Namshukuru Mungu nimeweza kuketi kuandika kumkumbuka Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kipindi hiki cha kumbukizi ya kuzaliwa kwake na kujiuliza swali ambalo bila shaka Watanzania wengine nao wamekuwa wakijiuliza: Mwalimu angekuwapo akaona utendaji wa Rais John Pombe Joseph Magufuli kwenye Awamu hii ya Tano, angesemaje?

Watanzania tuliokuwapo Awamu ya Kwanza tulishuhudia uongozi uliotukuka wa Mwalimu Nyerere. Mwalimu alijikita kwenye kujali na kushughulikia maendeleo ya wananchi wa Taifa lake. Kwa mfano, wakati nchi yetu inapata Uhuru, Mwalimu alichukua uamuzi wa makusudi wa kujenga shule na vyuo mbalimbali na kutoa elimu msingi hadi chuo kikuu ili hata watoto wa wananchi maskini nasi tupate elimu. Alipotoka madarakani asilimia 91 ya Watanzania walikuwa wanajua kusoma na kuandika ukilinganisha na asilimia 19 nchi ilipopata Uhuru. Mwalimu alitoa matibabu bure. Katika kuinua uchumi wa nchi Mwalimu alijenga viwanda vya kila aina, mabwawa kwa ajili ya kuzalisha umeme; alihamasisha kilimo bora na ufugaji wenye tija na alifanya mambo mengine mengi ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Mwalimu Nyerere hakujali nafsi yake, usiku na mchana alikuwa akiwaza na kuhangaikia maendeleo ya wananchi wake. Alikuwa jasiri hakutaka mtu yeyote kutoka nje aingilie uhuru wa nchi yetu. Nakumbuka jinsi ambavyo alikataa kuruhusu watu kutoka nje kuja kuchimba madini yetu. Alisema yabaki huko huko chini hadi Watanzania wenyewe watakapopata ujuzi wa kuyachimba.

Mwalimu Nyerere alipoamua kustaafu na kurudi kijijini Butiama, wananchi walimuaga kwa machozi ya upendo kutokana na uongozi wake uliotukuka na kazi nzuri aliyoifanya kwa taifa.

Nilikuwa miongoni mwa waliopata bahati ya kwenda naye Mwitongo, Butiama kuwa Katibu Muhtasi kwenye ofisi yake ya Rais Mstaafu. Tulipofika, Mwalimu hakuwa anakuja ofisini. Siku moja alikuja ofisini na kutuambia yeye amestaafu, tusione ajabu asipokuja ofisini. Kazi yake sasa ni kilimo, mwenye kutaka kulima amfuate apewe eneo la kulima!

Mwalimu alistaafu kikamilifu na kuweka msisitizo kwamba alikuwa hahusiki tena na mambo ya Serikali. Lakini, alimwambia Rais wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi kwamba endapo atahitaji ushauri wake asisite kumwita Ikulu.

Kwenye makala hii sina uwezo wa kuelezea kwa kina jinsi Awamu ya Pili na Awamu nyingine mbili zilizofuata zilivyoendeshwa. Ninachoweza kusema ni kwamba kwenye Awamu ya Pili, Rais Mwinyi alikuwa kiongozi mpole na muungwana sana. Alidhihirisha uungwana wake pale aliposema kwamba Mwalimu Nyerere ni kama Mlima Kilimanjaro na yeye ni kama kichuguu tu! Lakini, wachambuzi wa mambo ya siasa za nchi yetu wanadai kwamba upole wake ulitumiwa vibaya na viongozi wengine na washauri wake, ndio maana mwishowe alipewa jina la “Mzee Ruksa”.

Yapo mambo ambayo yalimkera Mwalimu Nyerere kwenye uongozi wa Awamu ya Pili. Moja ninalolikumbuka ambalo Mwalimu hakulifurahia lilitokea miezi michache tu baada ya Mwalimu kustaafu uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Agosti 1992. Machi, 1993 Viongozi wa Chama walikutana Zanzibar kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi wakaamua kuondoa Miiko ya Uongozi ndani ya Azimio la Arusha na kutoa Azimio jipya la Zanzibar.

Mwalimu alipozungumzia jambo hilo, alisema nchi zote zilizoendelea duniani ambazo zinajipambanua kuwa zina demokrasia, zina miiko ya uongozi. Kwenye uongozi kunapaswa kuwapo udhibiti wa namna fulani ili viongozi wasio waadilifu wasitumie vibaya nafasi zao. Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanadai kwamba baadhi ya viongozi wa CCM walikuwa wameichoka siasa ya Mwalimu Nyerere ya Ujamaa na Kujitegemea na walitumia upole wa Rais Mwinyi kupitisha azimio hilo ili wapate nafasi ya kufanya biashara na kujilimbikizia mali kwa njia halali na haramu. Utetezi uliotolewa ni kwamba nchi ilipaswa kwenda na wakati katika dhana ya kujenga uchumi. Kwa dhana hiyo biashara holela ziliruhusiwa, mashirika ya umma na viwanda alivyohangaika kuvijenga Mwalimu kwenye Awamu ya Kwanza, ama viliuzwa, au vilibinafsishwa.

