Ndugu Rais, dunia nzima hivi sasa imesukwa kwa mitandao. Hii haikwepeki. Imeyafanya yanayotendeka katika nchi zetu hizi yasiwe siri tena. Kila kitu kinaanikwa.

Katika siku za hivi karibuni habari zetu nyingi zimeijaza mitandao mingi. Ukitaka kujua habari zetu za kutusifia katika mitandao hiyo mpaka uzitafute. Zile ziileteazo nchi yetu na wanawema wa dunia hii majonzi na masikitiko, zinamwagika zenyewe kila mtandao utakaoufungua. Tunajua huu ni upepo uvumao, lakini hali hii haiwezi kukubalika. Yatupasa tukae kama wanafamilia moja ili tutafakari kwa pamoja hali hii mpaka lini?

Kuna mwanamwema hapa nchini aliandika kwa kirefu sana kuhusu Raila Odinga yule aliyekuwa mpinzani mkuu wa Rais Uhuru Kenyatta. Kila alipoandika alisema, ‘iko siku Raila Odinga atakuwa Rais wa Kenya’.

Mwanamwema huyu alikuwa kionambali. Akihutubia katika kile walichokiita ‘National Breakfast Prayer’ – meza ya maridhiano, Raila Odinga alisema, “Kama kaburu Fredrick de Klerk alikaa pamoja kwa maridhiano na Nelson Mandela kisha wakashikana mikono, mimi ni nani ambaye siwezi kukaa kwa maridhiano na ndugu yangu Uhuru Kenyatta na kisha tushikane mikono?”

Leo Afrika Kusini weupe kwa weusi wanaishi kwa amani kwa furaha wakiwa na matumaini makubwa ya ustawi. Leo wana Kenya si wale tuliowajua. Wana amani ya kweli. Wanaishi kama ndugu kwa upendo, umoja na mshikamano wakiwa na matumaini makubwa ya ustawi wao na wa nchi yao. Iweje sisi tuendelee kunyosheana vidole?

Kinachoshindikana ni nini kuwa na meza ya maridhiano watawala wetu na wapinzani wetu washikane mikono ili na sisi tupate amani ya kweli, tuishi kwa furaha tukiwa na matumaini ya ustawi wetu na wa nchi yetu?

Lakini baba si ndiye awaongoze wanae kwenye meza ya maridhiano.  Hawa hawakusema baba karibu mezani kwa maridhiano? Karibu mezani ili kwa pamoja kama ndugu tuulizane ni nani mwenye shida hii? Jahazi letu linazama. Tukiliacha lizame hakuna atakayebaki salama. Kama kuna mtu anajua kuwa ndiye mwenye shida hii, kwa unyofu aseme, “Nitupeni mimi!’’ Nchi yetu irudie kuwa na amani ili tuishi kwa upendo na furaha kama tulivyokuwa zamani. Leo kuna baadhi yetu wenye itikadi tofauti kuitana ndugu ni kama kutukana tusi. Waliosema hakuna makali yasiyokuwa na ncha walimaanisha kuwa hakuna chenye mwanzo kisichokuwa na mwisho. Kwa kuwa iko siku tulianza, basi iko siku na sisi tutapita.

Haya mabaya yanayosemwa juu yetu katika mitandao tukiyaacha yaendelee kuzagaa bila kuyatolea majibu sahihi, mwishowe yataaminika. Hivi sasa yanafunguka mengi. Wa kuyatolea majibu sahihi ni sisi wote katika ujumla wetu, lakini katika kweli na si kwa unafiki. Tukiyaacha yaaminike kutakuwa na kishindo kikubwa kwa sababu walisema hata mbuyu ulianza kama mchicha. Siasa sasa zinabadilika. Watawala kupambana na wapinzani ni siasa ambazo sasa zimepitwa na wakati. Dunia sasa inashuhudia maridhiano. Afrika Kusini viongozi wa maridhiano walituzwa nishani maarufu duniani ya ‘NOBEL’, tunayangojea ya Kenya. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tunayashudia maridhiano. Watu lazima wakubali kusoma alama za nyakati. Sisi siyo kisiwa.

