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Mwaka 2019 unaomalizika leo, Watanzania wameshuhudia serikali ikihamia Dodoma, jambo ambalo kwa zaidi ya miaka 40 lilibaki katika makaratasi, kiasi cha watu wengi kuamini kuwa haliwezi kutekelezwa.

Mradi mwingine ambao watu wengi walifikia hatua ya kuamini kuwa hauwezi kutekelezwa, lakini Serikali ya Awamu ya Tano imeanza kuutekeleza ni ujenzi wa Bwawa la Nyerere katika Mto Rufiji, ambalo awali lilifahamika kama Stiegler Gorge ambalo litazalisha megawati 2,115 za umeme litakapokamilika.

Mradi huu ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi, kwa nchi zilizoendelea duniani matumizi ya umeme ni kati ya megawati 50,000 na 200,000. Marekani na China zinatumia megawati 500,000 kila moja. Tanzania kwa sasa kabla ya bwawa hili ina uwezo wa kuzalisha megawati 1,500.

Kama ilivyo kwa uamuzi wa serikali kuhamishia makao yake makuu Dodoma, mradi wa Stiegler pia ulibuniwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere zaidi ya miongo minne iliyopita. Hata hivyo, utekelezaji wa mradi huu ulikwama kwa miaka yote hiyo kwa sababu mbalimbali.

Wakati wa Mwalimu Nyerere ilielezwa kuwa nchi haina mahitaji makubwa ya umeme. Miaka ya baadaye ikaelezwa kuwa mradi huo ni ghali sana kwa nchi kuweza kumudu kuutekeleza. Baadaye likaibuka suala la mazingira kwa hoja kuwa sehemu inayopaswa kujengwa mradi huo imo katika eneo la Hifadhi ya Urithi wa Dunia inayotambuliwa na UNESCO katika Hifadhi ya Selous.

Lakini muda mfupi baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli akaahidi kuwa atautekeleza mradi huo, na Julai 26, mwaka huu aliweka jiwe la msingi kuanza ujenzi huo unaofanywa na muungano wa kampuni mbili kutoka Misri.

Lakini kabla ya kufikiwa kwa hatua hiyo, serikali ilipitia kipindi kigumu cha kuutetea mradi huo dhidi ya hoja za wanaharakati wa mazingira ambao walidai kuwa faida zitakazotokana na mradi huo ni ndogo ikilinganishwa na hasara zake.

Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi, Rais Magufuli alisema mradi huo utaihakikishia Tanzania umeme wa uhakika katika kipindi hiki ambacho serikali imejikita katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Mradi huo unaojengwa katika Hifadhi ya Selous, mpakani mwa mikoa ya Pwani na Morogoro unaigharimu nchi takriban dola biloni 2.9 za Marekani, sawa na Sh trilioni 6.558 za Tanzania.

Nchi pia iliweka rekodi pale ilipokubaliana na Uganda kujenga bomba refu la kusafirishia mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga.

Aidha, Ni mwaka ambao Watanzania walishuhudia serikali ikitumia fedha taslimu kununua ndege mpya 11 ambazo zimekodishwa kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kama shemu ya jitihada za kulifufua.

Mpaka sasa zimeshanunuliwa ndege mpya tisa, nne zikiwa ni Bombardier Q400, tatu aina ya Airbus A220-300 na mbili kubwa Boeing 787 Dreamliner kwa ajili ya safari za masafa marefu.

Jitihada hizo pia ziliendana na kukamilika kwa jengo la tatu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, likitajwa kuwa ni moja ya majengo ya kisasa kabisa ya kuhudumia abiria katika viwanja vya ndege kwa eneo la Afrika Mashariki.

Kwa nyakati tofauti, Rais Dk. Magufuli ameonyesha kushangazwa kwa nini haya yanayofanyika sasa hayakuwezekana zamani, akisisitiza kuwa Tanzania si nchi maskini ya kushindwa kutekeleza miradi hiyo.

Hiyo inaonyesha kuwa kulikosekama utashi na kumfanya Rais Magufuli kubainisha hadharani kuwa haoni kama kuna Mtanzania mwingine ataweza kuendeleza yale ambayo yeye ameanza kuyafanya pale muda wake madarakani utakapofikia mwisho.

