Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Chato

SERIKALI imemkabidhi bendera ya taifa mwanariadha, Imelda Mfungo,ambaye ataiwakilisha nchi katika mashindano ya CRDB Marathon nchini Burundi.

Mwanariadha huyo ambaye amepata fursa ya kushiriki mashindano hayo ambayo yameandaliwa kwa mara ya kwanza na Benki ya CRDB Tanzania na kuzishirikisha nchi mbalimbali,anatarajia kuwa miongoni mwa washindani wa mbio hizo zitakazofanyika Agosti 10 mwaka huu.

Mkuu wa wilaya ya Chato,mkoani Geita, Louis Bura,akimkabidhi Bendera ya taifa Imelda Mfungo,mwanariadha pekee kutoka Tanzania anayeiwakilisha nchi katika mashindano ya CRDB Marathon nchini Burundi.

Akikabidhi bendera hiyo,Mkuu wa wilaya ya Chato mkoani Geita, Louis Bura, amesema serikali kwa kutambua umuhimu wa michezo imeamua kumkabidhi bendera ya taifa mwanariadha huyo ikiwa ni ishara ya kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo.

Amemtaka mwanariadha huyo kuiwakilisha vyema Tanzania katika mashindano hayo ili aweze kurejea na medali kwa kuwa ni jambo linalowezekana,huku akitumia fursa hiyo kuwataka vijana kupenda na kuthamini michezo kwa kuwa michezo ni ajira.

“Mwanariadha huyu anakwenda kuiwakilisha wilaya ya Chato,mkoa wa Geita na Taifa kwa ujumla na kwamba fursa hii inalenga kuifungua wilaya yetu katika michezo na utalii,hasa katika hifadhi zetu za taifa za Burigi-Chato na Kisiwa cha Rubondo” amesema Bura.

Kadhalika amewasisitiza vijana kote nchini kushiriki mashindano mbalimbali ya michezo ikiwemo riadha hatua itakayopunguza malalamiko ya ukosefu wa ajira hasa kwa vijana.

Ofisa michezo wa wilaya ya Chato, Mwl. Mataba Abel, ameishukuru serikali kutambua mchango wa mwanariadha huyo na kusisitiza kuwa michezo ni miongoni mwa mambo yanayoiletea heshima nchi kitaifa na kimataifa.

Aidha amesema serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwa wanamichezo wote nchini ikiwemo riadha ili kuwasadia vijana kutimiza ndoto zao badala ya vipaji vyao kupotea pasipo manufaa kwao na taifa kwa ujumla.

Akielezea kuhusu ushiriki wake,Imelda amewahakikishia watanzania kuwa anakwenda nchini Burundi kushiriki mashindano hayo na anaamini atarejea na medali kwa kuwa amejiandaa vizuri kiafya na kisaikolojia.

“Niwahakikishie watanzania kuwa sitawaangusha,heshima niliyopewa na nchi yangu ni kubwa sana niwahakikishie nitarejea nchini nikiwa na medali,nimejiandaa vyema na nipo tayari kwa mashindano na Mungu anisaidie” amesema Imelda.

Mwanariadha huyo ni tunda la kuanzishwa kwa Chato utalii Festival(2023), ambapo baada ya ushiriki wake ameendelea kushiriki mashindano mbalimbali ndani ya nchi.

                
Please follow and like us:
Pin Share