Kama utasababishiwa hasara yoyote, basi mtu anayekusababishia hasara hiyo ana wajibu kisheria kukufidia, isipokuwa kama umeamua kusamehe, au kama hasara hiyo ilitokana na mchakato ambao haukuwa halali kisheria. 

Katika kufafanua suala hili, makala ya leo itajikita katika Sheria ya Mikataba Sura ya 345 ambayo kimsingi ndiyo inayotoa ufafanuzi kuhusu jambo hili.

Tutaliangalia hili kwa ujumla wake kupitia mafungu matatu. Kwanza, kukataa kufidiwa; pili, kukubali kufidiwa, na tatu, mambo yanatotakiwa wakati wa kufidiwa.

 Kukataa kukufidia

Yumkini mtu aliyesababisha hasara anaweza kukataa kukulipa au kufidia hasara aliyoisababisha kwako. Ikiwa hili litatokea na wewe unahitaji kufidiwa, basi yafaa umwandikie taarifa ya kumtaka kukufidia mara moja. 

Itapendeza zaidi iwapo taarifa hii ikiandikwa kupitia kwa wakili na kwa anuani ya wakili huyo. Lakini hii haimaanishi kuwa wewe hauwezi kuandika. Hata wewe mwenyewe waweza kuandika na kuipeleka ikiwa na anwani yako.

Taarifa itapaswa kueleza kile alichotenda, hasara iliyosababishwa na hilo tendo lake, kumtaka afidie hiyo hasara, siku au muda ambao unampa afidie hiyo hasara, na hatimaye hatua ambazo utazichukua iwapo atashindwa kufidia hiyo hasara ndani ya muda uliompa. 

Kwa kawaida, unaweza kumpa siku saba, siku 14, siku 30, siku 45, au muda wowote kadiri ambavyo unaona unafaa na kutosha kumwezesha kulipa fidia hiyo. Na utaeleza pia kitu ambacho utafanya/hatua utakazochukua ikiwa atashindwa kukulipa. 

Kwa kawaida, hatua ambazo unaweza kuzichukua iwapo unayemtaka akufidie atashindwa kufanya hivyo huwa ni kumfikisha mahakamani. Usije ukamdhuru, au kumfanya kitu kingine chochote ambacho hakimo katika utawala wa sheria. Ukifanya hivyo, wewe ndiye utajiingiza matatizoni, kwani utakuwa umefanya jinai.

Basi, ikiwa kweli muda huo umekwisha na huyo mtu hajakufidia au kukuita katika mazungumzo ya kujadiliana kuhusu barua yako ya kudai fidia, basi unaweza kutimiza azima yako ya kumfikisha mahakamani. 

Kumfikisha mahakamani maana yake ni kufungua mashitaka ambayo yataitaka mahakama itoe amri ya kumlazimisha kukulipa fidia kutokana na hasara aliyoisababisha. 

Kumbuka kuwa utakapolifikisha suala hili mahakamani, malipo yanaongezeka, kwa sababu utajumuisha pia na gharama za kesi katika hesabu ya malipo anayopasa kulipa. Hivi ndivyo unavyoweza kumlazimisha aliyekataa.

2. Kukubali kulipa fidia

Kukubali kulipa fidia kupo kwa aina mbili. Kwanza, kukubali kwa maandishi, ambapo mtuhumiwa ataonyesha kukubali kuwa amesababisha hasara na kuweka ahadi ya kulipa. Pili, kukubali tu kwa mdomo kuwa mtuhumiwa amesababisha hasara hivyo atalipa. 

Kwa mujibu wa Kifungu cha 10 cha Sheria ya Mikataba, makubaliano ya mdomo ambayo hayako katika maandishi nayo ni mkataba halali kisheria.

Kwa hiyo, iwe ameahidi kulipa hasara kwa maandishi au kwa mdomo, bado yote ni makubaliano na yanakubalika kisheria. Lakini pia ile ahadi pekee ambayo huyu aliyesabababisha hasara ataitoa kwa yule aliyemsababishia hasara nayo ni mkataba kamili kisheria. Ahadi tu, yaani ile kutamka tu kuwa nitakulipa au nitakufidia, tayari ule ni mkataba tosha na yafaa utekelezwe.

3. Mambo ambayo yanatakiwa kufidiwa

Mambo haya ni kwa mujibu wa Kifungu cha 77 cha Sheria ya Mikataba. Kwanza, ni uharibifu wa aina yoyote ikiwa upo. Pili, ni gharama ambazo umetumia wakati unahangaika na huyo mtu mpaka kufikia makubaliano naye. Pengine ulimtafuta, ulifungua kesi, ulitumia nauli, ulipiga simu na kila aina ya gharama ambayo uliingia wakati unashughulikia suala lake anapaswa kukulipa fidia. 

Tatu, ni malipo mengine ambayo mtakubaliana, au yalikuwa yamekubaliwa katika ule mchakato wa mwanzo aliouharibu. 

Hivi ndivyo unavyoweza kufidiwa hasara.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.

By Jamhuri