Mwanamwema mmoja alisema, “Hakuna kitu unaweza kufurahia kama kujua siku yako ya kuzaliwa na kujua kwanini ulizaliwa.” Kama ingejulikana kuwa kuzaliwa kwetu ndiyo kungeleta mateso na machungu makubwa kwa wengine na kutusababishia wenyewe visasi vya maisha hakika wengi tungeijutia siku ya kuzaliwa kwetu. Nilitoa mfano wa Maonyesho ya Kimataifa ya vitabu ya Nairobi Kenya. Watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia walihudhuria. Yalifunguliwa na mpinzani ndugu Raila Odinga.

Kuonyesha mshikamano wa wana Kenya yalifungwa na mke wa Rais Uhuru Kenyetta. Mikosi gani tulizaliwa nayo sisi hata tunashindwa kuwaiga hata ndugu zetu wa Kenya?

Sheria ya mabadiliko ni moja. Katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu kilichoandikwa miaka 16 iliyopita maandiko yanasema, “Rashidi

Shangazi aliendelea, akasema, “Tunataka Rais ajaye awe na uwezo wa kusoma alama za nyakati. Aelewe kuwa nyakati hizi ni nyakati za mabadiliko. Mabadiliko yana tabia yake. Yakiamua kuja, huja bila mjadala wala mbadala. Ni kiongozi mwenye busara tu ndiye huyapokea mabadiliko kwa amani.

“Nyakati za kukosoa utawala mbovu ukaitwa mchochezi zimepita. Nyakati za kuomba kura kwa wananchi kwa kuwapigia zumari, gitaa au kunengua viuno kwa taarabu zimepita. Nyakati za kumwona mtu mwenye mawazo ya kisiasa tofauti na wewe ni adui wa nchi au ni hatari kwa usalama wa taifa zimepita.

“Viongozi wote ambao hawakuwa tayari kuyapokea mabadiliko kwa hiari na amani sasa hivi wanatangatanga katika sehemu mbalimbali duniani, wenyewe wakiziita sehemu hizo uhamishoni. Wengine wamefikia huko wakiwa hoi, maskini wa kutupwa, licha ya mali nyingi walizowapora wananchi wao. Nchi yetu ni mali yetu sote tuliyopewa na Mwenyezi Mungu katika umoja wetu. Hakuna chama cha siasa chenye hakimiliki ya nchi hii. Hata chama tawala hakina hakimiliki hiyo.’’

Akitetea hoja ya utaifa alisema, “Siku za kampeni na uchaguzi huja na kupita, lakini taifa hubaki. Lazima taifa libaki moja na lenye mshikamano hata baada ya uchaguzi. Huu ndio wakati wa vyama vilivyoshinda katika ngazi mbalimbali kutekeleza sera zao zilizoko katika ilani zao za uchaguzi. Ni wakati wa kutekeleza ahadi walizozitoa wakati wa kampeni. Hakuna nafasi ya chuki, kejeli au utengano wowote wa kiitikadi kwa walioshinda au walioshindwa. Baada ya hapo, wananchi lazima waelekeze nguvu zao kwa pamoja katika kazi ya ujenzi wa Taifa lao. Serikali lazima iwe na uwezo wa kuwajenga wananchi kuheshimu misimamo na mitazamo ya watu wengine na  kuwaimarisha kwa kuwapa uwezo wa kufanya uamuzi wa busara.’’

“Watu wanataka serikali ya watu, inayoendeshwa na watu wenyewe, kwa ajili ya watu. Rais ajaye lazima atambue ukweli kwamba mawazo yanayotawala nchi huwa si ya wanasiasa peke yao na vyama vyao. Kuna jumuiya na watu binafsi wenye nafasi kubwa kijamii ambao fikra na shinikizo lao huathiri mwenendo wa siasa, utawala na jamii.’’ Alimaliza Rashidi Shangazi.

By Jamhuri