Buriani Dk. Mengi

Kifo kimeumbwa, kifo ni faradhi. Kifo ni ufunguo wa kufunga uhai wa binadamu duniani na kufungua maisha ya milele ya binadamu huko ahera (mbinguni). Faradhi na ufunguo umemshukia ndugu yetu mpendwa, Dk. Reginald Abraham Mengi.  Reginald Mengi amefariki dunia.

Ni usiku wa kuamkia Alhamisi wiki iliyopita katika Jiji la Dubai, Falme za Kiarabu, Reginald alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi. Kifo kimezima nuru iliyoanza kung’ara tangu Mei 29, mwaka 1942 hadi mwezi kama huo lakini mwaka huu, 2019 katika akili na mwili wa Reginald.

Maelezo mengi yatasemwa, yatasimuliwa na yataandikwa kuhusu uzawa, makuzi na maisha yake. Utu, kipaji na ukarimu wake havitasahaulika kwetu. Yote ni kuonyesha ishara ya upendo, thamani na umuhimu wake. Hakika alikuwa mtu wa watu.

Marehemu amekamilisha hatua tatu za binadamu kuishi. Kabla ya kuja duniani, kuishi duniani na kwenda kuishi ahera (mbinguni). Amekamilisha matendo yake duniani na sasa anasubiri hesabu zake kwa Mwenyezi Mungu. Wewe na mimi bado, lakini tujiandae kwa safari ya ahera (mbinguni).

Watanzania tumejaa huzuni na machozi kutiririka mashavuni, tunayempenda katutoka na tunamkumbuka. Nuru ya miaka 77 tuliyoizoea haipo. Kifo kimeifungia na kimetufungulia mauti. Hatuyapendi mauti lakini ni lazima kwetu, kwa sababu kila nafsi itaonja mauti.

Umbo lake hatutaliona milele. Cheko lake hatutalisikia masikioni wala kuliona machoni mwetu. Tabasamu za huba, mapenzi na bashasha kwa mke, watoto, ndugu, jamaa na marafiki halitaonekana na kuambukiza tabasamu zetu. Limekwisha. Moyo wa nani utavumilia msiba huu? Kilio ni lazima.

Wafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara hawatasikia tena sauti hai nzito na ya kubana kama yenye mafua ikitoa nasaha na ushauri, kwa malengo ya kuwaongezea maarifa waweze kuboresha maisha yao. Vipi makundi haya yasiweke mikono vichwani na kubwaga vilio katika maeneo yao ya kazi?

Walemavu, mafukara na mayatima neema ya upendo, hisani na maliwazo kutoka kwa ndugu yao, baba yao na mlezi wao imekatika ghafla. Kifo badala ya neema kaleta mauti. Mauti kwao kama shetani, wanaogopa. Kipi kitawazuia kusikitika na kulia kipenzi chao hakipo. Si kufuru bali ni huzuni na kilio.

Waandishi wa habari, wasanii na wanamichezo wamebanwa pumzi, wanahemea juu juu, kwani ushauri umerudi kwao. Misaada na ajira ni kama vimeota mbawa. Kwa nini wasilie na kuomboleza? Viongozi wa serikali, siasa, taasisi za dini, jumuiya za kitaifa na mataifa kadhalika wanalia. Ni msiba mkubwa kwao.

Mawazo, fikra na falsafa za marehemu Reginald Mengi hazina budi kuenziwa na watu wote wapenda haki na wachukiao umaskini. Tumkumbuke katika mapambano yake dhidi ya umaskini. Amewahi kusema: “Ndoto yangu ni kushirikiana na serikali kutokomeza kabisa umaskini Tanzania.”

Ndoto bado kuaguliwa lakini mapambano dhidi ya umaskini yaendelee. Dk. Mengi amefanya mengi mazuri na machache mabaya kwa sababu binadamu si mkamilifu. Tumsamehe kwa hayo machache na tumuenzi kwa mengi mazuri. Mwenyezi Mungu ndiye muweza na mkamilifu.

Nafsi yake karimu yenye imani ya kiroho ndiyo iliyompa uthubutu kutenda haya tunayoyazungumza na kuyakumbuka. Tukiwa katika maombolezo, hebu tugangamale kushika na kusoma kitabu alichokitunga, kiitwacho: ‘I CAN, I WILL, I MUST.’  Soma tumuenzi kwa kauli na vitendo.

Nakumbuka kauli yake iliyojaa hekima na busara, utu, upendo na hisani aliyoitoa Januari 7, mwaka 2019 akisema: “Naomba nichukue fursa hii kuwaomba Watanzania wenzangu kuufanya mwaka 2019 kuwa mwaka wa maridhiano na kusameheana. Chuki ni mzigo mno kuubeba mioyoni mwetu, njia pekee ya kusonga mbele ni kusameheana na kudumisha upendo.”

Dk. Reginald Abraham Mengi kalale mahali pema peponi. Amin!