Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia,Pwani

Walimu 4,900 wanatarajia kufikiwa na kunufaika na mafunzo ya utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu ya awali na msingi unaotarajia kuanza rasmi Januari 2024.

Zoezi hilo linaendelea kwenye baadhi ya mikoa nchini kwa lengo la walimu wa somo hilo kunolewa ipasavyo ili kuweza kuwa na mbinu za ufundishaji na ufunzaji.

Mkurugenzi wa mafunzo wa Mtaala kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt.Fika Mwakabungu alieleza kuhusu zoezi hilo linavyotekelezwa , wakati akifunga mafunzo ya uboreshaji na ujifunzaji wa somo la kiingereza kwa walimu 100 kutoka halmashauri ya Chalinze na Kisarawe Mkoani Pwani.

Alieleza, mikoa inayonufaika ni pamoja na mkoa wa Iringa ambapo Jumla ya walimu 1,832 wamepata mafunzo hayo ,walimu 2,100 wa Jiji la Mwanza , Dar es salaam na mkoa wa Pwani walimu 1,110.

“Tuendelee kuishukuru Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kutoa kibali ili kuruhusu kufanyika mafunzo haya kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania TET katika mradi wa Shule Bora “alifafanua Mwakabungu.

Vilevile Mwakabungu anasisitiza matumizi ya TEHAMA kusaidia, kuwezesha walimu kutengeneza sauti zitakazotumika kufundisha mada zinazohusu matamshi ili kuongeza uweledi kwenye ufundishaji wa somo la kiingereza.

Alitoa wito kwa walimu watakaoweza kutamka sauti hizo kwa ufasaha kujirekodi sauti na kuziwasilisha TET ,ambapo watapewa nafasi ya kutengeneza kwa ufanisi zaidi.

Awali Ofisa elimu Msingi halmashauri ya Chalinze, Miriam Kihiyo alisema, walimu hao waende wakatekeleze kwa vitendo waliyoelekezwa na kuwaasa kulinda maadili yao ya kazi kwani ni kioo cha jamii.

Kwa upande wa walimu walioshiriki mafunzo hayo waliishukuru Serikali na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanyia maboresho mtaala wa elimu ya msingi.

Mwalimu Mary Cloud Kitambi kutoka shule ya Chanzige A Kisarawe alieleza, mafunzo yamemjenga na itakuwa chachu kubadilisha mfumo mzima ambao walikuwa nao katika somo la kiingereza kuwa gumu kulifundisha .

Mwalimu wa taaluma shule ya Msingi Ruvu Darajani Ismail Abdalah Kasikasi alieleza, mafunzo hayo yatamsaidia mwanafunzi kuwa ndie mzungumzaji mkuu .

Borah Hassan shule ya Msingi Kinzagu alisema kuwa, awali kulikuwa na mkanganyiko wa sera sasa watafundisha kwa vitendo na kuanzia darasa la kwanza ili wanafunzi wawe na msingi mzuri wa lugha ya kiingereza kuanzia ngazi ya chini ya kielimu.

By Jamhuri