Na Daniel Limbe, JakmhuriMedia, Chato

“SAFARI ya Maendeleo siyo lelemama” msemo huu ulitumiwa sana na aliyekuwa rais wa Tanzania,Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, kwa lengo la kuihamasisha jamii katika kuyapambania matamanio ya ndoto zao za maendeleo kwa manufaa ya sasa na baadaye.

Hatua hiyo ilikuwa ni chachu ya watu kufanya kazi kwa bidii baada ya serikali kuwatengenezea mazingira mazuri ya kuhakikisha kila mmoja anawajibika kwa kiwango chake ili kujiletea maendeleo yake,familia na taifa Kwa ujumla.

Hata hivyo kuna wakati alitumia maneno ya kitabu kitakatifu cha Biblia kwa nukuu ya “Asiye fanya kazi na asile” yote hayo ilikuwa ni kuwajengea watu uzalendo wa kufanya kazi kwa bidii na maarifa.

Aliyekuwa mwandishi wa tamthilia na Insha nchini Ireland,George Benard Shaw, aliwahi kuandika kuwa “Maendeleo hayawezekani bila mabadiliko ya kifikra, na wale ambao hawawezi kubadilika namna wanayofikiri hawawezi kubadili chochote”.

Maneno hayo yanadhihirisha wazi kuwa ili jambo zuri na jema liweze kutokea ni lazima baadhi ya watu waweze kufikiria kwa upana,watumie hekima,busara na maarifa yao katika kutekeleza wajibu wao kuhakikisha maendeleo yanapatikana licha ya uwepo wa baadhi ya wapingaji na wakosoaji wasioona manufaa kwa wakati huo.

Hata hivyo Makala hii inajikita kuzungumzia ndoto za Hayati Dkt. Magufuli katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam tawi la Chato mkoani Geita, ujenzi uliokwama tangu alipofariki dunia mwaka 2021.

Wachambuzi wa mambo wanasema ili jambo zuri litokee ni muhimu kupiga picha ya ndotoni kisha kuigeuza katika uhalisia na kuanza utekelezaji wake,na kwamba ujenzi wa chuo hicho ilikuwa ni ndoto njema yenye uhalisia kwa jamii ambayo ilibaki nyuma kielimu tangu enzi za ukoloni.

Aidha mradi huo ulijulikana kwa jina la Ujenzi wa miundombinu ya Kituo cha Utafiti wa Viumbe Maji Baridi yaani “Multi-Disciplinary Freshwater Research Centre” – Chato, Mkoani Geita kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Licha ya baadhi ya watu kubeza,kukejeli na kutoa dhihaka kwa ujenzi wa chuo hicho bado Hayati Dkt. Magufuli haikumkatisha tamaa katika kuisimamia ndoto hiyo ambapo hatua za awali za ujenzi zilianza kufanyika mwaka 2020 chini ya mkandarasi Suma JKT.

Msimamo wake huo unafananishwa na maneno ya Bruce Barton,aliyekuwa mbunge wa Amerika(1886-1967) anasema “Kabla ya kukata tamaa,tazama nyuma na kusoma masuto yaliyosemwa dhidi ya Lincoln”

Abrahamu Lincoln alikuwa rais wa Marekani,kufikia ngazi hiyo alikabiliana na uzushi,umbeya na masengenyo mengi lakini hakukata tamaa mpaka pale ndoto yake ilipotimia.

MAONI YA WANANCHI

Jackson Kashimba,mkazi wa Nyamirembe anasema maono ya Hayati Dkt. Magufuli, hayapaswi kupuuzwa hata kidogo na kwamba ujenzi wa Chuo hicho ni fursa njema kwa vijana wanaotamani kusoma masuala ya uvuvi.

“Naishauri serikali yangu itekeleze Kwa vitendo ndoto za mzee wetu Hayati Magufuli, kile Chuo Kikuu cha Kasagala kilisimama kujengwa tangu alipofariki na hiyo yote ilionyesha kulikuwa na watu wasiopenda maendeleo ya watoto wetu walioko pembezoni mwa nchini”.

“Hayati alikusudia kuzisambaza fursa za maendeleo sehemu zote za nchi ili kuwasogezea wananchi karibu maendeleo,ikumbukwe miaka ya nyuma wakazi wa Kanda ya ziwa tulikuwa nyuma sana ki elimu lakini hali hiyo ilitokana na vyuo kuwa vichache maeneo yetu na vingi vilikuwa mijini pekee”anasema Kashimba.

Roza Sebastian,mkazi wa kijiji cha Msilale anaitaka serikali kuendeleza ujenzi wa Chuo Kikuu cha UDSM tawi la Chato, Kwa madai ujenzi huo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na kwamba manufaa yake ni kwa jamii nzima na siyo kwa baadhi ya watu wachache.

Anasema kukamilika kwa ujenzi huo utasaidia sana uchumi wa nchi Kwa kuwa kutakuwa na ongezeko la vijana wenye maarifa ya juu katika nyanja za uvuvi wa samaki na uhifadhi wa mazingira.

