NATO: Chombo cha Marekani, kutekeleza sera zake duniani

Na Nizar K Visram

NATO ni muungano wa kijeshi wa mataifa ya Ulaya na Marekani ulioundwa kwa madhumuni ya kulindana iwapo taifa moja litashambuliwa kutoka nje. Uliasisiwa chini ya mkataba wa Washington uliosainiwa na mataifa 12 Aprili 1949.

Mataifa yenyewe ni Ubelgiji, Canada, Ufaransa, Iceland, Italy, Luxembourg, Uholanzi, Norway na Ureno.

Kifungu cha tano cha mkataba huo kinasema iwapo nchi moja itashambuliwa, hiyo ni sawa na kuzishambulia nchi zote za NATO. Wakati huo nchi za Magharibi zilihisi kuwa kuna uwezekano wa kushambuliwa na Umoja wa Kisovieti (USSR). 

Ndipo NATO ikaunda jeshi la pamoja likiongozwa na Marekani. Kamanda akawa Jenerali Eisenhower ambaye baadaye akaja kuwa Rais wa Marekani.  

Baada ya Vita Kuu ya Pili kumalizika Marekani ikawa inatoa misaada kwa nchi za Ulaya Magharibi (Marshall Plan). Baadaye mpango huu ukafutwa na badala yake Marekani ikaanzisha misaada ya kijeshi. 

Mwaka 1952 Ugiriki na Uturuki zikaingia NATO na mwaka 1955 Ujerumani Magharibi ikajiunga. 

Nchi za Ulaya Mashariki zikiongozwa na USSR nazo zikaamua kuunda muungano wao wa kijeshi uitwao Mkataba wa Warsaw (Warsaw Pact),  miaka sita baada ya kuundwa kwa NATO. 

Huo ndio mwanzo wa vita baridi baina ya nchi za NATO na Warsaw Pact. Uhasama huo haukuwapo wakati wa Vita Kuu, kwani Marekani, Uingereza na USSR zilishirikiana kupigana na Ujerumani na utawala wake wa kifashisti ulioongozwa na Adolf Hitler. 

Nchi hizi zilitofautiana kiitikadi lakini wote walikuwa wakikabiliwa na majeshi ya Hitler na ilibidi kukusanya nguvu zao ndipo wakamshinda. Katika vita hiyo USSR ilipoteza askari milioni 27.

Katika Vita Kuu, Marekani na Uingereza ziliikomboa Ulaya Magharibi na USSR ikaikomboa Ulaya Mashariki. Vita ikamalizika na uhasama ukarudi. Rais Harry Truman wa Marekani akatangaza kuwa nchi yake na washiriki wake wataendeleza mapambano dhidi ya USSR na ‘ukomunisti wa kimataifa’. 

Harakati hizi zikiongozwa na NATO ziliendeleza fikra kuwa USSR inataka kuzimeza nchi zote za Ulaya na kwingineko. Ukweli ni kuwa USSR isingeweza kufanya hivyo baada ya kupoteza watu milioni 27 katika Vita Kuu. Uchumi wake ulitikisika vibaya na ilibidi waujenge upya. 

Kwa upande wa pili, Marekani ikatumia bendera ya NATO kuweka kambi za kijeshi katika nchi za Ulaya Magharibi kama Ujerumani, Uingereza na Italia. Baadaye ikazichukua nchi za mashariki kwa kuchochea vita ya Yugoslavia.  

Leo hii NATO ina nchi wanachama 30. Karibu zote zina vituo vya kijeshi vya Marekani. Vituo vikubwa viko Ujerumani na Italia. Kila nchi inatakiwa ilipe gharama za vituo hivi. Yaani inalipa ili ikaliwe na majeshi ya kigeni.

Leo hii NATO ina wanajeshi milioni 3.5 Ulaya, wakiongozwa na makamanda wa Marekani. Wanajeshi kutoka Marekani ni 320,000. 

Majeshi ya NATO yanaongozwa kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Marekani (Pentagon). Makamanda wake wanateuliwa na Marekani. Chini ya sera ya ulinzi wa pamoja, nchi wanachama wa NATO wanafuata maagizo kutoka Marekani.  

Ndipo tunaona vituo vya kijeshi vya Marekani wimewekwa katika nchi za Ulaya Mashariki, Magharibi na Canada. Pia tunaona sera ya Marekani katika mambo ya nje ndiyo sera ya NATO. Ni pamoja na mkakati wa kuweka majeshi ya NATO kuizunguka Urusi. 

