Na Tatu Saad

Dakika 45 za kipindi cha kwanza ndizo dakika pekee zilizomtosha Stephan Azizi Ki katika mchezo wa jana wa  kombe la shirikisho barani Afrika, Yanga dhidi ya Real  Bamako ya Mali, baada ya kocha mkuu wa Klabu ya Yanga Nasreddine Nabi kuamua kumtoa mchezaji huyo mara tu baada ya kipindi cha kwanza.

Nabi ameyatetea maamuzi yake hayo kutokana na baadhi ya mashabiki na wapenzi wa soka kumlalamikia maamuzi yake, amesema mfumo ndio uliyomlazimu yeye kufanya maamuzi hayo.

Nabi amesema mfumo aliyoutumia kipindi cha kwanza sio sawa na mfumo aliyoutumia kipindi cha pili hivyo ilimlazimu kumtoa mshambuliaji huyo kutoka Burkina Faso na kumuingiza mchezaji mwingine anayecheza mfumo huo.

“Wote tunakubaliana na ubora wa Aziz, ni mchezaji mzuri, lakini unaweza kuwa mchezaji mzuri ila usipofuata mfumo timu inavyocheza unakuwa unaonekana sio bora” amesema Nabi

Nabi amesisitiza kuwa kwake linapokuja suala la mfumo, hana budi kumtumia mchezaji mwingine kwa maslahi ya timu.

“Hakuna asiyefahamu uwezo wa Azizi Ki, lakini linapokuja suala la mfumo sina budi kumtumia mchezaji mwingine kwa maslahi ya Yanga Sc”.Amesema Nabi.

Katika mchezo huo Yanga walikuwa wenyeji wa Real Bamako ndani ya dimba la Benjamin Mkapa, ukiwa ni mchezo wa mzunguko wanne wa kundi D, kombe la shirikisho Barani Afrika na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Ushindi ambao umeendelea kuwaweka Yanga katika nafasi ya pili wakiwa na alama saba, wakiongozwa na US Monastir ya Tunisia yenye Alama 12 huku Tp Mazembe Ukishuka nafasi ya tatu na alama tatu na Real Bamako wakiburuza mkia wakiwa na alama 2.

By Jamhuri