“Ukitazama kwa sasa shughuli za uvuvi zinazofanyika ni za kizamani sana,watu wanapaswa kupata elimu na maarifa ya uvuvi mpya wa kisasa ambao utakuwa endelevu Kwa vizazi vijavyo, ukitazama hivi sasa uvuvi uliopo niwa kubahatisha na ni hatari Kwa usalama wa mazingira” anasema Roza.

Simon Hezron msomi wa elimu ya juu katika fani ya uhandisi na elimu, anaishauri serikali kuendelea kitawanya matawi ya elimu ya juu ili kuwapunguzia wazazi gharama Kwa watoto wao wanaosoma kwenye vyuo vikuu vilivyoko Kanda zingine zilizoko mbali.

“Ukitazama pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) wanachuo ni wengi sana kiasi kwamba unaona wazi kuwa Chuo kile kimekuwa na wanafunzi wengi ikilinganishwa na miundombinu iliyopo”

“Hali hiyo imekuwa ikisababisha wanafunzi wengi kukosa hosteli za kukaaa na hivyo kulazimika kukaaa mbali na chuo, ambapo mazingira hayo huchagiza wanafunzi kuchelewa vipindi, majaribio na hata mtihani wa chuo au wa muhula(Semester exams(SE) au University exams(UE)”anasema Hezron.

Anasema mambo hayo na mengine husababisha ugumu za maisha kutokana na gharama kubwa za usafiri, chakula na gharama za vyumba mtaani wanakopanga,licha ya uwepo wa kozi mpya zinazoongezwa.

Kutokana na hali hiyo, ipo haja kubwa kwa baadhi ya kozi kuhamishiwa kwenye matawi ya vyuo vikuu ili kupunguza msongamano na gharama kwa wazazi na walezi.

“Binafsi ninapongeza sana maono ya Hayati Dkt. Magufuli katika ujenzi wa matawi ya vyuo vikuu ambavyo ni vikubwa hapa nchini,mfano hilo tawi la UDSM aliloanza kulijenga kule Chato lingesaidia sana wanafunzi wengi wanaotoka ukanda wa ziwa Kwa sababu takribani aslimia 75 ya wakazi wake ni wakulima na wavuvi”anasema Hezron.

Anashangazwa na kuona Chuo hicho kilikwama kuendelea kujengwa licha ya kwamba zilitengewa fedha na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,kupitia wizara ya elimu chini ya Waziri Prof. Adolf Mkenda.

Huku Paulo Butondo,mkazi wa mpogoloni,akitazama Chuo hicho kama kichocheo cha uchumi kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo kwa madai watapata fursa za kibiashara ikiwemo uuzaji wa vyakula na soko la nyumba za kupanga.

WAZIRI MKUU

Hata hivyo Juni 3 mwaka huu Waziri mkuu Kassim Majaliwa,akizungumza na wananchi wa wilaya ya Chato mkoani Geita kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika stendi ya zamani Chato mjini alifufua matumaini ya wananchi hao baada ya kusisitiza kuwa ndoto za Hayati rais Magufuli lazima zitekelezwe.

Akasema ujenzi wa Chuo Kikuu tawi la UDSM uliotazamiwa kujengwa kwenye kijiji cha Kasagala lazima ukamilike na kwamba ujenzi wa awali tayali umeanza.

“Tunajenga vyuo vikuu kimkakati,tuna vyuo vikuu saba ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es salaam ambacho kina vitivo mbalimbali, sasa tunaanza kuhamisha baadhi ya vitivo na kuvitawanya na Chato kitakuja kitivo cha Marini(Marine)” anasema.

“Lengo ni kuwaelimisha wananchi walioko maeneo haya ikiwemo,Geita,
Sengerema,Buchosa,Muleba,Ngara, Bukoba,Karagwe hadi kule Kyerwa wote wanatakiwa waje hapa kusoma ngazi ya digrii ya marini,na ndiyo maana serikali yenu ya awamu ya sita imeweka Chuo hicho hapa Chato na ujenzi umeanza”anasema Majaliwa.

Kadhalika anasema chuo hicho kitakuwa mwarobaini kwa vijana kupata maarifa na ujuzi mkubwa wa kujiajili ukilinganisha na awali ambapo vijana wengi walikuwa wakisoma kwa lengo la kuajiliwa na serikali ambako ajira zimejaa.

Hakika mpango mkakati huo unapaswa kuungwa mkono kwa sababu unakusudia kutoa haki sawa Kwa wananchi walioko pembezoni mwa nchi katika kupata maarifa bora na kwamba inaonyesha dhamira njema ya serikali kutekeleza ndoto za Hayati rais Dk. Magufuli.

Mwanamuziki maarufu na mwanzilishi wa miondoko ya Rege (Reggae) duniani,Robert Nesta Marley,aliwahi kusema “Rafiki wa kweli ni kama nyota,utamtambua wakati wa giza litakapokuwa limekuzunguka”.

