Maisha ya Mkristo ni maisha ya mapambano kwa saa 24. Ukristo si lelemama. Ukristo ni vita. Ukristo una gharama. Hakuna Ukristo laini. Hakuna Ukristo wa kununua wala kuuza. Kumbuka kwamba utakatifu wako hauko kwenye vyeti vyako vya ubatizo. Utakatifu wako uko katika matendo yako yanayompendeza Mungu na wanadamu.

A.W. Tozer aliandika: “Unapobatizwa usilegeze kamba yako ya Ukristo, ukiilegeza shetani atainyakua, na akiinyakua utabaki na majeraha yasiyoponyeka.”

Sali ili uiokoe roho yako. Kila wakati tembea kwenye kusudi la Mungu. Mungu ana mpango na wewe. Anataka jambo kubwa litokee kupitia wewe.  Anataka atukuzwe kupitia wewe. Wewe ni mpakwa mafuta wa Bwana.  Una upako wa ajabu.

Uwepo wako duniani si ajali ya kibaiolojia, bila kujali mazingira yaliyozunguka kuzaliwa kwako. Uko hai kwa sababu ya umwilishwaji wa ki-Mungu uliopitia kwa wazazi wako. Kutungwa kwako mimba na kuzaliwa kwako ni uthibitisho kwamba, Mungu ana mpango na wewe.

Usijutie kuwa miongoni mwa wanafamilia wa kibinadamu wanaoishi katika sayari hii ya dunia. Jambo moja na la muhimu ambalo kila mtu anapaswa kulifahamu ni kwamba Mungu anatutaka tuishi maisha ya sala ili tujiokoe na hila za yule mwovu.

Tabia ya maisha ni kwamba wakati wote maisha yanamtaka mwanadamu aishi kama Mungu. Tunapata ajali maishani pale tunapompa Mungu nafasi ya pili. Usiishi kama unavyotaka uishi, bali ishi kama Mungu anavyokutaka uishi. Mwanadamu ana tabia ya kumsahau Mungu wakati wa furaha na kumkumbuka wakati wa taabu.

Mwana mpotevu anayezungumziwa na Maandiko Matakatifu alimsahau Mungu wakati alipokuwa na furaha ya mali za kidunia. Alipoishiwa mali aliyokuwa nayo na kutengwa na marafiki zake wa karibu waliokuwa wakiponda naye starehe za kidunia, alimkumbuka Mungu. Alisema: “Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia… sistahili kuitwa mwana wako tena, nifanye kama mmoja wa watumishi wako.” (Lk 15:18-19).

Huyu mwana mpotevu kuna wakati alikuwa ameajiriwa kama kibarua wa kulisha nguruwe baada ya kuwa amemaliza mali ya urithi aliyokuwa amegawiwa na baba yake. Bila shaka wakati akiwa anawalisha wale nguruwe alikuwa anazungumza nao na kuwaambia habari ya utajiri wa baba yake. Ni kama aliwaambia: “Msinione nawalisha hapa, kwetu kuna utajiri, kuna wafanyakazi wengi wanaofanya kazi kama hii ninayoifanya hapa.” Ninafikiri kama nguruwe wale wangekuwa na uwezo wa kuongea wangeweza kumuuliza swali hili: “Kama kwenu kuna utajiri wa namna hiyo, hapa unafanya nini? Unastahili kuwapo hapa?”

Binafsi nimeshuhudia na kuona katika maisha yangu kwamba, pale nilipokuwa na mahusiano mabaya na Mungu maisha yangu yaliyumba na kupata mtikisiko wa ajabu. Maisha yako yote yatumie katika kumtumikia Muumba wako. Unapopata mafanikio ya kiroho, kifamilia, kiuchumi, kimaadili na kiuongozi usimsahau Mungu. Kila dakika ya maisha yako itumie kusali.

Bila Mungu maisha yako hayana maana. Bila Mungu mafanikio yako hayana maana. Bila Mungu afya yako haina maana. Bila Mungu ndoa yako haiwezi kuwa salama. Bila Mungu kazi yako haiwezi kuwa salama. Bila Mungu usingekuwepo. Itambue nafasi ya Mungu katika maisha yako. Ifundishe akili yako kumpenda Mungu. Ufundishe moyo wako kumpenda Mungu.

Kila siku Mungu anakusubiri umweleze mafanikio yako na misukosuko yako. Mweleze Mungu unachohitaji katika maisha yako. Hakuna wa kuweza kukuliwaza katika dunia hii zaidi ya Mungu wako aliyekuumba kwa sura na mfano wake.

Vuta hisia na kumbukumbu mbalimbali. Kumbuka ni magumu mangapi umekumbana nayo katika maisha yako. Je, ni nani alikuvusha katika magumu hayo? Unavuta hewa ya nani mpendwa? Unakunywa maji ya nani mpendwa? Unaishi kwenye ardhi ya nani mpendwa? Nani aliyewaumba wazazi wako? Nani aliyekuumba? Nani amekupa mume au mke? Zungumza na Mungu kwa njia ya sala.

Kiongozi wa zamani wa India, Mahatma Gandhi, alipata kutumia kalamu yake kushuhudia hivi: “Sala imeokoa maisha yangu. Bila kusali ningekuwa kichaa zamani. Katika maisha yangu yametukia magumu na machungu yaliyonikatisha tamaa, kama niliweza kujitoa kutoka katika hali hiyo ilikuwa ni kwa nguvu ya sala.”

Daktari bingwa wa magonjwa ya akili ya binadamu, Alexis Gabriel, anathibitisha nguvu ya sala kwa kusema: “Mimi kama daktari nimeshuhudia wagonjwa wengi wenye shinikizo la damu na mfadhaiko wakipona kwa nguvu ya sala wakati ambapo dawa za hospitalini zilishindwa kufanya kazi hiyo kwa wagonjwa.”

Je, unahangaika na magonjwa? Sali. Je, ndoa yako ina misukosuko? Sali. Je, umeshindwa kumsamehe aliyekukosea? Sali. Je, umedhulumiwa haki yako? Sali. Safari ya maisha ya mwanadamu haiwezi kuwa salama bila sala. Ongoza maisha yako kwa sala. Mungu wetu mwema, muumbaji na mkombozi wetu anazungumza nasi kwa njia ya sala.

608 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!