Iringa. Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa, Dady Igogo ameandika barua ya kujiuzulu wadhifa wake wa Naibu meya .

Kwamujibu wa barua yake ya Februari 13 aliyoiwasilisha kwa Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Alex Kimbe, Igogo amedai ameamua kujiuzulu wadhifa huo na kwamba atabakia na wadhifa wake wa udiwani.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Omary Mkangama amethibitisha kupokea nakala ya barua  ya kujiuzulu kwa naibu meya  na kwamba hajatoa sababu za kujiuzulu wadhifa huo.

“Nikweli taarifa hizo ni za kweli, nimepata nakala ya Naibu Meya kujiuzulu wadhifa huo na kubaki diwani kata ya Gangilonga lakini hajatoa sababu za uamuzi wake” amesema Mkangama.

Jitihada za kutafuta Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Alex Kimbe kuzunguzia taarifa hizo hazikuzaa matunda baada ya simu yake kuita bila kupokelewa.

Pia Igogo naye simu yake imeita bila kupokelewa.

Igogo amejiuzulu nafasi hiyo ya Naibu Meya wakati ambapo waliokuwa madiwani wa Halmashauri hiyo wapatao Tisa wakiwa wamejiuzulu nyazifa zao na kujiunga na CCM.

Kati ya Madiwani waliojiuzulu nyazifa zao ni sita kutoka katika kata na watatu viti maalum.

Kata ambazo waliojiuzulu ni Kata ya Kitwiru ambayo katika Uchaguzi mdogo  uliofanyika Novemba 26 aliyekuwa diwani wa kata hiyo Baraka Kimata alifanikiwa kutetea kitu chake safari hii akipeperusha bendera  ya CCM.

Kata nyingine ni Kihesa ambao Uchaguzi uliofanyika Januari 13  ambao Juli Sawani CCM ilipita bila kupingwa baada ya vyama Vya upinzani kususia Uchaguzi.

Kata nyingine ambazo ziko wazo hadi sasa ni Kwakilosa, iliyokuwa ikishikiliwa na Joseph Ryata aliyekuwa Naibu Meya, kata ya Mkwawa iliyokuwa ikiongozwa na Osca Kafuka, Mwangata Angelus Mbogo na Ruaha Gabriel Ndes.

By Jamhuri