Kwa mujibu wa sera ya elimu na mafunzo toleo la mwaka 2023 Serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu na mafunzo,itayaweka mkazo zaidi ili kuweka mazingira mazuri ya kufikia malengo ya mipango ya maendeleo katika elimu.

Masuala hayo ni pamoja na kuimalisha mfumo wa elimu na mafunzo ili uwe na tija na ufanisi,kutoa fursa za elimu na mafunzo kwa usawa na kuendelea kuboresha mitaala ya elimu na mafunzo ili kukidhi mahitaji ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Hivyo dira ya maendeleo na mafunzo nchini ni “Kuwa na Mtanzania aliyeelimika na mahiri mwenye maarifa,stadi,uwezo na mtazamo chanya utakaomwezesha kuchangia katika kuleta maendeleo ya taifa”

Kwa upande mwingine dhima ya sera hiyo ni “Kuinua ubora wa elimu na mafunzo Kwa kuweka mifumo na taratibu zitakazoleta ongezeko kubwa la watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha daima ili waweze kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa” inasema sera hiyo iliyosainiwa na Waziri wa elimu Prof. Mkenda.

KAULI YA RAIS SAMIA*

Machi 26 mwaka 2021 katika mazishi ya Hayati rais Magufuli, rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan,mbali na mambo mengine alisisitiza kuwa miradi yote iliyoanzishwa na mtangulizi wake itakamilika kama ilivyo kusudiwa.

Kauli hiyo pia aliilejea Oktoba 14 mwaka 2021, aliposhiriki kwenye kilele cha mbio za mwenge wa uhuru kitaifa zilizofanyika Chato kwenye uwanja wa Magufuli uliopo mlimani rubambangwe km chache toka nyumbani kwao Hayati rais Magufuli.

Hata alipopita kwenye kijiji cha Bwanga wilayani humo Juni 8 mwaka 2022, kwaajili ya kuelekea mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi,rais Samia aliendelea kusisitiza kuwa miradi yote iliyoanzishwa na mtangulizi wake kwenye wilaya hiyo itakamilika pasipo kukwama.

Kutokana na kauli hizo wananchi wamekuwa wakiendelea kusubiri ahadi za kiongozi huyo licha ya baadhi ya miradi kuonekana kusimama ikiwemo ujenzi wa Chuo hicho Kikuu ambacho fedha za ujenzi wake zilitolewa na serikali lakini utekelezaji ukawa fumbo la Imani.

Hata hivyo bado faraja ipo kwa kuzingatia msemo wa aliyekuwa rais wa Zaire (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) 1965 – 1997, Joseph Desire Mobutu Sese Seko,kuwa “Mtemi ni mtemi tu,yeye ni tai hawezi kuguswa na mate yaliyotemwa na chura”.

KATIBA YA JAMHURI

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 11 kifungu kidogo cha (2) Kila mtu anayo haki ya kujielimisha ,na Kila raia atakuwa huru kutafuta elimu katika fani anayoipenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake.

Aidha Ibara ya 13 kifungu kidogo cha (5) Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya Ibara hii neno “kubagua” maana yake ni kutimiza haja,haki au mahitaji mengineyo Kwa watu mbalimbali Kwa kuzingatia utaifa wao,kabila,pahala walipotokea,maoni yao ya kisiasa,rangi,dini,jinsia au hali yao ya maisha kwa namna ambavyo watu wa aina fulani wanafanywa au kuhesabiwa kuwa dhaifu au duni na kuwekewa vikwazo au masharti ya pingamizi ambapo watu wa aina nyingine wanatendewa tofauti au wanapewa fursa au faida iliyoko nje ya masharti au sifa za lazima, ispokuwa kwamba neno “kubagua” halitafafanuliwa Kwa namna ambayo itaizuia serikali kuchukua hatua za makusudi zenye lengo la kurekebisha matatizo mahususi katika jamii.

NINI KIFANYIKE ?

Baadhi ya wadau wa maendeleo akiwemo Peter Magege na Selemani Kahindi, wanaiomba serikali kutekeleza kwa vitendo ndoto za Hayati Dkt. Magufuli pamoja na ahadi za rais Samia katika kuhakikisha miradi aliyoachiwa na mtangulizi wake haikwami wala kukwamishwa na baadhi ya watu wasioitakia mema serikali ya awamu ya sita.

Waziri mkuu, afuatilie kwa ukaribu kujua hatua za ujenzi wa chuo Kikuu cha UDSM tawi la Chato ili kuondoa sintofahamu za baadhi ya watendaji waliochini yake katika mradi huo.

Mkuu wa mkoa wa Geita,Martine Shigela,amsaidie rais Samia katika usimamizi wa miradi yote iliyoahidiwa kwenye mkoa huo.

Wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa serikali ya awamu ya sita katika kudhibiti wizi na upotevu wa vifaa vinavyotolewa na serikali kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Jamii izitumie vizuri fursa za maendeleo zinazowekwa na serikali kwenye maeneo yao kuhakikisha wanajiondolea umaskini na vipato na kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora kwa manufaa ya sasa na baadaye.