Miradi mingine

Miradi mingine mikubwa ambayo imeanzishwa mwaka huu ni pamoja na upanuzi wa Barabara ya Morogoro kati ya Kimara na Kibaha. Vilevile ujenzi wa barabara za juu katika eneo la Ubungo ili kuondoa tatizo la foleni na msongamano wa magari. Ujenzi huo unakadiriwa kutumia kiasi cha Sh bilioni 247.

Pia, Awamu ya Tano imefanikisha ujenzi wa Daraja la TAZARA jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na Serikali ya Japan.

Kwa upande wa reli, serikali imekwisha kuonyesha dhamira yake ya kuboresha njia ya reli kwa kuanza mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma na Mwanza kupitia Morogoro, Dodoma, Tabora na Shinyanga.

Aidha, hivi karibuni Rais Magufuli amezindua ujenzi wa daraja ambalo litakuwa refu kuliko yote Afrika Mashariki, daraja hilo lenye urefu wa kilometa 3.2 linaunganisha Kigongo na Busisi kupitia Ziwa Victoria. Chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara (Tanroads), ujenzi wa daraja hilo utaigharimu serikali Sh bilioni 582 na kampuni mbili tayari zimeingia makubaliano ya kuanza ujenzi huo na kwamba ndani ya miezi 48 unatakiwa kuwa umekamilika.

Pamoja na mradi huo, pia serikali inatekeleza ujenzi wa meli mpya zitakazofanya kazi katika Ziwa Victoria na Nyasa.

Sambamba na hilo, serikali inafanya ukarabati mkubwa wa meli ya MV Victoria, MV Butiama na ujenzi wa chelezo chenye uwezo wa kubeba tani 4,000.

Kwa upande wa sekta ya afya, serikali inajenga hospitali kila wilaya 67 na vituo vya afya zaidi ya 352, jambo ambalo halijawahi kufanywa na serikali tangu tupate Uhuru.

Wadau wazungumza

Profesa Semboja ameipongeza hatua ya serikali kujikita katika miradi hiyo mikubwa. Anawakosoa watu wanaodai kuwa miradi inawakilisha maendeleo ya vitu badala ya watu, akiwafananisha wakosoaji hao na watu wanaopenda kufika peponi, lakini wanaogopa kufa.

“Kufa ni sehemu ya maisha, huwezi kukikwepa kifo na ukaiona pepo, ni lazima ufe ndipo uione pepo. Anachokifanya rais kwa sasa ni sawa na kifo, anatengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya watu kuja kuishi kwenye pepo baadaye. Lakini watu wanatazama karibu, hawafikirii miaka 10 ijayo,” anasema Prof. Semboja.

Anawataka watu kuacha kuifikiria miradi hiyo kwa mtazamo hasi na badala yake waanze kufikiria namna ya kuitumia miradi hiyo kama fursa ya kujiinua kiuchumi.

“Watu waanze kufikiria namna ya kutumia umeme utakaozalishwa katika mradi wa Rufiji, wafikirie kuanzisha viwanda, wafikirie ni bidhaa gani za kilimo waanze kuzalisha kwa ajili ya kuzisafirisha katika treni ya umeme badala ya kulalama,” anasema.

Anadokeza kuwa nchi nyingine dira ya maendeleo yao ni kuwekeza kwenye elimu au kilimo, lakini Dk. Magufuli yeye ametumia miundombinu ya barabara, reli na nishati kama dira ya kuiletea maendeleo nchi.

“Ni suala la mikakati tu, nchi nyingine zimechagua kuwekeza kwenye kilimo, nyingine kwenye elimu, nyingine kwenye viwanda na sasa zimepiga hatua kubwa. Ni lazima kila serikali iwe na kitu kimoja cha msingi ilichowekeza, Magufuli miradi anayoisimamia kwa sasa inaipeleka Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati,” anasema na kuongeza:

“Kujenga miundombinu ni sawa na uwekezaji, unaweza kuwekeza leo, lakini baada ya miaka 10 ndipo ukaanza kuona faida yake, ndicho anachofanya rais wetu.”

Aidha, anasema kutokana na uongozi wa Rais Magufuli kuwa imara mpaka sasa watu katika ngazi ya familia wameanza kuelewa thamani halisi ya pesa.

