Kwa nini Waislamu nchini wawe chini ya Bakwata? (2)

Katika sehemu ya kwanza ya makala hii nilieleza kuwa Bakwata ni chombo cha kudumu kilichoundwa mwaka 1968 kuratibu, kusimamia na kuongoza shughuli zote za Waislamu nchini Tanzania (Tanzania Bara) kwa lengo la kutekeleza wajibu wa Waislamu wa kuendeleza na kuimarisha itikadi yao ya kidini, kukuza na kuimarisha ushirikiano, umoja na udugu miongoni mwao na kwamba umma wa Kiislamu popote ulipo una wajibu mkuu wa kuwa na ‘kauli moja’ inayotafsiri umoja na mshikamano baina yao kama Allaah Mtukufu alivyowaamrisha katika Qur’aan Tukufu Sura ya 3 (Surat Ali-Imraan), Aya ya 103 kuwa: “Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni ishara zake ili mpate kuongoka.”

Pia nilieleza kuwa Bakwata kwa muundo wake unaobainishwa katika katiba yake ndiyo taasisi pekee inayotoa fursa kwa Waislamu wote kushiriki katika mchakato wa kuwachagua viongozi kwenye ngazi ya msingi ya msikiti na wawakilishi wanaokwenda kutengeneza uongozi wa ngazi ya kata, wilaya, mkoa hadi taifa.

Bakwata ndicho chombo kilicholenga kuwaunganisha Waislamu chini ya mwavuli mmoja unaosimamia uongozi wa kiroho (mabaraza ya masheikh katika ngazi ya kata, wilaya, mkoa na Baraza la Ulamaa ngazi ya taifa) na utawala, mipango, maendeleo, ustawi na fedha (halmashauri katika ngazi ya kata, wilaya, mkoa na taifa).

Bakwata inawaunganisha Waislamu ambao mwaka 1968 walikuwa wamegawanyika katika jumuiya za kimikoa kama vile Iringa Muslim Association, Arusha Muslim Union na kwamba hata Al-Jaamiatu Al-Islamiyyatu Bi-Tanganyika (Tanganyika Muslim Association) pamoja na kubeba jina la kitaifa bado ilihusika na eneo maalumu la Pwani. 

Hata East African Muslim Welfare Society ambayo ilikuwa ni muungano wa Waislamu Sunni Shafii na Mashia wa madhehebu ya Islamaailiyya (kundi la Shia linaloongozwa na Aga Khan) haikuwa ni jumuiya yenye uongozi wa wanazuoni wa Kiislamu bali ni jumuiya iliyojikita katika masuala ya ustawi wa Waislamu na maendeleo yao na ndiyo maana jumuiya hii mbali ya kuwa chini ya ulezi wa Kiongozi wa Kishia H. H. Aga Khan, Mwenyekiti wake alikuwa marehemu Tewa Said Tewa (si mwanazuoni wa Kiislamu) na Makamu wake marehemu Bibi Titi Mohamed (si mwanazuoni wa Kiislamu).

Nilitanabaisha pia kuwa Waislamu nchini wana wajibu wa kutambua nafasi yao katika Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) na namna linavyowapa fursa ya kufanya shughuli zao za kidini na kimaendeleo chini ya mwavuli wa Bakwata yenye hadhi na mamlaka ya kisheria.

Kwamba Waislamu wanapotaka kujenga msikiti, madrasa, hospitali, kitega uchumi iwe katika ngazi ya msikiti, kata, wilaya au mkoa hawana haja ya kusajili umoja wa Waislamu wa kata, wilaya au mkoa kwa kuwa tayari Bakwata imewafunika na mwavuli wa kisheria. 

Na ndiyo maana misikiti mingi hadi miaka ya 1990 haikuwa na usajili unaojitegemea, kwani ilitosha kwao kupata kibali cha Bakwata kujenga msikiti chini ya kivuli cha Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).

Ukiitafakari Katiba ya Bakwata utaona kuwa lau Waislamu wataizingatia falsafa ya Mheshimiwa Mufti na Sheikh Mkuu (Shaikhul Islaam) wa Tanzania Sheikh Abubakar bin Zubeir bin Ally Mbwana ya “Jitambue, Badilika, Acha Mazoea” wakaunganisha nguvu zao na kujenga daraja imara kati ya wasomi wa elimu ya dini na wasomi wa elimu-mazingira na kwa pamoja wakatekeleza yaliyomo ndani ya Katiba ya Bakwata kuanzia ngazi za msikiti, kata, wilaya, mkoa na taifa, wana uwezo mkubwa wa kubadilisha hali zao, na kufumba na kufumbua wakawa jamii bora yenye mchango stahiki kwa jamii yenyewe na taifa kwa ujumla.

Kwa mfano, ukiangalia katika ngazi ya msikiti kuna vyombo viwili muhimu: Kamati ya Msikiti chini ya uongozi wa Imamu wa Msikiti na Kamati ya Usuluhishi kwa ajili ya kusuluhisha migogoro yote inayowahusu Waislamu waishio katika eneo hilo lililo chini ya mamlaka ya msikiti husika.