Jambo jingine lililomuuma sana Mwalimu mpaka aliamua kuliandikia kitabu ni pale Serikali ya Awamu ya Pili iliposhindwa kulishughulikia ipasavyo suala la viongozi kuanza kuzungumzia Uzanzibari na Utanganyika, wakidai iwepo Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano. Mwalimu aliona jambo lile lilikuwa linahatarisha sana uwepo wa Muungano.

Mimi ndiye niliyechapa kitabu kile tangu mwanzo hadi mwisho. Niliona jinsi jambo hili lilivyomuumiza sana Mwalimu. Aliandika kwa umakini mkubwa kitabu chenye kurasa 69 alichokipa jina la “Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania”. Ilimchukua miezi zaidi ya sita kukiandika. Mwalimu alikuwa anaandika na kurudia-rudia kusoma na kusahihisha, kuhakikisha kwamba anatumia maneno ambayo yataeleweka vizuri kwa wale wote watakaokisoma. Aliporidhika na maandishi yake aliniandikia: “Anna, usinirudishie tena kazi hii!”

Mwishoni mwa miaka 10 ya Awamu ya Pili, Waandishi wa Habari na Watanzania wengine waliokuwa wanaitakia mema nchi yetu, walimuomba Mwalimu azungumze juu ya matatizo yaliyojitokeza nchini ili kusaidia apatikane rais ambaye angeliweza kuyarekebisha. Mwalimu alikubali kufanya hivyo na aliainisha matatizo yaliyojitokeza kwamba ni: Muungano kutikiswa; kukithiri kwa vitendo vya rushwa; kupuuzwa na kutojali Katiba na Sheria za nchi; na kuanza kuwapo ukabila na udini. Hatimaye, Mwalimu alifanya kila lililowezekana apatikane Rais wa Awamu ya Tatu atakayeweza kurekebisha mambo. Akapatikana Rais Benjamin William Mkapa.

Awamu ya Tatu: Mwalimu Nyerere alishuhudia uongozi wa Awamu ya Tatu kwa miaka mitatu na miezi michache tu kabla hajaugua na kuaga dunia Oktoba 14, 1999. Rais Mkapa alikuwa kiongozi mkali aliyejitahidi kutumia uzoefu wake wa mambo ya kimataifa kujenga uchumi wa nchi. Lakini, Mwalimu alitarajia Rais Mkapa atarejesha angalau kwa kiwango fulani siasa zake kwa kuendeleza yale aliyoyasimamia. Mwalimu hakuridhika sana pale alipoona Rais Mkapa anaendeleza sera za ubinafsishaji, utandawazi, soko huria na mageuzi yaliyotokana na matakwa ya vyombo vya fedha vya kimataifa vya ‘IMF, World Bank’, na kadhalika. Hata hivyo, katika uongozi wake, Rais Mkapa alifanya kazi kubwa na nzuri ya kulipa madeni kuifanya nchi ikopesheke na kurejesha heshima nje ya nchi iliyojengwa na Mwalimu.

Awamu ya Nne iliongozwa na Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. Rais Kikwete naye hakuhangaika na siasa za Mwalimu. Kwenye Awamu hii jina la Baba wa Taifa lilikuwa halisikiki kutajwa. Katika suala la kujenga uchumi, Rais Kikwete alitegemea ‘wajomba’ wa nchi za nje watalisaidia Taifa letu. Alitumia fedha nyingi kusafiri sana nje. Watanzania wakampachika jina la Vasco Da Gama. Mwisho wa utawala wa Rais Kikwete, waandishi wa habari wakamwandika sana magazetini kukosoa uongozi wake. Chama Cha Mapinduzi kilipata kazi ngumu ya kutafuta mgombea atakayeweza kushinda uchaguzi na kurekebisha yote yaliyokosewa kwenye awamu zilizotangulia yaliyovaliwa njuga na vyama vya upinzani.

