Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi amewataka Wana CCM kuacha nongwa za uchaguzi bali washirikiane katika kukijenga chama na kuwaletea wananchi maendeleo.

Hayo ameyasema jana kwenye kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Mkoa kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ya Familia takatifu Bombambili Manispaa ya Songea.

Dkt. Nchimbi amesema kuwa sio lazima jambo lako liungwe mkono na watu wote, kwani wengine wanamisimamo yao ambayo huwezi kuibadili nao ni watu Wazuri katika kuleta maendeleo kusudiwa ndani ya chama.

Katibu Mkuu CCM Taifa Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi akizungumza na wajumbe wa Halmashauri kuu ya Mkoa Ruvuma Jana wakati wa ziara yake ya siku nne mkoani humo.

Amesema kuwa amekuwepo Jimbo la Songea Mjini kama Mbunge kwa kipindi cha miaka 10 na  aliweza kushirikiana na wananchi wenye makundi tofauti tofauti na wenye misimamo tofauti na hakukuwepo na migongano yoyote kama ilivyo sasa watu limekuwa na nongwa.

“Ndugu zangu unakuta mtu aliyeshindwa uchaguzi ananongwa na aliyeshinda pia ananongwa hatuwezi kuendesha hiki chama kwa stahili hiyo na ndio maana tunatakiwa uchaguzi unapoisha tunaungana wote na kuwa kitu kimoja wapambe wote wanakwisha” amesema Dkt. Nchimbi.

Hata hivyo amewataka wanachama wa CCM na wasio wanachama kuhakikisha wanashiriki uchaguzi ujao wa serikali za mitaa kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha wanapatikana wenyeviti bora katika Nchi yetu na si vinginevyo.

Baadhi ya wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Mkoa ambao walikuwa kumsikiliza Katibu Mkuu CCM Taifa Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi.

Awali mwenyekiti wa CCM Mkoa Bw. Oddo mwisho amesema kuwa chama kipo imara kuhakikisha wanashinda kwa kishindo uchaguzi wa serikali za mitaa ikiwa ni pamoja na zawadi kwa Rais wa Jamuhuri  ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia suluu Hassan na kwamba ndio maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2025.

Baadhi ya viongozi wa Serikali waliohudhuria kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Mkoa.

By Jamhuri