Na isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar

Bondia Hassan Mwakinyo amesema hana hofu yoyote  na mpinzani wake Mbiya Kanku kutoka DRC Congo, atakayepigana naye Januari 27, 2024, kwani sifa kuu ya taifa hilo ni kucheza bolingo na si ngumi.

Mwakinyo ambaye atapanda ulingoni dhidi ya Kanku katika pambano lililopewa jina la ‘Mtata Mtatuzi’ litakalofanyika ndani ya ukumbi wa ndani wa uwanja wa Amani, amesema anajua mashabiki wake wana kiu ya kumuona ulingoni baada ya muda mrefu ambao hakucheza, hivyo watarajie kuona tofauti ya bondia na yeye ‘Profeshino’

“Maandalizi yangu yana shauku na utayari mkubwa sana wa kuwaonesha Watanzania na Wazanzibar ni nini nilikiandaa kwa ajili yao kwa muda mrefu, mpaka sasa tuna asilimia 98 za hili pambano kuwepo, mpaka tutakapopima uzito ndio zitatimia mia” amesema Mwakinyo

Aidha Mwakinyo amesema chochote kinaweza kutokea ndani ya ulingo japo anatamani kucheza ili kuwafurahisha mashabiki zake na endapo ataamua kumaliza pambano kwa ‘KO’ pia inawezekana kwa sababu sio kitu cha ajabu kwake.

Mbali na Mwakinyo ambaye ndiye atakayecheza ‘Main Card’ dhidi ya Mbiya Kanku, mabondia wengine watakaopigana kwenye pambano hilo ni pamoja na Hussein Itaba kutoka Naccoz gym dhidi ya Juma Misumari, Ally Mkojani wa Zanzibar dhidi ya Juma Kijo, Anuary Mlawa dhidi ya Kato Machemba, wanawake Deborah Mwenda dhidi ya Zulfa Iddy na wengine wengi.

By Jamhuri