Ndugu Rais, watuhumiwa wa makosa ya uchochezi, tukio lililotokea wakati wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni, ambao pia ulisababisha kuuawa kwa binti yetu, Akwilina Akwilini, msiba wake ambao hautakuja kusahaulika katika nchi hii, wamepatikana na hatia na wamehukumiwa.

Tuhuma zilikuwa nzito na hukumu ilikuwa nzito pia. Lakini labda kama athari za hukumu hiyo zingejulikana kabla, Sh milioni 350 ambazo zimetozwa kama faini, zingeonekana kuwa chache sana. Hukumu hii iliumiza Watanzania wengi huku walioifanikisha wakiwa wamejijengea chuki kubwa katika vifua vya Watanzania wema wote. 

Hukumu ile imekumbusha machungu mengi ya nyuma. Ni katika mahakama ileile, kwa kesi ya aina ileile, ambapo wakoloni walimshitaki Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati akipigania demokrasia ya kweli katika nchi hii. Alihukumiwa. Aliposhindwa kulipa faini wananchi walimchangia kwa thumuni thumuni zao.

Hukumu hii ya leo imeitia doa kubwa la aibu nchi yetu mbele ya uso wa wanadamu wenye utu. Kwa hakika yaliyojitokeza kabla na baada ya hukumu hii ni fedheha kusimulia. Tunapomuachia Mwenyezi Mungu kwa hukumu yake ya haki kwa wote waliohusika, itoshe tu kusema Mungu ni mwema na ni mwema kila wakati.

Waliotoka gerezani wametoka na kitu kikubwa sana cha thamani kubwa ambacho hawakuingia nacho. Upendo mkubwa na imani kubwa ya wananchi iliyojengwa juu yao kutokana na hukumu hiyo ulioonyeshwa na Watanzania kwa walio hukumiwa hauwezi kuthamanishwa na kiasi chochote cha fedha. Ndiyo maana wenye busara wanasema Sh milioni 350 ni chache! 

Kwa miaka yote hii wako walioshindwa kujifunza kuwa Nelson Mandela alipendwa zaidi na wana wa dunia hii baada ya kutoka gerezani alikokuwa amefungwa kimabavu. Kabla ya kufungwa ni wangapi walimjua? Gereza linamuinua juu yeyote aliyefungwa kwa uonevu. Acha vyote, muombe Muumba wako akujalie kupendwa na watu.

Namkumbuka diwani fulani aliyesema anatamani afungwe japo kidogo ili sifa hiyo imsaidie kushinda ubunge katika uchaguzi ujao. Si kazi yangu kumtangaza mshindi katika chaguzi, ila kwa hesabu za mcheza bao hodari waliotoka gerezani wana haki ya kutembea kifua mbele kwa uchaguzi ujao. Na wengine nao kwa kukosa aibu wanaweza kuwa wasindikizaji.

Kwa upande mwingine, waliofanikisha katika kupatikana kwa hukumu hiyo Sh milioni 350 ni chache sana ukilinganisha na ukubwa wa kuathirika kwao. Sasa hivi wakitembea wanaonekana watupu kila sehemu. Wanakuwa kama makabati yasiyokuwa na vyombo ndani. Wakisema wanasikika lakini ni timamu gani atawasikiliza? Na wao wanatazama lakini hawaoni. Laiti wangeijua hasira iliyomo ndani ya nafsi za wananchi wema, hakika wangetamani miamba iwafukie. 

Wanasema tamaa ya madaraka ikizidi humpumbaza mtu yeyote. Ole wao kwa tamaa hiyo! Itafika siku yatawageukia. Kwao itakuwa ni kulia na kusaga meno. 

Tunaposema hakuna suluhu ya kweli nje ya maridhiano wanakuwa kama hawasikii, lakini kweli nawaambieni siku itakapo enea watayakumbuka maneno yote haya nukta kwa mkato!

Hukumu ilikuwa na maneno mengi ya kustaajabisha. Akauliza: “Kuna tatizo gani? Au nibadilishe adhabu?” Hukumu iliyofikiwa kwa misingi ya haki na adhabu yake kutolewa kwa haki, haiwezi kubadilishwa kiholela tu kwa matakwa ya mtu hata kama mtu huyo ni hakimu. 

