Ndugu Rais toka tupate uhuru nchi hii imeongozwa na marais watano katika awamu tano tofauti.

Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere ameshatangulia nyumbani kwa Baba katika mapumziko yake ya milele. Kila anayemkumbuka humwombea mapumziko ya amani.

Tumekuwa tukifundishwa kuwa wakati wa uumbaji, Mungu aliumba watu wawili wawili, lakini `Nyerere wa pili’ katika nchi hii bado hajatokea. Basi wana wema tudumu katika imani.

Kama ni kweli maisha tuishiyo ni sawa na kitabu kinachoandikwa, basi Mwalimu Nyerere ametuachia kitabu chenye hadithi njema zinazofanana na zile zilizomo katika vitabu vitakatifu.

Huenda ni kwa bahati mbaya waliomfuatia katika mamlaka makuu ya nchi,  hakuna aliyefanana naye. Huenda siku moja tukaja kupata Rais aliye kinyume na Baba wa Taifa.

Kwa wanaomfahamu vizuri, Mwalimu  Nyerere, neno ‘wasiojulikana’ lisingeweza kuenea katika kichwa chake. Mtu huyu alikuwa muadilifu wa kweli.

Katika maisha yake alimtanguliza Mungu bila kujitangaza kama ambavyo wengine tunavyofanya sasa.

Mwalimu Nyerere alifanya kitakatifu kila jumapili kama amri za Mungu na kanisa zinavyoelekeza.

Kutangazwa kila mtu anapoigusa nyumba ya ibada siyo vibaya, lakini huko kunafanana na kumpaka rangi.

Timamu hupaka rangi kisichopendeza ili kipendeze. Pamoja na hayo lakini imeandikwa kuwa unapotenda jema kwa mkono wako wa kulia hakikisha mkono wako wa kushoto haujui.

Ndugu Rais, masikini wa nchi hii walimwita Mwalimu Nyerere, ndugu. Watanzania waliitana ndugu, kutoka mponda kokoto hadi Kiongozi Mkuu wa nchi. Sikumbuki kiongozi mkuu zaidi ya Olof Palme aliyeyaishi maisha ya wananchi.

Kama Mwalimu Nyerere angekuwa mroho au mbinafsi kwa kasi hii, katika miaka yake 23 ya urais Butiama leo, lingekuwa jiji kubwa. Alikuwa kiongozi mzalendo aliyeipenda nchi yake kutoka katika kifua chake.

Lakini zaidi aliwapenda Watanzania kama alivyoipenda nafsi yake na kumpenda Mungu wake. Alipokuwapo Mwalimu Nyerere, baba alikuwapo, hofu katika nchi ingetoka wapi?

Alitufundisha upendo, tupendane tuitane ndugu, nani angishi kwa hofu katika nchi hii iliyojaliwa neema nyingi kiasi hiki?

Alitujengea mazingira kuwa na umoja na mshikamano maiti zinazookotwa zingesababishwa na nani kwa maana wote tulikuwa tunajulikana!

Katika nchi zingine, Serikali kukiri kwa wananchi wake kuwa ndani ya nchi kuna wahalifu ambao imeshindwa kuwajua ingekuwa sawa na kusema Serikali imeshindwa kuwalinda raia wake.

Huko ni kukiri kushindwa. Ndugu Rais tumeanzisha mambo mema, makubwa karibu kila mahali lakini

huenda yalikuwa mengi mno.

Matamanio ya mioyo yetu kufanya hayo makubwa na mema yanalingana na uwezo wetu? Kusema na kutaka ni rahisi zaidi kuliko kutenda.

Hata hivyo, haiwezi kuwa ni busara pia tukaiangalia upya hali hii ili isije ikawa ni mingi na mikubwa, kwa maana muda uliobaki ni mchache mno.

Labda sasa ni wakati muafaka tukae chini tuangalie tulivyoanza na tunavyokwenda ili tupate kujua ni wapi tunakotaka kwenda.

