Salamu ndugu zangu wote mliopata baraka ya kuishuhudia Pasaka. Sina hakika, lakini ni kweli kwamba wengi walipenda kufurahia ufufuko wake Yesu Kristo mwaka huu lakini haikuwa hivyo.

Wapo ambao waliweka malengo ya miezi sita na mwaka, lakini mipango yao haikuwa na mkataba wa maisha au siha njema na mipango hiyo imevurugika. Vilevile nawatakia mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhani wote waliojaliwa kufunga.

Ninapofikiria mambo haya huwa ninakosa amani sana, na kuna wakati huwa nahisi kukata tamaa kabisa ya maisha, nawaangalia watoto nahisi niliwazaa ili niwaache kuwa yatima, machozi huwa yanagonga kope lakini ukweli unabaki palepale kwamba uzao wako ni lazima utaonja machungu ya uyatima japo hatujui ni lini, wapi na wakiwa na umri gani.

Kwa maana hiyo katika matayarisho yoyote yale ya mtu mwenye familia ni lazima azingatie kwamba watoto wake ni mali ya jamii, hautaishi nao milele, bali walimwengu wataishi nao. Ni vema kujua urithi pekee wa kuwaachia ni namna ya kuishi na watu wa ulimwengu huu na si vinginevyo, hapo ndipo ninapokumbuka mambo mengi ya malezi yetu sisi tukiwa wadogo na malezi ya sasa yanayoitwa ya kisasa.

Katika hili naona jinsi ambavyo maadili yamemomonyoka upesi sana kama theluji katika jua, ni katika kipindi kifupi mno ambacho maadili yamebadilika na kuifanya dunia kuwa mbaya miongoni mwa waadilifu na kuwa mbaya zaidi kwa hao wanaoita maadili mema ya kisasa yanayotakiwa kufuatwa, na ndiyo maana nikasema malipo ni hapahapa duniani.

Najua kuwa maendeleo huja na mambo yake, lakini hakuna maendeleo bora yanayokinza utamaduni wa mahali au eneo fulani. Maendeleo ya Tanzania ni pamoja na kutunza utamaduni wetu na kuuthamini. Utakuwa upumbavu na ujuha kama tutasema tuna maendeleo lakini tukiwa tumebomoa utamaduni wetu ambao kimsingi ulijengwa na wazee wetu kwa mustakabali wa maisha ya ukwetu.

Kila nikiamka najikuta nakumbana na maendeleo mapya ya kisasa ambayo kwangu huwa ni kero sana. Kwanza ninakiangalia kizazi hiki kwa jicho la huruma kwa jinsi ambavyo kimevaa uhusika wa watu wazima wakati bado wadogo.

Nawaona kaka zao ambao wamevaa uhusika wa utoto wakati umri wao na watendayo ni tofauti kabisa.

Hii dhana ninayotaka kuizungumzia leo naona kama nitagombana  na wote waliowaumini wa maendeleo ya mparaganyiko. Naomba mniwie radhi kwa kusema haya, kuna dhana ya usawa katika umri na jinsia, nakubaliana ni maendeleo lakini sina hakika kama inachukuliwa kwa jinsi ambavyo wenzetu waliichukulia na walimaanisha.

Mtoto mdogo ana haki zote za msingi katika malezi yake, mtoto anajifunza vitu vipya kila siku katika dunia iliyo wazi, tofauti na sisi ambao tuliishi katika dunia iliyofumbwa na ikafumbwa zaidi na wazazi wetu, lakini leo kwa mujibu wa takwimu za maendeleo ni pamoja na kumwacha mtoto ajifunze yote kutoka nje na ndani, ni pamoja na kumwacha na uhuru wake unaotambulika katika ibara za kimataifa kama uhuru wa mtoto na ndiyo maana tunaona tabia mbaya za watoto ambazo nina uhakika kwamba watawaachia watoto wao huku wakijuta.

Huwa naelewa mataifa ambayo yameamua kupiga marufuku aina fulani ya maisha, inawezekana wao hawaelewi kama tunavyoelewa sisi wasakatonge, kwa maana ya kuruhusu kila kitu halafu tunaanza kujilaumu wakati kumekwisha kuchwa.

Matatizo yote yanayojitokeza leo hii katika masuala ya nje ya utamaduni inaweza ikawa ni chachu ya kujiuliza maswali katika dhana ya maendeleo ya kweli. Kama tunadhani kuna uhuru na maendeleo katika kujiuza miili yetu bila kupigiwa kelele ndiyo maendeleo, basi nadhani kuna mahali tunafeli. Kama tunadhani kuna uhuru wa kupokea chochote kutoka nje na kukirithi kwa utamaduni wetu, basi nadhani kuna mahali tumepitiwa.

Inawezekana tukaleta maendeleo kwa kuiga maisha ya siasa za wenzetu lakini bila kupitia hatua ambazo wao walipitia, inawezekana tukaiga maendeleo ya ndoa za jinsia moja kwa hatua ambayo wao wamefikia lakini sisi hatujapitia hatua ngumu ambazo wao wamepitia mpaka kufikia hapo.

Inawezekana tukapata maendeleo kwa watoto kukosa adabu kwa watu wazima na kuwaona wazazi kama mizigo na kuwaacha katika vijumba vyao sanjali na wenzetu wanaojiita wameendelea wanaowaweka katika majumba maalumu ya wazee kama mizigo ya serikali, hapo naamini bado haukuwa utamaduni wetu na maendeleo hayo sitayakubali asilani.

Sasa yapo maendeleo mengine mengi ambayo nimeyaona na wewe umeyaona; uongo, unafiki, uigaji, wizi, rushwa, ngono, mawasiliano, kujitegemea, kujiuza, mitandao, usafiri, malezi, makazi, taarifa, majibizano, maziko, harusi, ngoma na mengine mengi, labda hayatakuuma sasa lakini mwishowe tutapata malipo hapahapa duniani.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

Please follow and like us:
Pin Share