Gazeti la JAMHURI linalochapishwa na kusambazwa siku ya Jumanne kila wiki nchini na nchi jirani Afrika Mashariki, limeongoza dhidi ya vyombo vingine vyote vya habari Tanzania Bara na Zanzibar vilivyohusishwa kwenye utafiti wa ubora wa maudhui kwa vyombo vya habari nchini kwa mwaka 2018.

Utafiti huo uliofanywa na Baraza la Habari Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Spurk Media Consulting Ltd ya Switzerland, umeweka bayana kuwa Gazeti hili la JAMHURI limevibwaga vyombo vingine vya habari 24, kuanzia baadhi ya magazeti mengine maarufu ya kila siku, televisheni kubwa nchini, redio mbalimbali na mitandao mashuhuri ya kijamii katika tasnia ya upashanaji habari.

Katika kipimo cha ubora wa maudhui kwa vyombo vya habari Tanzania 2018, JAMHURI limeongoza kwa kupata asilimia 47.6 mbele ya Gazeti la kila siku la Mwananchi lililoshika nafasi ya pili kwa kuwa nyuma ya JAMHURI kwa asilimia 4.3, yaani likiambulia asilimia 43.3.

Katika orodha hiyo ya kitafiti, magazeti mengine yalishika nafasi za mbali; Gazeti la Serikali la Daily News likishika nafasi ya saba, gazeti la Nipashe nafasi ya 10, gazeti la Kiingereza la The Citizen likishika nafasi ya 12 wakati Guardian likishika nafasi ya 13, huku ZanzibarLeo likiwa mbele yao kwa kushika nafasi ya sita kati ya vyombo vya habari 24 vilivyohusika.

Vyombo vingine vya habari vilivyoshirikishwa ni CG FM iliyoshika nafasi ya nne, Azam TV iliyoshika nafasi ya tano, Pangani FM nafasi ya nane, ITV nafasi ya tisa, TV TBC1 nafasi ya 11, Dodoma FM nafasi ya 14, Arusha 1FM nafasi ya 15, Radio TBC Taifa nafasi ya 16, Radio Free Africa nafasi ya 17, Highlands FM nafasi ya 18, ZBC Radio nafasi ya 19, Radio Clouds FM nafasi ya 20, Radio One nafasi ya 21, Zenji FM nafasi ya 22, Ayo TV nafasi ya 23 na Michuzi nafasi ya 24.

Kwa mujibu wa watafiti hao, vigezo vilivyotumika katika kupima ubora wa maudhui vilipata kujadiliwa na kukubaliwa na wahariri na wadau wengine wa sekta ya habari nchini, vigezo ambavyo vimekuwa vikitumika kupima ubora wa maudhui nchini,  na katika utafiti huu viligawanywa katika maeneo manne.

Kwanza, sampuli ya vyombo vya habari. Katika hili, mwaka 2017 jumla ya vyombo vya habari 12 vilijumuishwa kwenye utafiti wa aina hii ukiwa ni utafiti wa majaribio, ambavyo ni The Citizen, Daily News, The Guardian, Mwananchi na Nipashe.

Aina ya vigezo hivyo vya kitaaluma ni pamoja na matumizi ya vyanzo vingi vya habari, makala na vipindi, kuripotiwa kwa habari ambazo hazitokani na matukio ya habari, bali zitokanazo na jitihada ya chombo cha habari chenyewe.

Aina nyingine ya kigezo ni utimilifu wa habari na hapa, mambo ya kuzingatiwa ni uwepo wa mitazamo mbalimbali kwenye habari, ujumuishaji wa sababu za kuripotiwa kwa habari fulani na uwepo wa usuli wa habari husika, lakini pia ujumuishaji wa maoni mbalimbali, yakiwemo yale yanayokosoa utendaji wa Serikali.

Aina nyingine katika orodha ya vigezo ni kueleweka kwa habari, mambo makuu matatu yakitazamwa, kwanza, muundo mzuri wa uandishi ambao unaunganisha sehemu mbalimbali za habari kwa ufasaha, lakini pia uwezo wa mwandishi kuelezea ama kufafanua takwimu kwa wasomaji, wasikilizaji na watazamaji. Aina nyingine ya kigezo ni maadili, kilicholengwa zaidi hapa ni kutoa nafasi kwa watuhumiwa kujieleza.

Mengine yaliyobainika kwenye utafiti huo ni vyombo vingi kutoripoti habari zitokanazo na juhudi binafsi za vyombo hivyo na badala yake vimekuwa vikitegemea zaidi habari za matukio.

Hata hivyo, utafiti huo hauonyeshi sababu za mwenendo huo, lakini wadau walioalikwa katika uzinduzi wa taarifa hiyo, Februari 15, wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, walibainisha maoni tofauti kuhusu hali hiyo.