“Kila mtu sasa hivi anahangaika kutafuta pesa tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma, vijana wengi walikuwa wakiishi kwa kuwategemea wajomba na shangazi zao wenye nazo, lakini sasa hivi hali imebadilika, kila mtu ni mtafutaji,” anasema.

Kwa upande wake Prof. Abdallah Safari, mtaalamu wa masuala ya sheria, anasema kuwa miradi ya kimaendeleo inayotekelezwa na Awamu ya Tano inatekelezwa kishabiki na haizingatii haki za watu.

“Mwalimu alikuwa na kaulimbiu ya ‘Uhuru na Kazi’, lakini serikali ya sasa hivi yenyewe inahubiri ‘Kazi na Uhuru’, hizi ni kauli mbili tofauti,” anasema Prof. Safari.

Anaongeza kuwa serikali hii inajinasibu kuleta maendeleo, lakini imeshindwa kuzingatia Katiba na Utawala wa Sheria, jambo ambalo haliwezi kustawisha maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Anaikosoa Sera ya Elimu Bure kwamba inaongeza idadi ya waliofika shuleni, na si kuzalisha wasomi, kwa hoja kwamba huduma ya elimu inayotolewa nchini kwa sasa ni ya kiwango cha chini mno.

“Kama maendeleo anayojinasibu kuyaleta rais hayaendani na mawazo ya wananchi wake, hapo ujue kuna kazi kubwa ya kuifikia dira ya nchi. Wanajidai kutoa elimu bure, mbona juzi juzi wamefukuza wanafunzi wa vyuo vikuu waliodai haki yao ya kupatiwa mikopo?” anahoji Prof. Safari.

Hata hivyo, anasema utekelezaji wa miradi mikubwa nchini utachangia nchi kutoendelea kwa kasi inayotakiwa, kwani inatumia kiasi kikubwa cha fedha zake za kigeni kuagiza vitu nje huku uuzaji nje wa bidhaa zinazozalishwa nchini ukiwa mdogo.

“Wachina wamekuwa matajiri kwa kuuza na kununua vitu vyao vya ndani wanavyotengeneza wenyewe. Hawaagizi bidhaa kutoka nje, wao wanatengeneza vitu vyao, sasa sisi tukiagiza sana vitu nje, maana yake kinachotumika kuagiza vitu hivyo ni akiba yetu, tunaowafaidisha ni wageni,” anasema Prof. Safari.

Kana kwamba anamjibu Prof. Safari, mtaalamu wa masuala ya uchumi aliyeomba asitajwe gazetini, ameliambia JAMHURI kuwa Tanzania inachofanya kwa sasa ni sahihi. “Kinachoagizwa nje ya nchi ni mitambo itakayoliwezesha taifa kuzalisha bidhaa hapa hapa nchini na kuwauzia watu wake, kisha ziada kuuzwa nje ya nchi. Ukiangalia bidhaa zinazoingizwa nchini ni mtaji utakaoliondoa taifa katika utegemezi. Hivyo wanaosema tunatumia fedha za kigeni kuagiza bidhaa nje, wana upofu wa fikra au uelewa mdogo juu ya misingi ya uchumi,” anasema.

Kwa upande wake, mchambuzi mwingine, Gaudence Mpangala, anaielezea miradi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano kuwa ni mizuri, lakini inayohitaji utaratibu mzuri wa kuitekeleza.

“Miradi mikubwa kuitekeleza kwa wakati mmoja si mbinu nzuri kwa maendeleo ya nchi. Hapa mapato ya nchi yataathirika kwa kisasi kikubwa kwa kufanya kazi mbili, yaani kuendeleza miradi na maisha ya watu,” anasema Mpangala.

Anasema nchi kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi hiyo ilitakiwa kuanza na mradi wa kuzalisha chuma cha Mchuchuma na Liganga kwa ajili ya kujenga viwanda mama ambavyo vingezalisha maligahafi.

“Chuma cha kutekeleza hii miradi tunakiagiza nje wakati kipo, madhara yake hela ya kuendeleza maisha ya watu inapungua, mwisho wa siku watu wanaanza kulalamika hela kukosekana mtaani,” anasema.

Anabainisha kuwa yalifanyika makosa kwa kuivunja Tume ya Mipango ya Taifa kwani ndiyo ingetoa dira ya miradi inayotakiwa kutekelezwa kwa kuzingatia mahitaji ya watu na uchumi wa nchi.

By Jamhuri