Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Serikali ya Mtaa Kivule, Amos Habgaya ameshauri Serikali uweke mkakati maalum kwa ajili ya kujenga miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam kwani bila kufanya hivyo changamoto za barabara kumalizika itakuwa ngumu.

Amesema lifanyike hilo kwa kuangalia uhalisia, wingi wa watu na uhitaji mkubwa uliopo kwani bajeti inayotengwa haitoshelezi.

Alizungumza hayo mwishoni mwa wiki baada ya kuona hali mbaya ya barabara za Ukonga na utatuzi wake hautamaliza changamoto zilizopo katika barabara nyingi ambazo hazijaingizwa kwenye mfumo.

“Kwa bajeti iliyopo upande wa miundombinu itatuchukua miaka mingi sana kulifanya Jimbo la Ukonga lenye watu 900000 lifanane na majimbo mengine.

“Nashauri hili Jiji liwekwe kwenye mkakati maalum, bajeti inayotengwa kwa ajili ya wilaya haitoshi , mfano Mtaa wa Kivule una watu takribani 25000, Kata nzima Ina watu zaidi ya 80000 na barabara zenye urefu wa kilometa 40 mpaka zaidi ya 50.

“Kwa bajeti ya kujenga barabar tatu, kujenga barabara zilizopo hadi zifanane na zingine itakuwa ngumu, barabara nyingi bado hazijasajiliwa ili kuingizwa kwenye mfumo kwani sensa ya kuzisajili haijafanyika kwa muda mrefu.

“Serikali ikfanikiwa kuweka mkakati maalum wa kimiundombinu na kulipendezesha Jiji la Dar es Salaam, malalamiko kwa wananchi yataisha,”alisema Hangaya.

Hangaya anashauri awepo Katibu Mkuu maalum kwa ajili ya kushuulikia miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam au wizara maalum ili kuangalia changamoto hizo katika majimbo yote, zitatuliwe, wakazi wa Dar es Salaam waondokane na adha wanayokutana nayo wakati wa mvua na wakati wa jua pia kutokana na ubovu barabara.

By Jamhuri