Na Tatu Saad, JAMHURI MEDIA

Wana Manungu kutoka mkoani Morogoro, ‘Mtibwa Sugar’ wameeleza kuzitaka alama tatu muhimu kwa kulipa kisasi, katika uwanja wa nyumbani dhidi ya Simba Sc, mchezo utakaopigwa Jumamosi ya Machi 11 mwaka huu katika uwanja wa Manungu huko Morogoro.

Akizungumza kuhusu maandalizi yao mkuu wa idara ya Habari na mawasiliano wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru amesema wachezaji wao wamefanya mazoezi ya kutosha na wapo tayari kuwakabili Simba Sc vyema kabisa.

Mtibwa sugar inawakaribisha Simba Sc katika dimba la Manungu wakiwa na dhamira kubwa ya kupata ushindi wa alama tatu katika mchezo huo ili kuweza kujihakikishia wanaendelea kukaa sehemu nzuri katika ligi kuu ya Tanzania Bara.

Hata hivyo Kifaru amesema kuwa alama tatu wanazoenda kuzichukua kwa Simba sc ni sehemu ya kisasi chao juu ya kichapo walichokipata katika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ambapo Simba Sc waliwacharaza Mtibwa mabao 5-0 katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

“Mbali na kuzihitaji alama tatu za mchezo huo wa Jumamosi, pia dhamira yetu nyingine ni kulipa kisasi dhidi ya wageni wetu, unakumbuka Simba SC ilitufunga mabao matano pale Dar es salaam, kwa hiyo na sisi tutahitaji kuwanyong’onyesha.” amesema Kifaru.

Pia Kifaru amesema mchezo huo sio rahisi kwani Simba Sc wana wachezaji wazuri ambao wanaweza kupata ushindi nyumbani na ugenini lakini Jumamosi hii hawatatoka katikati ya shamba la miwa huko Manungu.

“Tunafahamu Simba SC ina wachezaji wazuri wenye uwezo mkubwa wa kupambana katika michezo ya nyumbani na ugenini, lakini hata sisi tuna wachezaji wa kaliba hiyo, hivyo tunawakaribisha katikati ya mashamba ya miwa ili tuoneshane kazi.”Amesema Kifaru.

Simba wameondoka leo mchana jijini Dar es Salaam kuelekea Morogoro tayari kwaajili ya mchezo huo wa Jumamosi dhidi ya Mtibwa sugar katika dimba la Manungu, Tuliani, mchezo utakaochezwa majira ya saa 10 jioni.

Mchezo wa mwisho kwa Mtibwa sugar walipoteza kwa idadi ya mabao 2-0, dhidi ya Singida Big Stars katika uwanja wa CCM Liti huko Singida, huku Simba Sc mchezo wao wa mwisho ni mchezo wa kimataifa wa kombe la klabu bingwa Afrika na kuibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Vipers ya Uganda.

Simba SC anashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ya Tanzania bara ikiwa na alama 54, ikitanguliwa na Yanga Sc yenye alama 62 huku Mtibwa sugar ikishika nafasi ya tisa ikiwa na alama 29.

By Jamhuri