Naamini Mwenyezi Mungu alilitazama Taifa la Tanzania kwa jicho la huruma. Naamini pia kwamba uadilifu na ucha Mungu aliokuwanao Mwalimu Nyerere katika uhai wake ndio uliokiwezesha Chama Cha Mapinduzi kumpata mgombea Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli kuwa Rais wetu wa Awamu ya Tano, aliyekuwa na maono ya kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa utimilifu.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Mtanzania mmoja aliandika Makala kwenye Gazeti la JAMHURI toleo la tarehe 13 – 19 Oktoba yenye kichwa cha habari: “Ndani ya Dk. Magufuli namuona Mwl. Nyerere”. Mwandishi huyu aliandika: “Nimepata muda wa kukaa na Dk. Magufuli kwa nyakati mbalimbali tangu akiwa Naibu Waziri wa Ujenzi hadi sasa anapowania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwanasiasa huyu anayepewa nafasi kubwa ya kushinda kiti cha urais, ni mfuasi mzuri sana wa fikra za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa yeyote anayekaa na Dk. Magufuli ni nadra mno kumaliza nusu saa ya mazungumzo bila kumsikia akilitaja kwa mazuri jina la Mwalimu Nyerere. Kwake yeye, Mwalimu ni ‘role model’ wake kisiasa na kiutendaji kazi…”

Naye Mwandishi wa Habari nguli wa Gazeti la JAMHURI Manyerere Jacton, katika moja ya makala zake, akizungumzia sababu zinazotolewa na wanaohama vyama vya upinzani kwenda CCM, alisema: “….Hawa wanaorejea CCM wanatoa sababu zinazofanana. Wanasifu utendaji kazi wa Rais John Magufuli. Nani asiyejua utendaji kazi wa kiongozi huyu? Mbona sisi kwa miaka zaidi ya 20 tunaujua na tumeendelea kuwa watiifu kwake? Wao walikuwa nchi gani hata wasijue namna alivyofanya kazi za kutukuka akiwa Ujenzi, Ardhi, Uvuvi na kurejea Ujenzi? Walikuwa wapi wakati Rais Benjamin Mkapa akimtaja kama askari wake wa mwavuli?…”

Maandiko ya hawa Watanzania wawili ni wasifu unaoelezea jinsi ambavyo Tanzania imepata kiongozi mchapakazi anayemuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo.

Rais John Joseph Magufuli, amefufua mambo na kuendeleza yale Mwalimu aliyokuwa akiyasimamia.  Rais huyu amekuwa mkali sana katika kupambana na maovu nchini na katika kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayogusa ustawi wa maisha ya Watanzania wanyonge na maendeleo ya nchi yetu.

Rais Magufuli, kama alivyokuwa akifanya Mwalimu Nyerere, amekuwa akiwaza usiku na mchana ni jinsi gani anavyoweza kuwasaidia wananchi wanyonge na kufanya taifa lipige hatua kubwa kimaendeleo. Pengine alipokuwa waziri haikuwa rahisi kwake kufanya aliyokuwa anataka kufanya. Lakini, sasa kutokana na kuwa Rais na muamuzi wa mwisho wa masuala ya nchi, amepata nafasi nzuri ya kutekeleza yale Mwalimu Nyerere aliyoyaachia katikati na kuongezea ya kwake kwa kadri anavyoona inafaa.

Kuyaorodhesha na kuyaelezea yote aliyoyafanya Rais Magufuli ndani ya miaka mitatu tu ya uongozi wake kunahitaji kuandika vitabu na si makala fupi kama hii. Itoshe kusema amekonga nyoyo za Watanzania wanyonge ambao ndio wengi na ndio wanaofurahia uongozi wake kama walivyofanya wale wananchi waliomuaga Mwalimu kwa machozi!

Tukirejea kwenye swali: Mwalimu angekuwepo angesemaje kuhusu uongozi wa Awamu ya Tano, Awamu ya Rais John Pombe Joseph Magufuli? Mimi binafsi naamini Baba wa Taifa letu angefurahi sana kuona amepatikana Rais ambaye ni muumini wa siasa zake za kujali maendeleo ya Watanzania wanyoge ambao ndio wengi, Rais ambaye ameweza kurejea yale aliyoyasimamia yeye na anayafanyia kazi kulingana na mazingira ya wakati uliopo. Pia, naamini uwepo wa Mwalimu ungelikuwa faraja kubwa kwa Rais Magufuli kwa sababu Rais hangesita kutafuta ushauri na msaada wa Mwalimu katika mambo mbalimbali. Mwalimu angelikuwa tayari kabisa kumpa ushauri katika mambo yoyote yale na naaamini kabisa Rais Magufuli angeupokea ushauri wa Mwalimu kwa furaha na kuufanyia kazi.

Mwisho, kwa kuangalia yote yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufuli ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake na juhudi zake za kutaka kujenga Tanzania Mpya kwa ‘ari mpya, kasi mpya, na nguvu mpya’, wasomaji wa makala hii nao nawaomba waangalie yote hayo, wayatafakari ili na wao kwa mtazamo wao watoe jibu la swali: “Kama Mwalimu Nyerere angekuwepo angesemaje kuhusu uongozi huu wa Awamu ya Tano?”

Anna Julia Chiduo-Mwansasu

Mstaafu,

Mkazi wa Yangeyange, Kivule

0655 774 967

Please follow and like us:
Pin Share