Utafiti huo unaonyesha kuwa masuala ya kisiasa yaliripotiwa kwa kiwango chini – kwa asilimia 11 wakati asilimia 29 ya habari zilihusu miundombinu, mafuta na gesi, usafirishaji na biashara zikitawala kwa asilimia 29.

Habari nyingine kuhusu maeneo mengine ni pamoja na maendeleo (asilimia 28) ikijumuisha afya, elimu, kilimo na mazingira, masuala yenye mvutano kama matatizo ya kijamii, migogoro, haki za binadamu, jinsia na utawala bora yalitawala kwa asilimia 16, huku ajali na uhalifu au kesi za mahakamani zikitamba kwenye kuripotiwa na vyombo vya habari kwa asilimia 12.

Akiwasilisha matokeo yao utafiti huo siku hiyo jijini Dar es Salaam, mmoja wa watafiti, Abdallah Katunzi, alisema sampuli ya utafiti huo imejumuisha habari, makala, vipindi na ‘posti – mitandaoni’ 1,886 kutoka magazeti saba, redio mbili, vituo vinne vya televisheni, blogu moja na mtandao mmoja.

Katunzi, ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema katika utafiti huo, magazeti yanaongoza kwa kuripoti masuala ya kisiasa, lakini yako katikati kwenye masuala ya kiuchumi, maendeleo na ajali au uhalifu. Alisema redio zinaripoti zaidi habari za maendeleo wakati televisheni zikiripoti habari za uchumi.

“Habari zinazotoka mijini ni asilimia 56 ya habari zote. Magazeti na redio za kitaifa zinaripoti kwa kufuata mfumo huo. Televisheni zinaripoti zaidi habari za mijini kwa asilimia 69, lakini redio za mikoani zinaripoti kwa kiwango kidogo, badala yake zinatoa nafasi kwa habari zinazotoka nje ya miji mikubwa na maeneo ya vijijini,” anasema.

Mtafiti Mwenza, Christoph Spurk kutoka Taasisi ya Spurk Media Consulting Ltd ya mji wa Bern, Switzerland, anasema utafiti huo unabainisha kwamba vyombo vingi vya habari haviripoti habari zitokanazo na mikakati yao badala yake vinategemea matukio.

Spurk alisema utafiti unabainisha kwamba vyombo vingi vinaripoti habari zenye chanzo kimoja cha habari, havitumii kiasi cha kuridhisha – wanawake kama vyanzo vya habari na haviripoti ukosoaji dhidi ya serikali.

Kuhusu habari za kuikosoa serikali, Spurk alisema mtandao wa Jamii Forum unaongoza kwa asilimia 35 na kufuatiwa na kituo cha redio cha Pangani FM kilichopata asilimia 15 wakati vyombo vingine vikiwa na viwango vya chini.

Utafiti huo unabainisha kwamba vyombo vya habari vinavyoripoti habari ambazo vyanzo vyake ni wanawake pia vimeshuka, Gazeti la JAMHURI linaongoza likiwa na asilimia 16 wakati Mwananchi lina asilimia 8.

Kuhusu habari zenye mitazamo tofauti ndani ya habari, utafiti umebainisha kushuka kwa kiwango hicho huku Gazeti la JAMHURI likipata asilimia 30, likifuatiwa na Daily News pamoja na Zanzibar Leo lililopata asilimia 15.

Awali akizindua ripoti ya utafiti huo, Balozi wa Uswisi nchini, Florence Mattli, alisema vyombo vya habari nchini na ulimwenguni kote vinapita katika wakati mgumu kutokana na msukumo mkubwa kutoka serikalini.

Alisema vyombo vya habari vinakabiliwa na changamoto hiyo ambayo inaathiri maudhui yake kwa sababu vinakuwa katika udhibiti mkubwa wa maudhui, jambo linalokwamisha majukumu yake ya msingi.

“Ninaamini vyombo vya habari bora ni muhimu kwa maendeleo ya nchi. Kupitia vyombo vya habari tunaweza kupambana na rushwa. Wanaonufaika na vyombo vya habari vinavyofanya kazi ipasavyo ni wananchi,” anasema Mattli.

Balozi Mattli alivitaka vyombo vya habari kutumia matokeo ya utafiti huo kama kioo cha kujisahihisha.

Wakizungumzia matokeo ya utafiti huo, baadhi ya washiriki walishtushwa na taarifa ya habari za siasa kushuka. Pia, walieleza kushangazwa na taarifa ya kwamba redio za kijamii zinafanya vizuri kuliko redio za kitaifa.

Walisema vyombo vya habari vinawajibu mkubwa wa kuhamasisha maendeleo kwa kutoa habari zenye weledi, zenye masilahi kwa umma na zenye kuwasimamia wenye mamlaka kuhakikisha wanatenda kulingana na taratibu zilizowekwa. Hata hivyo, washiriki hao walisema wajibu huo muhimu unaweza kutimizwa na kuendelezwa pale tu vyombo vya habari vinapoweza kuripoti  kwa kufuata vigezo vya taaluma.

