Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wiki iliyopita nchi yetu ilipata mshituko. Si mshituko mdogo, bali wenye kishindo. Katika kipindi ambacho Rais Samia Suluhu Hassan anaponya vidonda vikubwa vilivyotokana na utawala wa Awamu ya Tano, ambapo Tanzania iliingia katika historia ya watu kupotezwa na watu wasiojulikana, sasa ni bayana mauaji yamerejea tena nchini.

Sitanii, zilianza taarifa za watoto kutekwa. Wimbi likapita. Zikaja taarifa za watu 84 kupotezwa, na kwa kweli sisi Gazeti la JAMHURI tumeandika mara kadhaa juu ya watu wanaotekwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo Geita, ikaonekana serikali imeingia kazini, kasi ikapungua. Wakati vumbi halijatuama sawa sawa, akatekwa na kuuawa Mohamed Ali Kibao, kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kinachosikitisha na kuogofya ni jinsi Kibao alivyotekwa. Kwanza, alikuwa kwenye basi. Basi lilikuwa na abiria wengine. Akashushwa Kibo, Tegeta jijini Dar es Salaam, akapelekwa kusikojulikana. Hii ilikuwa Septemba 6, 2024. Siku mbili baadaye, yaani Septemba 8, 2024 mwili wa Kibao ukaokotwa eneo la Ununio, Dar es Salaam.

Uchunguzi wa madaktari umethibitisha kuwa Kibao alipigwa, akamwagiwa tindikali, na mwili wake ukaharibiwa. Zipo dhana nyingi, kwamba waliohusika na utekaji huu ni polisi, kwani wahusika waliingia kwenye basi wakiwa wamebeba bunduki ya Sub Machine Gun (SMG). Taarifa nyingine zinazopeperushwa kwenye mitandao zinasema CHADEMA wanatekana wenyewe kutafuta huruma ya kisiasa.

Sitanii, taarifa nyingine zinasema mahasimu wa kisiasa wa Rais Samia wanateka watu, watoto na kufanya maovu yote yawayo kuonyesha jamii kuwa ameshindwa kusimamia usalama wa raia na mali zao, hivyo asipewe nafasi ya kugombea urais mwaka 2025.

Kwa vyovyote iwavyo, kila ncha ya sababu inayoelezwa polisi bado wanaguswa. Kwamba CHADEMA wanatekana wenyewe, hili mbali na kutoingia akilini, bado ni wajibu wa polisi wakifahamu kuna kundi la wahalifu wa aina hii, walipaswa kuchunguza, kukamata na kuwafikisha mbele ya vyombo vya dola. Usalama wa raia hauna itikadi, dini, jinsi wala kabila. Ni kazi ya polisi kuzuia uhalifu, hivyo kama wahalifu wapo kwenye vyama vya siasa inabidi wakamatwe mara moja na wafikishwe mahakamani.

Hili jingine kwamba wagombea urais wanamtafuta Rais Samia, nalo jibu lake ni sawa na hilo la wahalifu kuwa ndani ya CHADEMA. Kama kuna mgombea urais mtarajiwa anayefanya uharamia wa aina hii kuondoa maisha ya wananchi kabla hajachaguliwa, akichaguliwa si atatuchoma mishikaki? Kama lipo kundi hili, nalo linapaswa kuchukuliwa hatua haraka na kufikishwa mahakamani.

Sitanii, zipo taarifa kuwa Kibao alikuwa askari mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), na alipigana Vita ya Kagera, hivyo wapo wanaosema kuwa kwa wadhifa aliofikia katika utumishi alikuwa na kiapo, alipaswa kutunza siri za nchi.

Kwangu mimi ukiniuliza naona hili nalo si sababu ya kumuua mtu. Hivi kama mtu akishakuwa askari haruhusiwi kufanya siasa? Kama hivyo ndivyo, basi nchi kama Marekani au Uingereza ambako chama tawala kikishindwa kurejea madarakani utawala wa wapinzani unaengua maafisa wa juu wote wa polisi na vyombo vingine vyote vya dola, nao wangeuana kama kuku maana siri za nchi wanaondoka nazo – hadi nywila (password) za nyuklia!

Maana, mfano alipoingia madarakani Donald Trump, aliengua kuanzia mkuu wa majeshi na vyombo vingine vyote unavyovifahamu. Kingine kinachonipa shida, ikiwa vyombo vya dola ndivyo vimemteka na kumuua Kibao, najiuliza kweli vyombo vya dola vinaweza kufanya uzembe mkubwa kiasi hiki kumshusha mtu kwenye basi lenye watu kweupe na kwenda kumuua?