Marekani inaposhambulia nchi kwa kutumia bendera ya NATO, nchi wanachama nazo zinachangia kwa kutoa majeshi. Maana yake nchi za NATO zinapigana vita ya Marekani. 

Majeshi ya Marekani si tu yamewekwa katika nchi za NATO, bali hata nje ya NATO. Kuna nchi duniani ambazo zinashirikiana kijeshi na Marekani nazo ziko Afrika, Marekani Kusini, Mashariki ya Kati, Asia na visiwa vya Oceania. Ni pamoja na Israel ambayo inapewa hadhi sawa na nchi za NATO.

Kwa ujumla Marekani ina vituo zaidi ya 800 katika nchi zisizopungua 80 duniani. Barani Afrika ina vituo 29 katika nchi 15. Ujerumani inaongoza kwa kuwa na vituo takriban 39 vya Marekani. Hata anga za juu hawakuziacha. Huko nako Marekani inaweka majeshi yake. Siku zijazo huenda sayari zikawa makoloni ya Marekani!   

Baada ya kusambaratika kwa USSR na kuvunjika kwa Warsaw Pact, NATO haikuwa na mantiki ya kuendelea kuwapo kwa sababu lile ‘jinamizi’ halikuwapo tena. Hata hivyo, NATO si tu iliendelea kuwapo bali ilipanuka na kuzidi kujitutumua. 

NATO ikapanua mipaka yake na nchi za Warsaw zikawa wanachama. Yugoslavia ikavunjika na mwaka 1995 NATO ikatuma wanajeshi 60,000 huko Bosnia. Mwaka 1999 ikaporomosha jumla ya makombora 38,000 katika Serbia. Mwaka 2001 Marekani ikatumia bendera ya NATO kuishambulia Afghanistan. Mwaka 2011 ikaishambulia Libya na kumuua Gaddafi.

Marekani ikawa inachangia bajeti ya NATO kwa asilimia 22 hadi 25. NATO ikawa chombo cha Marekani katika kutekeleza sera zake duniani. Ripoti ya siri kutoka Pentagon ilitayarishwa na Paul D. Wolfowitz aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekanim ikavujishwa.

Ripoti hii imeionya nchi yoyote inayothubutu hata kujaribu tu kuchukua nafasi ya Marekani kisiasa na kijeshi duniani. Yaani Marekani ndiyo nchi pekee itakayotawala sayari hii. 

Ripoti inasema lengo kuu la Marekani ni kuzuia taifa lolote lisijitokeze na kuchukua nafasi yake. Ndiyo maana ni muhimu sana kuitunza NATO kama chombo cha ulinzi wa Magharibi.  

“Wakati huohuo ni lazima Marekani izuie Ulaya isijitoe kutoka NATO na kuunda chombo chake cha ulinzi bila ya kutegemea Marekani.”

Ndipo tunaona baada ya kuziteka nchi za Ulaya Mashariki, NATO ikidai kuwa ina wajibu wa kupambana na ugaidi duniani. Lakini wakati huohuo tumeona NATO ikiwatumia na kuwafunza wapiganaji waliofungamana na Al Qaeda katika Kosovo, Libya na kwingineko.

Nchini Syria, tangu Machi 2011 wapiganaji wa mujahidina walipewa mafunzo na silaha na NATO na Uturuki. Hii iliripotiwa na majasusi wa Israel waitwao Debka.

Vyombo vya habari navyo vikacharuka katika kuunga mkono NATO licha ya kujua fika kuwa hakuna nchi ya kigeni iliyotangaza vita dhidi ya Marekani. Hizo ndege hazikutoka Afghanistan wala si mali ya Afghanistan. Magaidi walioteka nyara ndege hizo si raia wa Afghanistan bali walikuwa raia wa Saudia. 

Licha ya kujua yote haya, Afghanistan ikashutumiwa kwa mashambulizi ya New York, kuwa ilikuwa inamlinda Osama bin Laden aliyepanga mashambulizi. Serikali ya Taliban nchini Afghanistan mara mbili iliwasiliana na Marekani na ikawa tayari kumkabidhi Osama kwa Marekani. Bush akasema yeye hazungumzi na magaidi. Vyombo vya habari vilificha habari hii.

Katika muda wa siku 28, Marekani na washirika wa NATO wakaishambulia Afghanistan. Wachambuzi wa kijeshi wanasema haiyumkiniki kukamilisha maandalizi ya vita katika siku 28. Ukweli ni kuwa mashambulizi ya Afghanistan yalipangwa hata kabla ya New York kushambuliwa. Habari hii nayo ikafichwa. 

[email protected]

+1 343 2048996