Miongoni mwa habari zilizopewa umuhimu katika toleo hili inahusu kuachiwa huru kwa mahabusu 201 waliokuwa katika magereza ya wilaya za Musoma, Tarime na Serengeti mkoani Mara.

Kuachiwa kwao ni matokeo ya ziara ya ukaguzi ndani ya magereza hayo uliofanywa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju; Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga na wadau wengine.

Wiki kadhaa zilizopita niliandika kuhusu mateso yanayowapata maelfu kwa maelfu ya mahabusu na wafungwa. Nikaomba rais, kwa mamlaka aliyonayo afanye kila linalowezekana ili kuwe na kikosi kazi cha wataalamu wa sheria kipite katika magereza yote kubaini watu waliobambikiwa kesi.

Nikiri kuwa sikujua kama upo utaratibu mzuri wa kisheria wa Ofisi ya DPP na Wizara ya Katiba na Sheria wa kushughulikia masuala haya.

Takwimu za Jeshi la Magereza zinaonyesha kuwa uwezo wa magereza yote nchini ni kuhifadhi wafungwa na mahabusu takriban 30,000 lakini hadi Aprili, mwaka huu kulikuwa na ongezeko la mahabusu na wafungwa takriban 9,000. Fikiria watu 9,000!!! Hii ni idadi kubwa mno.

Jambo la kutia faraja kwenye hoja hii ni kauli ya DPP baada ya kuamuru kuachiwa mahabusu 201 mkoani Mara – kwamba wapo ambao kesi zao zimekaa muda mrefu bila kusikilizwa. Wapo wenye viji-kesi vya kawaida kama vya mtu kukutwa akinywa gongo, au kesi za kutukanana! Kesi ya kutukana inamweka mtu rumande miaka mitano bila kusikilizwa!

Lakini kwenye kundi hilo kuna kesi nyingi za kubambikiwa. Mtu mwenye mamlaka akiamua, basi anampeleka mbaya wake polisi na hatimaye gerezani.

Baada ya kuiona habari hii ya Mara nilizungumza na DPP, na kwa kweli niseme wazi kuwa nilimpigia simu kumpongeza kwa dhati ya moyo wangu kwa kitendo alichokifanya Mara na kitendo kama hicho ambacho naambiwa kimekwisha kufanywa mkoani Lindi.

Kitendo kilichofanywa na viongozi hawa wote kwa umoja wao ni cha kizalendo na cha kiutu. Unaweza kusema Mungu atawalipa kwa wema, huruma na zaidi ya yote, kwa haki waliyowatendea wanadamu hawa.

Binadamu anayeshangilia mateso ya binadamu mwenzake asiye na hatia, huyo si binadamu. Magerezani kuna maelfu kwa maelfu ya watu wanateseka kwa kuonewa. Wanataabika kwa sababu ya matumizi mabaya ya madaraka ya baadhi ya viongozi wa kiserikali, polisi, watu wa vyombo vya usalama na wale wenye hila. Kuna watu wanaozea mahabusu kwa sababu tu ya chuki ya watu wenye madaraka au uwezo wa kifedha.

Sote tu binadamu. Ifike wakati kabla ya kumpeleka binadamu mwenzako polisi, jiridhishe kama kweli kuna ulazima huo. Kumpeleka mtu rumande kusifanywe kuwa ni kitu chepesi au rahisi.

Kwa dhati kabisa nampongeza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, DPP na wadau wote walioamua kiungwana kabisa kupita katika magereza ili kuwaokoa watu wanaotaabika humo bila hatia.

Hili jambo tunaweza kuliona ni dogo, lakini ukweli ni kuwa si dogo kamwe. Hili ni jambo kubwa linalostahili kujulikana kwa Watanzania wengi kwamba pamoja na malalamiko mengi tuliyonayo, bado tunao viongozi wanaotekeleza wajibu wao kwa kuwatendea haki watu wanyonge.

Ziara hizi za ukaguzi hazina budi zifanywe katika magereza yote nchini, na ikiwezekana ziguse hadi mahabusu za polisi ambako nako kuna watu wanaomaliza wiki na miezi wakiwa wanashikiliwa bila kufikishwa mahakamani.

Kwa kuwa uongozi unaonyesha utayari wa kushughulikia matatizo haya, sote hatuna budi kushiriki kwa pamoja kuwasemea wanyonge wanaoteseka kwa hila za wachache wenye madaraka na ukwasi.

Nakumbuka mwanzoni mwa miaka ya 2000 nilipiga picha ambayo nilijua wazi kuwa navunja sheria. Niliwapiga picha wafungwa kadhaa wa Gereza la Tarime wakiwa nusu uchi kwa kukosa nguo. Picha ile niliwaonyesha viongozi wa Jeshi la Magereza. Wakanionya nisiitumie kwa sababu sheria haziruhusu. Nikasema kama ni kufungwa ningekuwa radhi nifungwe kwa sababu isingewezekana binadamu wale watembee makalio yakiwa wazi na wengine sehemu za mbele zikiwa zinaonekana halafu niikalie picha niliyonayo.

Mungu ni mwema. Picha ile moja ilibadili kabisa hali ya wafungwa wote nchini mwetu. Zilishonwa nguo kwa wafungwa wote wa Tanzania na kuanzia hapo wakaanza kuvaa suruali badala ya kaptula. Kutetea heshima na utu wa binadamu ni jambo linalowezekana hata ikibidi kwa kuvunja sheria [zisizofaa].

Nirejee kuwapongeza DPP na timu yote iliyohusika kwenye kazi hii ya kuwaokoa maskini wanaoteseka magerezani bila sababu. Haya ya Mara na Lindi yatendeke nchi nzima. Kwa kufanya hivyo tutawafanya Watanzania wenzetu hawa wayafurahie maisha na bila shaka waipende serikali yao, kwa sababu wataona inawatendea haki. Mungu awabariki sana.

1671 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!