Kujiandaa ni kujiandaa kushinda na kutokujiandaa ni kujiandaa kushindwa. Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln (1809 – 1865) anasema: “Ukinipa saa sita ili niukate mti, nitatumia saa nne za awali kuliona shoka langu.”

Hii ni busara inayoonyesha umuhimu wa kujiandaa. Dunia inamilikiwa na watu waliojiandaa kuimiliki. Huwezi kuimiliki dunia bila kujiandaa kuimiliki. Eleanor Roosevelt anasema: “Wakati ujao unamilikiwa na wale wanaoamini katika uzuri wa ndoto zao.” Watu wengi hawafanikiwi kwa sababu hawajiandai kufanikiwa. Usikubali kuwa tajiri wa kushindwa, kubali kuwa tajiri wa kushinda. Acha mawazo ya kushinda yaitawale akili yako. Watu wote waliofanikiwa kiroho, kimwili, kiuchumi na kisiasa walijiandaa kufanikiwa.

Jiandae kufanikiwa. Jiandae kushinda. Jiandae kulinda ndoto yako na kuitimiza. Barabara ya kwenda kwenye mafanikio haikunyooka. Ina vilima, mito na mabonde. Ina kona nyingi. Kuna kona inayoitwa kushindwa. Kuna matuta ya kupunguza kasi yanayoitwa mafariki. Pambana na changamoto ili uibuke kuwa mshindi wa changamoto. Kuna taa nyekundu zinazoitwa adui. Kuna pancha zinazoitwa changamoto. Unahitaji kuwa na tairi la akiba linaloitwa uvumilivu. Wahenga walisema: “Mvumilivu hula mbivu.” Mtu yeyote anayehitaji kufanikiwa ni lazima ajiandae kuvumilia na kukubali kukubaliana na kila aina ya changamoto anazokutana nazo katika safari yake ya kuyaendea mafanikio.

Kutokujiandaa ni kujiandaa kushindwa. Uwepo wako duniani una umuhimu  sana.  Jiandae vema ili uweze kutimiza kusudi lako la kuishi hapa  duniani. Sahau mambo yote lakini kumbuka jambo hili: ‘Hukuumbwa kwa bahati mbaya’. Nakupa  angalizo kuwa hai na kuwepo duniani pasipo kutimiza kusudi la maisha yako ni dhambi. Hii ni dhambi ya kutokutumia vema uwezo na vipawa ulivyojaliwa na  Mwenyezi  Mungu.

Mwaka 2010 nilianza safari yangu ya uandishi wa vitabu. Nilikatishwa sana tamaa.  Nilibezwa sana.  Niliambiwa kwamba, sina  elimu ya kuandika vitabu  na  makala katika magazeti mbalimbali. Nakumbuka kuna siku moja nilimwendea padri mmoja na kumwambia: “Baba padri nina kipaji cha kuandika vitabu.”  Padri huyu alicheka kwa kejeli. Baada ya kucheka kwa kejeli alinitazama usoni na kuniambia: “Wewe huwezi kuandika vitabu.” Majibu ya padri yalinikatisha tamaa lakini hayakunifanya niache kujiandaa kuandika vitabu. Moyoni nilijiambia, haya ni maneno ya binadamu anayeishi chini ya jua. Miaka miwili baadaye nilikutana na yule padri niliyemwendea kwa ushauri halafu akanicheka. Nilikutana naye nikiwa tayari nimetoa chapisho langu la kwanza la kitabu. Padri aliambia: “William, kumbe una kipaji cha kuandika vitabu? Hongera sana.” Mara ya kwanza nilipokutana naye alinikejeli, mara ya pili alinipongeza. Jitie moyo kabla hujatiwa na watu wengine. Jiamini kabla hujaaminiwa na watu wengine. Jipende kabla hujapendwa. Hiyo ndiyo siri ya ushindi katika maisha. Nilichojifunza katika maisha ni hiki hapa: “Ukikubali kukatishwa tama, hautafanikiwa.”

Tafakari ushuhuda huu wa maisha ya Nick Vujicic. Nick Vujicic alizaliwa Desemba 4, mwaka 1984 nchini Australia. Nick Vujicic  alizaliwa akiwa hana miguu wala mikono. Nick Vujicic ameoa mke mmoja anayejulikana kwa jina la Kane Mihayara ambaye walioana mwaka 2012.  Nick Vujicic na mke wake wamejaliwa kupata watoto wanne. Nick Vujicic akiwa na umri wa miaka 10 alimwambia mama yake mzazi maneno haya: “Mama nina nia ya kufanikiwa na nitafanikiwa.” Leo hii dunia nzima inasoma vitabu vya hamasa vilivyoandikwa na Nick Vujicic. Nick Vujicic anafanya mikutano ya kutoa hamasa kwa watu kujituma kufanya kazi. Nick Vujicic ni miongoni mwa mabilionea duniani.

Watu wengi wanatamani kufanikiwa katika maisha yao, lakini wanaogopa kujitoa sadaka kwa ajili ya mafanikio wanayoyataka. Je, una nia ya kufanikiwa kimwili, kiroho, kiuchumi, kifamilia na kisiasa? Jitoe sadaka kwa ajili ya mafanikio  unayoyataka. Fanyika gharama. Mwandishi mashuhuri wa vitabu wa Marekani, Bud Wilson, anasema: “Kama unataka kuwa mshindi lazima ukubali kulipa gharama kubwa.’’ Dunia inamilikiwa na watu wanaokubali kulipa gharama za mafanikio wanayoyataka. Mgunduzi wa mtandao wa kijamii wa facebook, Mark Zuckburg, anasema: “Dunia inabadilishwa na  kumilikiwa na watu wenye nia.”

788 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!