Dunia haitilii makini kwa mambo mia mema uliyotenda. Jambo moja ovu laweza kuyafuta yote. Au kwa akili zetu nyingi au kwa ujinga wetu tumeifanya mbele yetu kuwa nyeusi tii.

Kipande kikubwa na muhimu cha kuwapo hapa tulipo tunakimaliza mwaka huu. Miaka miwili ya mwisho changamoto zake ni nyingi na kubwa.

Mwaka kesho ni pilikapilika za uchaguzi wa Serikali za mitaa. Mwaka unaofuatia kwanza siyo mwaka  mzima, ni miezi kadhaa tu ambayo kwakuwa ni uchaguzi mkuu akili yote itakuwa huko.

Hivyo mipango mikubwa na mingi tuliyoianzisha kama haikukamilika mwaka huu huko mbele ni giza nene hatutaona kitu.

Tumwombe Mungu mingine isije ikatumalizikia kwa aibu. Ndugu Rais tayari watu wengine waliishaanza kusema bandari tuliikuta na bandari tutaiacha kama tulivyoikuta.

Labda kwasababu wengine tunakaa huku shamba Mbagala hatujui flowmeter ni nini. Lakini tunajiuliza kama tumeweza kununua ndege mpya kabisa nyingi hivi hii flowmeter kama ni moja, kama ni mbili ni shilingi ngapi ambazo hatuna?

Watanzania walishuhudia mawaziri wa ‘kwenye bandari’ wakipanguliwa muda baada ya muda. Ni nani asimame ili bandari ipone? Nilikusikia baba ukiwa bandarini na kwa uchungu ulisema, ‘kwanini mnanifanya mimi nifanye kazi zenu?’

Kwa kuwa nia yako ni njema endelea kumwomba Mungu. Lakini baba watu wako wanaelewa wanapoambiwa shirika lenyewe la ndege linajiendesha kwa hasara? Si tungelifanya hili litengamae kwanza kabla ya kumwaga matrilion mengine kwenye Reli?

Hatukujua kuwa hata reli inajiendesha kwa hasara ya mabilioni? Baba unakumbuka nguvu kubwa iliyotumika katika mradi wa madawati?

Inasikitisha leo kusikia kuna shule fulani huko ukanda wa ziwa wanafunzi wanalazimika kutoka kwao na viti vya kukalia darasani.

Wananchi walisikia kuwa miezi sita ikiisha suala la madawati liwe limeisha, la sivyo mkuu wa wilaya husika naye ataisha!

Tunasikia hapa kwetu kuna madawati yamekosa madarasa. Mkubwa akiwajibu walimu waliosema shule zao hazina vitabu aliwataka wakavitafute kwenye mtandao Google!

Bila Azimio la Arusha watakaosema tulikuwa tunapuyanga wataonekana wanasema kweli!

Tuliyasikia ya Mugabe na Grace wake, Zimbabwe. Sasa tunayasikia ya Zuma wa Afrika Kusini. Tumwombe Mwenyezi Mungu yetu yasije yakatuhuzunisha!

Nia yetu njema ya kutaka kufanya mambo mengi na makubwa. Lakini je, siyo haya ambayo mzee Mwinyi aliyaita maendeleo ya vitu?

Je, isingekuwa pia ni busara kupunguza fedha kidogo kutoka katika haya matrilion tuliyopanga kutumia katika mambo hayo makubwa, tukazitumia kuliimarisha jeshi letu la polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili vipate uwezo wa kuwajua wale wasiojulikana?

Hakika hili la wasiojulikana linaweza kuja kuzaa mengi ya maumivu. Watanzania wataendelea kusikia maiti za wenzao zinaokotwa mpaka wafike wangapi?

Leo tupo katika nafasi mbalimbali. Kesho tutakuwa pia katika nafasi mbalimbali tofauti. Watoto wetu na wajukuu wetu wakijakusema wasiojulikana tulikuwa ni sisi wenyewe, tutajitetea vipi?

Giza nene limetanda mbele yetu, tunatazama lakini hatuoni; tunasikia lakini

hatusikilizi!