Na Mwandishi Wetu , JamhuriMedia, Arusha

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko amesema kama Serikali haitafanya Tathmini ya Shughuli zake haitakuwa na uwezo wa kujipima na vihatarishi vya utekelezaji wa mipango yake. 

Naibu Waziri Mkuu Dkt. BITEKO ameyasema hayo mapema leo jijini Arusha alipofungua Kongamano la Pili la Kitaifa la Ufuatilijai, Tathmini na Mafunzo ambapo amesema Serikali imegawanyika katika maeneo mengi kama vile Serikali Kuu na Serikali za Mitaa hivyo ufuatiliaji na tathmini ni eneo muhimu na linalopaswa kutiliwa mkazo. Kutokana na umuhimu huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anasisistiza Serikali kuwa na Uratibu wa shughuli zake.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko akihutubia wakati alipofungua kongamano la pili la wiki ya kitaifa ya Ufutailiaji na Tathmini lililofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa AICC Jijini Arusha.

“Unaweza kukuta Serikali za Mitaa na Serikali kuu kila mtu anafanya jambo lake hakuna vinavyosomana, tujifanyie tathmini ili tusije kuwa watu wa kuduwaa kunini hili limetokeaje.” amesisitiza

Dkt.Biteko aliongeza kusema kuwa asiyejifanyia tathmini atakuwa ni mtu wa hasara hivyo kujifanyia tathmini kunaifanya serikali kubaini matatizo mapema na kuweza kuyatafutia ufumbuzi kabla hayajaleta hasara. Dkt. Biteko ametoa wito kwa washiiriki wa kongamano hilo hasa watendaji wa serikali kufanya ufuatiliaji na tathmini bila kuweka mbele rasilimali fedha.

Sambamba na hilo, Naibu Waziri Mkuu Dkt. BITEKO amewataka maafisa masuhuli wote nchini kuviwezesha vitengo vya ufuatiliaji na tathmini katika wizara na taasisi zao kwa kuhakikisha kunakuwa na wataalamu wa kutosha, vitendea kazi na rasilimali fedha ili viweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulika na masuala ya (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama amesema, wakati kongamano hili likifanyika kwa mara ya Pili hapa nchini, Serikali imefanyia kazi kwa Asilimia mia, (100%) utekelezwaji wa agizo la uanzishwaji wa Idara za Ufuatilijaia na Tathmini katika Wizara na Serikali.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko akimkabidhi tuzo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati wa Kongamano la pili la Wiki ya Kitaifa ya Ufutailiaji na Tathmini lililofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa AICC Jijini Arusha.

Awali akiongea wakati wa Ufunguzi wa Kongamano hilo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi, alisema kwa kufuatilia mwendeno wa utekelezaji wa kujipima matokeo, Taasisi za Umma zinaweza kujihakikishia kuwa zipo katika njia sahihi za utekelezaji katika kufikia malengo yake, hivyo Ufuatiliaji na Tathmini ni njia nzuri ya kujifunza na kuwajibika.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama akitoa salamu wakati wa Kongamano la pili la Wiki ya Kitaifa ya Ufutailiaji na Tathmini lililofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa AICC Jijini Arusha.

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko alipotembelea Banda la Idara ya Menejimenti ya Maaafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu wakati Kongamano la pili la Wiki ya Kitaifa ya Ufutailiaji na Tathmini lililofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa AICC Jijini Arusha.
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko akiwa na Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu baada ya kuhutubia  Kongamano la pili la Wiki ya Kitaifa ya Ufutailiaji na Tathmini lililofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa AICC Jijini Arusha.

By Jamhuri