Kama ni kundi la majambazi, najiuliza hawa majambazi walikuwa wanataka nini kwa Kibao maana hadi kubeba SMG, labda kama angekuwa na fuko la dola za Marekani, maana majambazi hutafuta fedha, si roho za watu.

Maswali haya na mengine yananirejesha katika jibu moja la msingi: Katika nchi yetu, yupo mwanasiasa aliyekabidhiwa dhamana ya kulinda usalama wetu na huyu si mwingine, ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Masauni Yusufu Masauni.

Sitanii, kabla sijakumbusha mambo ya mbali nigusie yaliyotokea miaka 11 tu iliyopita. Sote tulikuwapo. Mwaka 2013 katika kukabili ujangili, ilianzishwa Operesheni Tokomeza. Operesheni hii ilidhibiti ujangili, lakini pia maisha ya watu yalipotea. Mawaziri wanne waliwajibika kisiasa. Pamoja na kwamba hawakuwa porini kupambana na majangili waliwajibika. Mawaziri waliowajibika ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki; Waziri wa Ulinzi, Shamsi Vuai Nahodha; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi; na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Mathayo David.

Sitanii, mwaka 1975 na 1976, yalitokea mauaji ya vikongwe katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Rais wa Tanzania wakati huo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliunda Tume ya kuchunguza mauaji hayo. Ile alipounda Tume tu, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ali Hassan Mwinyi, hakusubiri matokeo ya uchunguzi, bali Januari 22, 1977, aliandika barua ifuatayo:-

Mheshimiwa Mwalimu J. K. Nyerere,

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Ikulu,

DAR ES SALAAM

Mwalimu,

KUJIUZULU

Hivi karibuni, kiasi cha miaka miwili iliyopita palizuka vikundi fulani vya mauaji katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Idadi kubwa ya wananchi wakiuliwa ovyo kila mwezi kwa visingizio vya uchawi na vinginevyo. Serikali ililazimika kuyamaliza maovu hayo kwa nia njema ya kuzuia hali hiyo isiendelee na pia kuwajua wahalifu hao ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

Katika kutekeleza nia nzuri ya serikali, vyombo vinavyohusika na utekelezaji, polisi ikiwamo, vilivuka mipaka ya wajibu wao na vikajipa madaraka ya kuogelea katika vitendo viovu vya kishenzi, kimyama na kikatili hata baadhi ya watu waliokamatwa kwa kushukiwa tu kwamba wanahusika wakafa na wengine wakapata vilema vya kudumu.

Polisi ni chombo cha kulinda amani, mali na maisha ya watu wake, si chombo cha kuwaua. Pia polisi ni chombo cha kuhifadhi na kudumisha usalama na haki; si chombo cha kudhulumu, kuonea na kuwatesa makusudi wananchi wake wale wale wanaokigharimia kukiweka. Kwa bahati mbaya maovu kama haya ndiyo hasa yaliyotendwa na vyombo vya serikali huko Mwanza na Shinyanga.

Kijinai, mimi binafsi nisingehusika kwani sikushiriki wala kushauri, sikuagiza wala kuelekeza kwamba mambo yafanywe kama hivyo yalivyofanywa. Kwa kweli hata mimi nilifichwa kwani niliarifiwa baada ya Tume yako kuteuliwa.

Hata hivyo, kisiasa nakiri kuwa nahusika siwezi kukwepa kwa sababu dhamana yangu ya uwaziri inaambatana na wajibu unaonitaka nijue yanayotendeka wizarani na pia niweze kudhibiti na kuhakikisha mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi.

Msahafu unatuusia kwa kusema: “Wala hatabeba mbebaji mzigo wa (mtu) mwingine.” Kisiasa mzigo huu ni wangu na nakubali kuubeba kwani hakuna mwingine wa kuubeba.

Kwa hiyo, Mwalimu nakuomba mambo matatu. Kwanza naomba radhi mimi nafsi yangu na pia naomba radhi kwa niaba ya askari wote walio wema. Pili, naomba vilevile uelewe sehemu yangu katika kosa hili. Tatu, kwa fedhea hili, naomba unikubalie kujiuzulu.

