Moja ni mtihani. Kuna nguvu ya moja. Anayefunga goli ni mtu mmoja lakini timu nzima inafurahi. Lakini kwa upande mwingine kosa la mtu mmoja linachafua picha ya kundi zima, samaki mmoja akioza wote wameoza. Kuna nguvu ya moja.

Kuna uwezekano mkubwa mtu kuidharau moja. Kumbuka mdharau mwiba mguu huota tende. Kuna nguvu ya moja. Okoa shilingi moja, shilingi moja itakuokoa. Shilingi milioni moja ina shililingi moja mara milioni moja. Tukithamini shilingi moja tunafanikiwa.

Haba na haba hujaza kibaba. Tone tone hujaza ndoo. Siku moja mbele yako ni nzuri zaidi kuliko miaka kumi nyuma yako (Methali ya Urusi). Siku moja mbele yako unaweza kuitumia kufanya makubwa. Wahenga walisema: “Moja ya mkononi yashinda mia za mbali.” Kitu kimoja ulicho nacho mkononi ni bora kuliko vingi vilivyo mbali. “Nyumba moja imara ni bora kuliko mia ambazo ni magofu.” (Methali ya Kurdistan).

Neno moja linaweza kuwa na nguvu ya ajabu. Kuna mtu aliyemuuliza rafiki yake siri ya umashuhuri wake na kupendwa na watu. Alisema ni kwa sababu ya neno moja “ajabu.” Alisema: “Miaka mingi iliyopita baada ya kusikia jambo ambalo sikubaliani nalo nilizoea kusema ‘upumbavu.’ Watu walianza kunikwepa kama baa. Kwa sasa nimebadilisha neno ‘upumbavu’ na neno ‘ajabu’ na simu yangu kila mara inaita na orodha ya marafiki zangu inaendelea kuwa ndefu.

Hapo tunaona nguvu ya moja – neno moja ‘ajabu.’ Kama mtu mmoja anakusifia, watu elfu moja watairudia sifa (Methali ya Japan). Katika maisha unahitaji mtu mmoja wa kuanzisha mnyororo wa kukutia moyo kupitia sifa. Katika maisha unahitaji mtu mmoja wa kukupendekeza kushika wadhifa fulani. Lakini kinyume chake ni kweli. Mtu mmoja anaweza kutia sumu katika mwonekano wako kwa watu. Mtu mmoja anaweza kushika breki usipate wadhifa fulani.

Nguvu ya moja tunaiona katika muda. Dakika moja ni dakika moja, dakika moja mara sitini tunapata saa moja. Jackson Brown alisema: “…usiseme huna muda wa kutosha. Una namba ya saa kadhaa kwa siku kama waliyopewa Helen Keller, Pastuer, Michelangelo, Mama Theresa, Leonard da Vinci na Albert Einstein.”

Tunaweza kuongeza kuwa una namba ya saa walizopewa kwa siku Bill Gates, Dangote, Donald Trump na Bakhresa. Ukitaka kujua nguvu ya mwaka mmoja muulize mwanafunzi aliyerudia darasa. Ukitaka kujua nguvu ya mwezi mmoja muulize mama aliyejifungua kabla ya mwezi mmoja. Ukitaka kujua nguvu ya wiki moja muulize mhariri wa gazeti linalotoka kila wiki. Ukitaka kujua nguvu ya saa moja waulize wachumba ambao wamepanga kukutana baada ya saa moja.

Safari moja huanzisha nyingine. Ni nguvu ya moja. Kuna aliyemfuga paka. Alimnunulia maziwa kutoka kwa jirani. Baadaye akaona bora afuge ng’ombe wa maziwa ili aweze kupata maziwa kwa urahisi. Ilikuwa shida kupata nyasi za kumlisha ng’ombe akaamua kuanzisha kilimo cha shamba la nyasi. Shamba lilikuwa kubwa hadi akashawishika kuongeza ng’ombe wengine. Ng’ombe walipokuwa wengi alinunua mashine ya kukamua maziwa. Kutokana na samadi ya ng’ombe aliweza kuzalisha gesi. Yote yalianzia kwenye paka mmoja. Tunaona nguvu ya moja.

Nguvu ya moja tunaiona katika mfano. Kuna nguvu ya mfano mmoja. Kinachowafanya batamzinga waruke si kufika kwa adui bali eneo lao, mfano mmoja wa batamzinga anapoanza kuruka wengine wanafuata nyayo. Hiyo ni nguvu ya moja – mfano mmoja. “Mfano ni kitabu ambacho watu wote wanaweza kusoma,” alisema Gilbert West.

1266 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!