Haki inabaki haki daima. Haki huwa haibadilishwi. Inapotolewa kauli kama hiyo na mtu mwenye mamlaka ya kutoa hukumu ni ishara kwamba hukumu iliyotolewa imetolewa kukidhi malengo tofauti ambayo hata hivyo si ya haki. Unaweza kuwa unatafuta u-DC ukapewa lakini kwa ujaji itakuwa ni kuinajisi taaluma.

Ukizingatia kuwa ni wakosaji wa mara ya kwanza na ukizingatia na muda wa miaka, ambao wamekuwa wakiutumia kuja katika usikilizaji wa kesi hii, na kwamba wengine walishafutiwa dhamana, hivyo kukaa mahabusu, hawa walianza kuitumikia hukumu yao hata kabla haijatamkwa. Wengine wanapokuja na shaka ya kutumwa unatoa sababu gani kuikataa? Kutafuta maisha kuko aina nyingi, lakini kuifanya jamii ijiridhishe kuwa umeidhalilisha taaluma yako ndiyo kujidhalilisha. Kumbe!

Niliwahurumia wote lakini mpendwa John Mnyika alikuwa wa tofauti kwa sababu nilikuwa sijawahi kumuona gerezani. Lakini sasa ajue kuwa kama ni kweli wakati mwingine neema huja na balaa, basi ni kweli pia kuwa wakati mwingine balaa huja na neema. Naye amepewa tuzo ile iliyokuwa haionekani kwake. Wale mama watatu pamoja na mwenyekiti wao sijui kama wanaiona tofauti kubwa kati ya magereza na sebule zao makwao.

Kusema wengine walishafutiwa dhamana hivyo kukaa mahabusu ni kuonyesha huruma. Nitawaepusha na adhabu ya kifungo pia ni kuonyesha huruma. Kusikia hivyo umati wa watu waliokuwapo hususan kina mama wa huruma, walilipuka kwa shangwe kwa sauti ya juu, jambo ambalo kumbe lilimkera. Akawataka wasilete mambo ya kihuni pale. Inashangaza kushangaa uchafu jalalani. Uhuni ukijibiwa kihuni kuna ubaya gani? Ajabu ya Musa kutegemea bikira kwenye chumba cha wazazi! Huu ni upepo uvumao, utapita! 

Ajue haya yakiendelea kama yanavyoendelea, nyimbo za kihoro nazo zitaendelea kusumbua fikra za Watanzania!

Mwenyezi Mungu aendelee kumbariki Jaji Mkuu wetu. Laki nina wewe baba, tambua kuwa sayansi ni somo jema, lakini kwa kazi mnazozifanya sasa somo la historia ndilo lililo muafaka zaidi. Kemea kwa unyenyekevu kuwa hakuna mahali popote katika dunia hii ambapo upanga uliwahi kuleta amani. Kufikiri mara mbili mbili kuwa ni kwa njia ya maridhiano pekee ndipo amani ya kweli hupatikana katika nchi, si ujinga.

“Akwilina, Mungu Baba, Mungu wee, Mungu wee, mweke pema Akwilina. Najaribu kuvaa viatu vya wazazi wake vinanipwaya! Ndugu jamaa na marafiki Tanzania yote tunahuzunika! Ndoto zake zimeyeyuka x 3.

Mungu mwenye haki atahukumu kwa alotenda. Sisi tunaomba upumzike salama.

Tutaonana tena oh! Akwilina upumzike salama. Inshallah Mola jalia maumivu yapate pungua kwa wazazi waliomzaa Akwilina. Alikuwa na ndoto kubwa sana ndiyo maana kwa juhudi akaamua kusoma ili aje awasaidie familia na jamii yake Tanzania.

Vijana poleni, kina mama poleni, yatapita tu. Iwe makusudi au bahati mbaya, kila kitu kina mwisho wake, kwanini tuuane? Yatapita tu. Kila nafsi itaonja mauti. Siasa zina mwisho wake.

Mungu mwenye haki atahukumu kwa alotenda tu, naomba upumzike salama. Poleni ndugu, jamaa haya yatapita. Poleni Watanzania. Tutaonana tena. Oh! Akwilina upumzike salama.”

Baba, sisi siyo wa kwanza. Tusome historia tujifunze kwa yaliyowakuta wengine!

By Jamhuri