Utafiti unabainisha, kwa mfano, habari za magazeti ni zao la habari za matukio kwa asilimia 72 wakati makala zinazalishwa kwa kutegemea jitihada ya vyombo husika kwa asilimia 85. Kwa upande wa televisheni, asilimia 78 ya habari ni zao  la habari za matukio, wakati asilimia 90 ya vipindi vinazalishwa nje ya mfumo wa kufuata matukio. Lakini pia kuna tofauti kubwa miongoni mwa vyombo vya habari, kwa mfano, Gazeti hili la JAMHURI lililofanya vizuri  kwa mwaka 2018 habari zake zinatokana na jitihada za waandishi wake kutafuta habari hizo kwa asilimia 63, wakati Gazeti kama la The Guardian katika eneo hilo linafanya kwa asilimia 19 pekee.

Ukitazama vigezo vya ukamilifu wa habari, matokeo ya utafiti yanaainisha kwamba si wa kuridhisha, ni asilimia 23 tu ya habari, vipindi na makala zilizochambuliwa  ndizo zilikuwa  na maelezo ya kwa nini habari hizo zimeandikwa (root causes) wakati asilimia tisa pekee ya sampuli yote ndiyo imeweza kutoa usuli (back ground) wa habari zilizoandikwa.

Kwa upande wa habari kueleweka kwa walengwa (wasomaji, watazamaji na wasikilizaji) hali inaridhisha kwani asilimia 56 ya kazi zote zilizochambuliwa zimekuwa na muundo mzuri wa uandishi huku zikiunganisha sehemu mbalimbali za habari  kwa mtiririko mzuri.

Hata hivyo, bado kuna changamoto kwa vyombo vya habari, inakuwa namna ya kuelezea takwimu kwa namna ambayo inamsaidia msomaji au msikilizaji kuelewa takwimu hizo. Ni asilimia 25 pekee ya kazi zote imeweza kueleza takwimu kwa kumrahisishia  mlengwa kuzielewa.

Kwa upande wa maadili, asilimia 42 ya sampuli yote imeshindwa kuwapa nafasi watuhumiwa kujieleza, ukilinganisha  na asilimia 60 ya mwaka 2017. Magazeti yamekamata kigezo hiki  kwa asilimia 50 huku redio na televisheni ni kwa asilimia 33.

Kuna tofauti kubwa kati ya redio, televisheni na magazeti lakini hata hivyo kwa ujumla, magazeti yamefanya vema kwenye vigezo vingi  ukilinganisha na televisheni na redio. Magazeti yanaongoza kwa vigezo vyote kwa asilimia 37.2 yakifuatiwa na televisheni (asilimia 31.4) na redio za mikoani kwa asilimia  30.5 na redio za kitaifa kwa asilimia 24.9.

Moja ya matokeo ya kipekee katika utafiti huu ni kwamba redio za mikoani zimefanya vizuri kuliko redio kubwa za kitaifa, na vyombo vya habari kutoka Zanzibar vimefanya vizuri  kama vile vya Tanzania Bara.

Habari nyingi zinazoripotiwa kwenye vyombo vya habari ni kutoka Dar es Salaam ikifuatiwa na Dodoma pamoja na Arusha. Kwa upande wa Zanzibar, Mkoa wa Mjini Magharibi  unaongoza ukifuatiwa na Kaskazini Pemba. Mikoa mingine inapewa  nafasi pia japo kidogo, isipokuwa pale inapojitokeza kuna kituo cha redio kwenye mkoa fulani.

Utafiti huu pia umebaini kwamba ni vyombo vya habari  vichache vinavyoandika habari kwa namna moja au nyingine zinakosoa utendaji wa serikali. Ni mtandao wa JamiiForums pekee ndio ulioonekana kuwa na idadi kubwa ya maudhui ambayo yanakosoa utendaji wa serikali kwa asilimia 35, ukifuatiwa  na redio za mikoani na magazeti kwa asilimia nne kila moja. Kwa upande wa magazeti, Gazeti la JAMHURI linaongoza kwa asilimia 9 likifuatiwa na Mwananchi (asilimia 8) kwa kuwa na habari zenye mlengo huo. Kwa upande wa redio, Pangani FM inaongoza  kwa asilimia 15, CG FM (asilimia 10) na Micheweni  FM (asilimia 6), redio kadhaa (kwa idadi kubwa) zimebainika kutokuwa na  habari yenye  kukosoa utendaji wa serikali (TBC Taifa, Clouds FM, Arusha 1 FM, Zenji FM na ZBC).

Ili kuimarisha ubora wa vyombo vya habari, imependekezwa kwamba ili kujiboresha vyombo vya habari vitumie matokeo ya utafiti huu na hasa vikijikita kwenye  maeneo ambayo havijafanya vizuri au viko chini ya wastani.