Kwa mujibu wa Katiba ya Bakwata Ibara ya 15 (1-12), Kamati ya Msikiti itakuwa na mamlaka na madaraka yafuatayo:-

1.  Kutekeleza maagizo na maazimio ya Mkutano Mkuu wa Msikiti, kata, wilaya, mkoa na taifa.

2. Kushughulikia huduma mbalimbali za msikiti.

3. Kufanya daawa kwa Waislamu wanaoishi katika eneo la msikiti huo.

4. Kuanzisha na kuendeleza mafunzo ya dini kwa watoto na watu wazima wanaoishi katika eneo la msikiti huo.

5. Kubuni, kuendesha, kusaidia miradi ya uchumi ya msikiti, kukusanya swadaka, zaka na misaada mbalimbali kutoka kwawaumini na wahisani na kuzitia katika vitabu vya kumbukumbu za hesabu.

6. Kuanzisha na kuendesha huduma za jamii katika msikiti.

7. Kukadiria na kusimamia mapato ya msikiti.

8. Kuandaa vikao vya Mkutano Mkuu wa Msikiti.

9. Kutayarisha taarifa za utekelezaji wa shughuli za Baraza Kuu katika eneo la msikiti na kuwasilisha kwenye kikao cha Mkutano Mkuu wa Msikiti.

10. Kuweka takwimu za Waislamu wanaoishi katika eneo la msikiti.

11. Kuweka madaftari ya kumbukumbu za mali za Baraza zinazohamishika na zisizohamishika zinazohusika na msikiti.

12.  Kupokea taarifa za usuluhishi na kuzifanyia kazi.

Ukizingatia yaliyoelezwa kama dira ya utendaji wa Kamati ya Msikiti utaona kuwa yakitekelezwa vilivyo yanaleta umoja wa Waislamu wa eneo lote la msikiti, kwa kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Msikiti kwa mujibu wa Katiba ya Bakwata Ibara 18 (4) ni waumini wote wanaoishi katika eneo la msikiti huo na kuswali katika msikiti huo.

Pia kwa mujibu wa Katiba ya Bakwata Ibara 20 (1-10), Mkutano Mkuu wa Msikiti ambao wajumbe wake, kikatiba, ni waumini wote wanaoishi katika eneo la msikiti huo na kuswali katika msikiti huo una mamlaka na madaraka juu ya mambo haya yafuatayo:-

1. Kupokea taarifa ya uteuzi wa Imamu wa msikiti kama ulivyofanywa na Baraza la Masheikh la Wilaya.

2. Kumchagua katibu wa msikiti.

3. Kumchagua muweka hazina.

4. Kuwachagua wajumbe wawili wa kuingia katika Mkutano Mkuu wa Kata.

5. Kuwachagua wajumbe watano (5) wa usuluhishi wa migogoro katika msikiti.

6.  Kupokea na kuzingatia taarifa ya Kamati ya Msikiti juu ya shughuli za Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania katika eneo la msikiti.

7.  Kupokea na kuzingatia taarifa za mapato na matumizi ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) katika eneo la msikiti.

8.  Kumsimamisha Imamu wa msikiti pale itakapodhihirika kuwa matendo na tabia zake havilingani na Qur-aani na Sunna wala na maadili ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA), na kupeleka mbele maazimio hayo katika kikao cha Baraza la Masheikh la Kata na baadaye katika Baraza la Masheikh la Wilaya kwa uamuzi.

9. Kumwachisha uongozi kiongozi yeyote wa msikiti, isipokuwa Imamu pale itakapodhihirika kwamba vitendo vyake au tabia yake havilingani na madhumuni na maadili ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA).

10. Kuweka mipango madhubuti ya utekelezaji wa shughuli za Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) katika eneo lililo chiniya mamlaka ya msikiti.

Nihitimishe kwa kusisitiza kuwa ni dhahiri Waislamu nchini wanajirudisha wenyewe nyuma kwa kutojua nafasi ya Bakwata, ambayo kwa katiba yake ni nyezo ya kuwaleta pamoja kwa masilahi ya dini yao na ustawi wao. 

Kila wanachokitaka, ikiwemo kujua idadi yao, kupanga mipango yao, kudhibiti nidhamu ya uendeshaji wa chombo chao, tayari kimo ndani ya Katiba ya Bakwata, iliyo bora kuliko katiba ya taasisi yoyote ya Kiislamu nchini. 

Kwa nini sasa mambo hayaendi? Ni kwa kuwa Waislamu hawajatekeleza wajibu wao kuanzia ngazi ya chini ya msikiti ambayo ndiyo yenye watu na kwamba baadhi ya Waislamu wameshindwa kung’amua siri ya Waislamu kuwa chini ya chombo kimoja kinachotafsiri umoja na mshikamano baina yako kama walivyotakiwa na Qur’aan Tukufu Sura ya 3 (Surat Aali-Imaraan) Aya ya 103.

 Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).

Simu: 0713603050/0754603050