Je, unashangaa?

Ishi maisha ya kushangaa na kuchukua hatua. Dawa ya makosa yetu ni kufanya toba, kufunga, ukarimu na kusali. 

Matendo hayo yote yanaanza na kushangaa. Ni matendo ambayo Wakatoliki wanapaswa kufanya kipindi cha siku arobaini. Je, unashangaa mahali ulipo? Mt. Bernardo kila asubuhi alijiuliza: “Bernardo, Bernardo kwa nini uko hapa?” Je, unaishangaa barabara ambayo umeichukua? Je, unaishangaa milango ambayo imefungwa mbele yako? Je, unamshangaa Mungu? Kama umewahi kushangaa kwa nini mambo mabaya yanawapata watu wema ni kwa sababu wanaweza kuyakabili. Je, unashangaa kama Mungu anakujua? Jibu, si kwamba anajua jina lako, bali matendo yako na historia yako. Biblia imeshajaa washangaaji. Neno shangaa limerudiwa mara 148 katika Biblia. 

Kushangaa ni mwanzo wa kufikiri na kutafakari. “Kufikiri kote kunaanza na  kushangaa,” alisema Socrates. Kuna mwanafalsafa wa Kigiriki aliyesema: “Mtu alishangaa ni kama miwani ambayo nyuma yake hakuna jicho.” Dk. Seuss alisema: “Fikiri na shangaa, shangaa na fikiri.” Kutafakari ni kushangaa. Mtoto kwa mshangao alimuuliza mama yake: “Kwa nini uliolewa na dadi?” Mama yake alijibu: “Ee! Unashangaa kama ninavyoshangaa.” Huu ni mwanzo wa kufikiri na kutafakari. Bwana wetu Yesu Kristo alipomwomba mwanamke Msamaria maji ya kunywa, mwanamke Msamaria alishangaa: “Je, wewe uliye Myahudi, unaniomba mimi niliye mwanamke Msamaria maji ya kunywa?” (Yohane 4:9). Wayahudi hawakuwa na ushirika na Wasamaria. Mwanamke Msamaria alikuwa ‘mtu wa nje’ kama Msamaria. Tuishangae misemo inayotutenga na tuchukue hatua: mtu wa ndani na mtu wa nje; mwenzetu na si mwenzetu; sisi na wao; makwetu na si makwetu. Ukishangaa na kuchukua hatua utagundua baba yetu ni mmoja – Mungu, na sisi ni wana wa Adamu, yaani binadamu.

Kushangaa ni mwanzo wa kubadilika kiroho. “Watu huenda  nchi za nje kushangaa urefu wa milima, mawimbi makubwa ya bahari, urefu wa mito, upana mkubwa wa bahari, mwendo wa duara wa nyota na wanajipita bila kujishangaa,” alisema Mt. Augustino wa Hippo. 

Mwanamke Msamaria alishangaa Yesu alipomwambia: “Ulikuwa na wanaume watano, na yeye uliye naye sasa mume wako.” (Yohane 4: 18). Mwanamke huyu hakuwa huru na hakuwa na amani. Alikwama. Kupenda kwake sita kijasho kilimtoka. 

Mwanamke aliacha mtungi wake. Mwanamke huyu kwa kuacha mtungi wake aliacha shida zake, aliacha aibu yake, aliacha vidonda vyake. Aliacha ukabila, utumwa, ukosefu wa amani, hofu na aibu. 

Alibadilika kiroho. Mtoto mmoja alikuwa anavaa nguo zake kwenda kanisani. Alimuuliza mama yake kwa sauti ya juu aliyekuwa chumba cha karibu: “Mama shati langu hili ni chafu?” Mama yake bila kuliona alisema: “Ndiyo, ni chafu; vaa shati jingine ambalo si chafu.” Baada ya kuvaa shati safi alimuuliza mama yake: “Ulijuaje kama shati ni chafu bila kulitazama?” Mama yake alimjibu: “Kama lingekuwa safi, ungejua na usingeniuliza. Kumbuka, kama linakutia shaka na mshangao ni chafu.” Mwanamke Msamaria maisha yake yalimtia shaka na mshangao. 

Kushangaa ni mwanzo wa kujifunza. Usiache kushangaa. Mwanamke Msamaria alimuuliza Yesu:  “Bwana, hauna chombo cha kutekea, na kisima ni kirefu; utapataje maji ya uzima?” (Yohane 4:11). Yesu hakuongelea maji ya kawaida. Aliongelea kiu ya kumpata Mungu. Mt. Augustino alisema:  “Hatutulii, tutatulia katika Mungu.” Mioyo yetu ina tundu ambalo linaweza kujazwa na Mungu. Mtoto akililia maziwa usimpe vitu vya kuchezea. Binadamu anapomtafuta Mungu mali haitatuliza kiu yake.

By Jamhuri