Kutelekezwa ni pamoja na kunyimwa huduma za muhimu ambazo kama mke alistahili kupata. Huduma muhimu ni kama chakula, mavazi, makazi, matibabu, hela ya kujikimu kwa matumizi ya kawaida ya mwanamke, pamoja na kila hitaji ambalo kama mwanamke alitakiwa kulipata.
Ifahamike kuwa habari ya kutelekeza inawahusu wote mke na mume kwa maana ya kuwa mume anaweza kumtelekeza mke, hali kadhalika mke anaweza kumtelekeza mume. Hata hivyo, makala itazungumzia mume kumtelekeza mke ambapo sura ya 29, Sheria ya Ndoa iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 itarejewa.

1. Aina za kutelekeza    
(a) Aina ya kwanza ni kutelekeza ambako mume anaondoka kabisa ndani ya nyumba ambayo alikuwa akiishi na mke wake kama wanandoa na kwenda kuishi kwingine. Bila kujali huko alikoenda panajulikana ni wapi au hapajulikani suala la msingi ni kwamba hayupo katika makazi yake ya kawaida ya familia.
Aidha, ikiwa hayupo nyumbani lakini kwa sababu za msingi na za kisheria huko siyo kutelekeza. Sababu hizo ni kama kuwa jela, kuwa hospitali, kuwa amehamishiwa sehemu nyingine kwa sababu ya matibabu kwa mfano wengine huhamishiwa mikoani, na pia kuwa vitani labda baadaye mkapoteza mawasiliano na mazingira mengine ya dharura za kibinadamu na ambayo siyo ya makusudi, hayawezi kuitwa kutelekeza.
(b) Aina nyingine ya kutelekeza ni hatua ya kuwa mume na mke wanaishi wote katika nyumba moja au chini ya paa moja, lakini mume huyo hajishughulishi na kutoa matumizi au matunzo kwa mke huyo kwa namna yoyote ile.
Hajui anakula nini, hajui anavaa nini, hajui anapata vipi matibabu, kwa ufupi hajui lolote zaidi ya kumuona tu kama binadamu wengine ambao anawaona mitaani na hana uhusiano nao.
Pia kuishi chini ya paa moja lakini vyumba tofauti nako ni kutelekeza hata kama mke anapewa matumizi yote yanayostahili. Zaidi, hata kulala chumba kimoja lakini vitanda tofauti kwa muda mrefu tena kwa makusudi kwa sababu ya mgogoro wowote, nako ni kutelekeza.
Lakini pia kulala kitanda kimoja bila kushiriki tendo la ndoa kwa makusudi kwa muda mrefu bila sababu za msingi za kiafya au vinginevyo, nako ni kutelekeza.

2. Nini afanye aliyetelekezwa
Kifungu cha 115(1)(b) cha Sheria ya Ndoa kinasema kuwa Mahakama inayo mamlaka ya kumwagiza au kumwamrisha mwanaume kutoa matunzo au matumizi kwa mke wake. Kwa hiyo, kumbe huna haja ya kulalama na kulia na hali tayari sheria inaweza kukusaidia katika hili.
Unachotakiwa kufanya ni kwenda mahakamani na kufungua malalamiko ambapo mume huyo ataitwa na atatakiwa kujibu kwanini hatoi matunzo na hapo baada ya taratibu za kimahakama uamuzi utatolewa.  
Kifungu cha 76 cha Sheria ya Ndoa kinazitaja mahakama ambazo unaweza kutumia katika kufungua malalamiko. Ipo Mahakama ya Mwanzo, ya Wilaya, ya Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu.
Hata hivyo, unashauriwa kuanzia ustawi wa jamii ambako taratibu zake ni nyepesi na za muda mfupi. Ofisi za Ustawi wa jamii zipo kila makao makuu ya wilaya, ukifika utauliza na utaoneshwa.
Ikishindikana hapo, sasa unaweza kwenda mahakamani lakini pia unashauriwa kutumia Mahakama ya Mwanzo iliyo katika eneo lako au ya wilaya iliyo katika wilaya yako. Kwa kufanya hivi hakuna shaka habari ya kutelekezwa na kunyimwa matumizi itakuwa imepatiwa dawa sahihi.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.

By Jamhuri