Tume Huru ya Uchaguzi nchini (2)

Narudia kutamka kuwa tangu Watanzania tuwe huru mwaka 1961 (Tanganyika) na mwaka 1964 (Zanzibar) tumefanya uchaguzi kitaifa kila baada ya miaka mitano na kuwapata viongozi bora katika ngazi ya urais, ubunge na udiwani.

Chombo kilichofanya uratibu, usimamizi na uendeshaji wa uchaguzi nchini ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa mujibu wa Katiba. Chombo hicho kimefanya kazi zake vizuri na kwa ufanisi mkubwa.

Watanzania tunapotaka tuwe na Tume Huru ya Uchaguzi maana yake tuwe na viongozi na watendaji huru katika sakafu ya nafsi na mioyo yetu. Kauli na matendo ya watu yaonyeshe uhuru wa nafsi na mioyo. Mambo yanayohitaji utu na ari.

Tunapozungumzia Tume Huru ya Uchaguzi ni vema kufahamu maana ya maneno huru, tume na uchaguzi. Tume ni kikosi cha watu walioteuliwa kwa ajili ya kufanya shughuli maalumu, kama vile haki za binadamu, uchaguzi n.k.

Tunaposema huru tunamaanisha kutokuwa na shinikizo, kwa maana ya ulazimishaji wa kufanyika kwa jambo, kama vile shurutisho au chagizo. Kiungo cha neno Tume na Uchaguzi ni neno huru ambalo ndiyo moyo wa chombo chenyewe.

Uchaguzi ni upigaji kura kwa lengo la kumpata kiongozi au mwakilishi wa eneo, taasisi, kampuni au serikali. Katika nchi huru kama Tanzania inayofuata misingi ya haki, usawa na demokrasia, uchaguzi haukwepeki. Ndiyo maana mwaka huu 2020 tunajiandaa kumchagua rais, wabunge na madiwani watakaotuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Tusidai au kutaka Tume Huru ya Uchaguzi tukiwa na hoja ya kubadili tume ikiwa ni mtindo. La hasha. Tume Huru ya Uchaguzi ni dude tu. Tume tunayoitaka kiwe chombo cha kuratibu, kusimamia na kuendesha shughuli za uchaguzi, chini ya misingi na kanuni za uaminifu, uadilifu na haki.

Asili na maana ya Tume Huru ya Uchaguzi haina budi kutokana na wananchi wenyewe kuwa huru katika nafsi na mioyo. Mteuzi au wateuzi wa tume, wajumbe wa tume kadhalika wawe huru. Watendaji au watumishi wa tume nao wawe huru. Haitakuwa na maana kutaka Tume Huru ya Uchaguzi wakati hatupo huru.

Huru ya mtu inaanzia ndani ya nafsi na moyo wa mtu mwenyewe, kutoa kauli itakayosema ukweli na itakayodhihirishwa na matendo yaliyojaa uaminifu na uadilifu mbele ya wananchi. Wananchi nao kwa mtazamo wao watakiri, naam, huyu ni mwaminifu na mwadilifu.

Tume za Uchaguzi zilizopita hazikuwa na neno huru, lakini ziliweza kufanya kazi zao vizuri na zilitupatia viongozi. Ni kweli wakati fulani hapa na pale zilitetereka na kutia walakini kutokana na tabia ya mwanadamu. Hapa penye tabia ndipo penye mtihani, hata kutaka tume huru ya uchaguzi.

Ni matarajio yangu madhali mamlaka kuu ya nchi imewatangazia Watanzania Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu utakuwa huru na wa haki, ni dhahiri sifa, masharti na taratibu za uchaguzi huru zitazingatiwa na zitafuatwa.

Ifahamike Tume ya Uchaguzi yoyote inapaswa kuwa huru kutokana na wateuzi wa tume, wajumbe wa tume, watumishi wa tume na wapiga kura (wananchi) wawe huru. Iwapo makundi haya si huru, tume haitakuwa huru.

Neno huru siyo sifa, kigezo au shahada ya tume ya uchaguzi kuwa huru, hata kama neno huru lina rangi ya dhahabu au ni lulu, haifanyi tume kuwa huru. Ninasisitiza nafsi na moyo wa mtu katika tume ikiwa huru, tume itakuwa huru.

Watanzania tusitokwe mishipa ya shingo na sauti kujaza mwangi anga ya Tanzania kwa kulalama kutaka tume huru ya uchaguzi, ama sivyo tutasusia uchaguzi wa mwaka 2020, ilhali wanaharakati, wanasiasa na wengineo hatupo huru. Tutafakari, Tume Huru ya Uchaguzi maana yake nini?