Wako mtiifu,

H. Mwinyi (Mbunge)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Mzee Mwinyi alipojiuzulu, alifungua mlango wa uwajibikaji, ambako mamlaka ya uteuzi iliwastaafisha kwa maslahi ya umma, Mkuu wa Usalama wa Taifa Mkoa (RSO) Andrew Mayalla, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Peter Kisumo; Mkuu wa Usalama wa Taifa Wilaya (DSO) Ihuya, Mkuu wa Polisi Mkoa (RPC) Mkwawa, na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD). Hawa baada ya kustaafishwa walifikishwa mahakamani na baadhi wakakutwa na hatia, wengine wakaachiwa huru.

Sitanii, kwa kazi hii nimepata fursa ya kuzungumza na baadhi ya mawaziri, baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mabalozi wetu nje ya nchi na wastaafu kadhaa. Kama vile wameambizana. Mawazo yao ni Masauni ajiuzulu! Wanarejea matukio ya utekaji watoto, watu kupotea na hili la Kibao limetia mafuta katika moto unaowaka tayari.

Mimi nafanya uchambuzi wa mitazamo na kinachoendelea kwenye jamii yetu. Baada ya kuifanya kazi ya uandishi kwa miongo mitatu sasa, nadiriki kusema kwa uhakika kuwa naweza kutabiri tunakoeleka kama Masauni hatajiuzulu. Baadhi ya watu wameanza lugha za kujiandaa kukataa kukamatwa na polisi. Wanashauri mtu akikamatwa watu wachangishane fedha wakodi bodaboda na kufuatilia gari la polisi hadi litakapoishia. Wanatumia maneno kuwa “wawajazie nzi!”

Mawazo haya ukiyasikia, unafahamu kuwa watu wanakwenda kukata tamaa. Watu wakikata tamaa huacha kutii sheria. Wakiacha kutii sheria, taa itazimika. Nakiri, binafsi sina ugomvi wowote na Masauni. Kupitia tamko la Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), nimemwomba Rais Samia aunde Tume ya Kijaji kama ilivyoundwa mwaka 1976 na mwaka 2013. Tume hii ichunguze kila kiwacho na kwa uwazi.

Hii itakuwa sehemu ya kutekeleza 4R. Falsafa ya Rais Samia ya Maridhiano (Reconciliation), Ustahimilivu (Resiliency), Mabadiliko (Reforms), na Kujenga Upya (Rebuilding) ilianza kuonekana inafanya kazi. Wafuasi wa vyama vya upinzani walirejeshewa haki ya kufanya mikutano ya hadhara. Watanzania tulianza kuzungumza bila hofu, ila mauaji ya Kibao yameturudisha nyuma.

Sitanii, tusiposema leo, mawe yatasema. Leo kama kuna mtu anayefurahia kifo cha Kibao, anapaswa kufahamu kuwa Kibao ametangulia na sisi tuko nyuma yake. Tuweni watu wenye huruma kwa mioyo ya binadamu wenzetu. Kuua ni jambo baya mno. Nirejee nukuu iliyopo katika makaburi ya Pungu jijini Dar es Salaam: “Mlivyo ninyi, ndivyo tulivyokuwa sisi. Tulivyo sisi, ndivyo mtakavyokuwa ninyi.”

Rais Samia ameelekeza ufanyike uchunguzi wa mauaji ya Kibao na mengine ya aina hiyo na kupatiwa taarifa haraka. Amesema Tanzania ni nchi ya kidemokrasi na hakuna anayepaswa kuuawa.

Nimalizie kwa nukuu ya maneno ya Mzee Mwinyi: “Hata hivyo, kisiasa nakiri kuwa nahusika siwezi kukwepa kwa sababu dhamana yangu ya uwaziri inaambatana na wajibu unaonitaka nijue yanayotendeka wizarani na pia niweze kudhibiti na kuhakikisha mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi. Msahafu unatuusia kwa kusema: “wala hatabeba mbebaji mzigo wa (mtu) mwingine.” Kisiasa mzigo huu ni wangu na nakubali kuubeba kwani hakuna mwingine wa kuubeba.”

Sitanii, Mwinyi alijiuzulu akamsaidia Nyerere, Masauni amsaidie Rais Samia, amani irejee nchini. Kuna maisha baada ya uwaziri. Mwinyi baadaye alipanda akawa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na baadaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dk. Nchimbi amepanda sasa ni Katibu Mkuu wa CCM. Masauni usisubiri kufukuzwa baada ya uchuguzi kukamilika. Mungu ibariki Tanzania.

078440482

Please follow and like us:
Pin Share